Dodoma. Wananchi 1,113 wamepoteza maisha kutokana na ajali zilizosababishwa na pikipiki maarufu bodaboda katika kipindi cha 2022 hadi 2024, Bunge la Tanzania limeelezwa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo ametoa takwimu hizo bungeni jijini Dodoma leo Jumanne Februari 11, 2025 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Fatuma Hassan Toufiq.
Mbunge huyo ameuliza ni wananchi wangapi wamepoteza maisha kutokana na ajali za pikipiki kati ya mwaka 2022 hadi 2024.
Katika swali la nyongeza Toufiq ameuliza ni mkakati gani wa kuwadhibiti madereva wa pikipiki ambao wamekuwa na utaratibu wa kupakia abiria zaidi ya mmoja (mishikaki) ambao ajali ikitokea huweza kupoteza maisha wote.
Naibu Waziri amesema kati ya wananchi hao madereva wa pikipiki waliopata ajali na kufariki dunia ni 759, abiria waliopanda pikipiki na kupata ajali zilizosababisha vifo vyao ni 283.
Kwa upande wa wananchi waliokuwa wanatembea kwa miguu kandokando ya barabara au njiani, ama walikuwa wanavuka barabara na kupata ajali ya kugongwa na pikipiki na kufariki dunia ni 71.
“Nitoe wito kwa madereva wote wanaoendesha pikipiki kuzingatia sheria ya usalama barabarani ili kupunguza ajali zinazoathiri wananchi wengi na kupunguza nguvu kazi katika Taifa letu,” amesema Sillo.
Sillo amewataka madereva wa pikipiki kuzingatia sheria za usalama barabara ikiwemo kutopakia abiria zaidi ya mmoja na akamwagiza Kamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani kuliangalia jambo hilo.
Wakati Sillo akieleza hayo, takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania – Kikosi cha Usalama Barabarani ajali zilizorekodiwa kati ya 2019 na 2023 zilikuwa 10,174 sawa na wastani wa ajali 2035 kila mwaka.
Takwimu hizo zilionyesha zaidi ya nusu za ajali (asilimia 53) zilisababisha kifo cha angalau mtu mmoja na angalau mtu mmoja alijeruhiwa kwenye kila ajali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya polisi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita watanzania wanne hadi watano walifariki kila siku kutokana na ajali za barabarani wakati wengine saba hadi wanane walijeruhiwa kila siku.