Dar es Salaam. Wakati Nigeria na Kenya zikiongoza kwa kupokea kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa raia wao walioko ughaibuni (Diaspora), Tanzania imezindua ripoti ya kufuatilia fedha hizo zinazoingia nchini kutoka kwa raia wake wanaoishi nje.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba ameongoza uzinduzi wa Ripoti ya Ufuatiliaji wa Fedha zinazoingia katika nchi kutoka kwa Watanzania wanaoishi ughaibuni (Cross-border Remittance Diagnostic) jana Februari 10, 2025 kwa ajili ya kustawisha sekta ya fedha nchini.
“Nalishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) kwa msaada wake wa kiufundi katika kufanya utafiti ambao una mchango mkubwa katika kustawisha sekta ya fedha nchini.
“Fedha hizi (remittance) zinaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kufadhili maendeleo ya muda mrefu kupitia majukwaa mbalimbali ya uwekezaji, kubadilishana uzoefu na teknolojia, kuboresha mapato ya kaya, na kusaidia maendeleo ya jamii kwa ujumla,” amesema Tutuba.

Ameongeza kuwa michango hii inaunga mkono moja kwa moja Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya Tanzania, hasa katika kupambana na umaskini, njaa, kuboresha huduma za afya, elimu bora, maji safi na salama, ajira, ukuaji wa uchumi pamoja na kuleta usawa.
Pia, ameeleza kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali za kisera ili kuongeza kiwango cha malipo ya fedha zinazoingia nchini kupitia Watanzania waishio ughaibuni.
“Hatua hizo ni pamoja na kuanzishwa kwa Mfumo wa Malipo ya Kielektroniki ya Mipaka (Cross-border Payment System) kwa lengo la kuunganisha mifumo ya malipo nchini na mifumo ya malipo ya kimataifa na kikanda na mabadiliko katika Kanuni za Akaunti za Nje za 2022 (Foreign Account Regulations, 2022) ambazo zimewaruhusu Watanzania waishio nje kuwekeza katika dhamana za Serikali,” amesema Tutuba.
Wakati Tanzania ikijipanga hivyo Taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu mwenendo wa uhamiaji duniani (KNOMAD, 2024) inaonesha kuwa kufikia Desemba 2023, Diaspora wa Nigeria walituma kiasi cha Dola bilioni 19.5 kwa nchi hiyo, ikiwa ndio kiwango kikubwa zaidi barani Afrika. Kiasi hiki ni zaidi ya robo ya jumla ya dola bilioni 54 zilizopokewa na nchi 49 za ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Mtaalamu wa uchumi, Rashid Aziz amesema sababu ya Nigeria kuwa na takwimu kubwa za fedha hizo za Diaspora ni idadi yao kubwa nje ya nchi yao.
“Sababu kubwa ni kuwa na idadi ya raia wengi wanaoishi au kufanya kazi nje ya nchi, wanaweza kuwa raia wa Nigeria au wenye asili ya nchi hiyo. Miongoni mwao wapo wenye ujuzi wa kitaalamu ambao wamepata nafasi katika soko la ajira ughaibuni.
“Kwa Afrika, michango ya diaspora ni muhimu sana na inaweza kuzidi kiasi cha mikopo au misaada ya kimataifa kwa mwaka. Kwa mfano, nchini Nigeria, mwaka 2022, fedha zilizotumwa na Diaspora zilifikia Dola bilioni 25, sawa na asilimia 6.1 ya Pato la Taifa (GDP). Kwa ulinganisho, kiwango hiki kilikuwa kikubwa zaidi kuliko jumla ya fedha za uwekezaji wa kigeni (FDI) na misaada,” amesema Aziz.