Dar es Salaam. Kuendelea kuwapo kwa tozo za Serikali na makato katika miamala ya kifedha, ikiwemo ile inayofanywa kwa simu, kumetajwa kuwa sababu ya gharama za matumizi ya fedha kidigitali kuwa juu.
Hali hii pia imetajwa kuchelewesha ujumuishaji wa kifedha na matumizi ya malipo ya kidigitali, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira mazuri ya kuvutia watumiaji wengi zaidi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Silcom Microfinance, Leonard Mususa amesema licha ya huduma za kifedha kidigitali kuwezesha urahisi wa biashara na miamala, gharama zake bado ni kubwa.
“Licha ya mapinduzi ya huduma za kifedha kwa simu, bado gharama ziko juu. Kuna gharama zinazotokana na kampuni husika na pia kodi. Ukikokotoa gharama za kulipa kwa simu au benki kidigitali, utaona sehemu kubwa ni gharama za kampuni na sehemu nyingine kubwa ni kodi, haya mawili yanafanya gharama iwe juu,” amesema Mususa katika uzinduzi wa Selcom Fedha uliofanywa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, Februari 11, 2025.
Mususa ameongeza kuwa Serikali inasaidia kampuni mbalimbali zinazotoa huduma za kifedha kupunguza gharama kwa kuwezesha Mfumo wa Malipo wa Haraka (TIPS), ambao unarahisisha na kuharakisha uhamishaji wa fedha kati ya watoa huduma.
“Tunaendelea kuboresha na kupunguza gharama za miamala. Zamani kutuma muamala mmoja kuligharimu hadi Sh10,000, lakini sasa gharama zimepungua sana. Selcom Fedha imekuja na makato nafuu kwa ajili ya Watanzania,” amesema Mususa.

Ameongeza kuwa lengo la Selcom Fedha ni kuhakikisha ujumuishaji wa kifedha unakuwa wa kweli kwa kila Mtanzania, na si tu ndoto. Pia, kampuni hiyo inalenga kutoa mikopo rahisi na nafuu kwa muda mfupi kusaidia Watanzania kutatua changamoto zao za kifedha.
Kwa upande wake, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, amesema uzinduzi wa Selcom Fedha unaendana na dhamira ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya huduma za kidigitali.
“Lengo ni kuona gharama za miamala zinaendelea kushuka na kuwafikia wananchi wote, hasa wale walioko pembezoni. Tunataka matumizi ya fedha taslimu yapungue na watu wategemee huduma za kidigitali. Uzinduzi wa Selcom Fedha umekuja kwa wakati muafaka na unatarajiwa kuleta mapinduzi katika sekta ya fedha kidigitali,” amesema Tutuba.
Aidha, amebainisha kuwa BoT iko katika hatua ya tatu ya maboresho ya mfumo wa TIPS, ambao utawezesha malipo kwa kutumia QR Codes, kabla ya kuingia katika hatua ya nne ambayo itawezesha matumizi ya kadi za taifa.
“Mfumo wa TIPS ni mojawapo ya mikakati ya serikali kuhakikisha utumaji wa fedha na malipo unakuwa rahisi, haraka, na nafuu kwa kila Mtanzania. Tunagharamia mfumo huu kama Benki Kuu ili watumiaji wabaki na gharama zao za uendeshaji pekee,” alisema.
Kwa mujibu wa utafiti wa Finscope 2023, huduma za kifedha rasmi zilifikia asilimia 76 mwaka 2023, huku serikali ikilenga kufikisha asilimia 85 ifikapo mwaka 2028.