KIKOSI cha Yanga jana jioni kilishuka uwanjani kuvaana na JKT Tanzania katika mechi ya Ligi Kuu Bara, lakini kipa namba moja wa kikosi hicho, Djigui Diarra alikuwa anaumiza kichwa kwa alichokifanya dakika 1080 zilizopita sawa na mechi 12 alizocheza.
Diarra ambaye huu ni msimu wa nne anacheza Ligi Kuu Bara, kabatini ana tuzo mbili za kipa bora wa Ligi Kuu Bara, lakini sasa ni kama ufalme wake unakwenda kukumbana na upinzani mkali kwa msimu wa pili mfululizo baada ya ujio wa Moussa Camara anayecheza Simba.
Rekodi zinaonyesha Diarra ambaye alibeba tuzo za kipa bora wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo akimaliza utawala wa Aishi Manula aliyebeba mara sita mfululizo tangu akiwa Azam kabla ya kutua Simba 2017, ana kazi ya ziada kufanya msimu huu.
Diarra msimu huu kwenye ligi amecheza mechi 12 kati ya 17 na kuruhusu mabao sita wakati kikosi chake kikiwa kimeruhusu saba. Mawili amefungwa Khomeny Abubakar aliyedaka mechi tatu dhidi ya Coastal Union na Namungo alizoondoka na clean sheet huku dhidi ya Mashujaa akiruhusu mawili Yanga iliposhinda nyumbani 3-2.
Aboutwalib Mshery amecheza mechi tatu dhidi ya Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Fountain Gate ambazo zote ana ‘clean sheet’.
Katika mechi 12 za Diarra, ameondoka uwanjani mara nane bila ya nyavu zake kutikiswa ‘clean sheet’ kitu ambacho anaumiza kichwa kufikia rekodi ya msimu uliopita alipomaliza na 14 sambamba na kumfikia Camara anayeongoza.
Camara aliyecheza mechi 17 za ligi sawa na dakika 1530 na kukusanya clean sheet 13, amebakiwa na clean sheet mbili kuifikia rekodi ya msimu uliopita iliyowekwa na Ley Matampi akiwa Coastal Union. Kipa huyo kutoka Guinea naye amefungwa mabao sita kama Diarra.
Matampi aliyecheza mechi 24 kati ya 30 kwa dakika 2160, alimpiku Diarra clean sheet moja baada ya kucheza mechi 21 kwa dakika 1846.
Camara ambaye huu ni msimu wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara ana nafasi ya kuweka rekodi mpya ya clean sheet kutokana na kubaki mechi 13 kabla ya kumaliza msimu huu huku akiwa chaguo la kwanza.
Mbali na kukimbizana clean sheet wawili hao wanaozipambania timu zao kuwania taji la ligi, kila mmoja ana upungufu wake ambao wapinzani wanautumia vizuri kuwaadhibu na hiyo inaweza kuwa shida kwao katika kufukuzia rekodi.
Makipa hao wa kisasa wamekuwa wakiruhusu mabao ya kufanana kwa mashuti ya mbali kitu ambacho kimeonekana kuwatesa sana. Wakati vita yao ya ‘clean sheet’ ikiwepo, pia kila mmoja anapambana asiruhusu mabao mengi. Diarra ameruhusu matano na Camara sita.
Msimu huu Diarra katika mabao matano aliyoruhusu kati ya saba ya Yanga, mawili ni kwa mashuti ya mbali kutoka kwa Offen Chikola wa Tabora United wakati Yanga ikifungwa 3-1 na Seleman Bwenzi wa KenGold siku ambayo Yanga ilishinda 6-1.
Camara naye mabao sita aliyoruhusu ukiachana na lile ambalo winga wake, Ladack Chasambi alimrudishia mpira wa mbali, pia alifungwa mawili na nyota wa Coastal Union, Abdallah Hassan na Hernest Malonga katika sare ya 2-2. Ubora wao unavyozungumzwa na aina ya mabao ya kufanana waliyoruhusu, inaibua maswali ikiwemo kujiamini kupitiliza.
Aliyekuwa kipa wa Simba huku pia akiwahi kuwanoa makipa wa timu hiyo, Idd Pazi ‘Father’ alisema makosa wanayofanya Diarra na Camara yanatokana na kujiamini kupitiliza wakisahau udhaifu wao unaweza kuwaadhibu.
“Selemani Bwenzi wa KenGold alimwangalia Diarra na akagundua ameshatoka eneo analotakiwa kukaa, kisha akapiga shuti. Sasa Diarra baada ya kurudi upande upande akawa anarudi kinyumenyume ndio maana akausukumia ndani ya nyavu, ila angekuwa upande angeusukumia nje,” alisema mkongwe huyo.
“Camara pia mabao aliyofungwa dhidi ya Coastal Union pia alikuwa nje ya eneo lake. Bao lingine alilofungwa na Ladack Chasambi wakati wamecheza dhidi ya Fountain Gate mpigaji alikuwa mbali na Camara alitoka eneo lake, mbaya zaidi badala ya kuokoa na mguu wa kushoto akawa anajaribu kutumia mguu wa kulia, lakini wanafanya yote hayo wanajiamini kupitiliza makosa hayo hayawezi kufanywa na Mshery.”