Pamba Jiji yatuma ujumbe kwa waamuzi Ligi Kuu

Pamba Jiji imetuma ujumbe kwa waamuzi wa Ligi Kuu Bara ikionyesha masikitiko juu ya vitendo vya baadhi ya waamuzi kulazimisha matokeo yanayozifurahisha baadhi ya timu na kuziumiza nyingine.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya timu hiyo kunyimwa bao lililofungwa na Salehe Masoud kwenye mchezo dhidi ya Azam FC uliopigwa Februari 9, mwaka huu, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, huku pia ikidai kunyimwa penalti baada ya mchezaji wake kuangushwa kwenye eneo hatari.

Mlezi wa timu na Mwenyekiti wa kamati ya hamasa, Said Mtanda alisema timu zinatumia gharama kubwa kuwekeza kwenye vikosi vyao na maandalizi ya mechi, hivyo, baadhi ya maamuzi yanakatisha tamaa na kuleta uvunjifu wa Amani viwanjani.

Mtanda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, alisema Pamba Jiji inatumia zaidi ya Sh60 milioni kwa mwezi kulipa mishahara ya wachezaji pamoja na gharama nyingine za kusafiirisha timu, ada za usajili na kusajili wachezaji.

“Inapofika mahala tunawekeza kwenye timu alafu anakuja mtu anaamua kutengeneza matokeo yake uwanjani siyo sawa na hailengi kukuza mpira wa Tanzania. Tukileta ujanja kwenye viwanja na kupindisha sheria sisi wadau hatuwezi tukaukubali,” alisema Mtanda na kuongeza:

“Sasa tujenge utulivu kwenye michezo marefarii wachezeshe mpira wa miguu kwa mujibu wa sheria za soka zilizowekwa ili amani itawale kwenye viwanja vya michezo. Marefarii wasiwe chanzo cha kuondoka kwa amani halafu baadaye waseme uwanja fulani una vurugu.”

Kocha wa Pamba Jiji, Fred Felix ‘Minziro’ alisema alama sita walizozipata dhidi ya Azam na Dodoma Jiji haikuwa kazi rahisi huku akiupongeza uongozi wa timu na mkuu wa mkoa kwa sapoti wanayompa kuhakikisha timu hiyo inakuwa salama.

“Kazi yetu ni kuhakikisha mchezo unaofuata tunapata matokeo mazuri na tunaendelea kuwa salama zaidi. Jambo kubwa tunalowaambia mashabiki wetu ni tunapambana ili Pamba isishuke daraja mengine yatafuata baadaye,” alisema Minziro.

Related Posts