UCHAMBUZI WA MALOTO: Lowassa aliwatazama Watanzania kama rasilimali namba moja

Edward Ngoyai Lowassa, tayari ameshatimiza mwaka mmoja tangu alipovuta pumzi ya mwisho, Februari 10, 2024 akiwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Muhimbili. Ndani ya mwaka mmoja, mengi yametokea, mengine akiamshwa na kunong’onezwa, hata na mkewe Regina, atakataa.

Lowassa anaweza kuamini vipi kuwa Freeman Mbowe si Mwenyekiti wa Chadema? Chama alichokitumia kama tawi la ziada, kupigania nafasi yake ya kuwa Rais wa Tanzania, baada ya chama chake, CCM, kumnyima tiketi mwaka 2015.

Inawezekana asishangae Mbowe kuachia uenyekiti, maana hakuna marefu yasiyo na ncha. Hata hivyo, akisikia Mbowe ameondoka mamlakani kwa kushindwa uchaguzi, atastaajabu zaidi. Ikifika hatua akiambiwa aliyemshinda ni Tundu Lissu, ataikataa simulizi. Ataona ni uongo mtupu.

Lissu na Mbowe, ukaribu waliokuwa nao. Kama ndugu wanaochangia damu. Hakuna namna yoyote Lowassa angetarajia ndugu hao wawili walioshibana, wangeweza kushindania uenyekiti wa chama chao. Imewezekana na imeshatokea.

Hata Peter Msigwa yupo CCM hivi sasa. Lowassa hawezi kukubali hili. Akiambiwa Mkutano Mkuu maalumu CCM, ulioketi Januari 18 na 19, 2025, ulifanya uamuzi wa kihistoria kwa kumpitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu 2025, anaweza kubaki na maswali mengi kichwani. Ilishindikanaje kwake?

Katiba ya CCM imetoa mamlaka ya mwisho kwa Mkutano Mkuu. Nao wajumbe waliona watumie mamlaka yao kwa kubadili mchakato wa uteuzi wa mgombea urais, wakamteua Rais Samia Suluhu Hassan kwa njia ya mkato, kinyume na utamaduni wa chama hicho. Mambo ni mengi yametokea. Lowassa atatikisa kichwa. Hakika!

Kuna jema litampendeza Lowassa, ni uteuzi wa Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza. Alikuwa akipigania afya yake kipindi Nchimbi anateuliwa kuwa Katibu Mkuu CCM. Kama CCM watashinda urais Oktoba 2025, Nchimbi atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nchimbi hufahamika kuwa kijana wa Lowassa. Mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM kwenye Uchaguzi Mkuu 2015, ulisababisha hekaheka. Nchimbi akiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba, vilevile Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa, walitangaza kujitenga na uamuzi wa Kamati Kuu.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Nchimbi alisema, wao kama sehemu ya wajumbe, walijitenga na uamuzi wa Kamati Kuu kwa sababu kuna majina yalikatwa kabla ya kufika Kamati Kuu, ambacho ndicho kikao halali cha kwanza cha mchujo wa wagombea.

Nchimbi, Sophia na Kimbisa, japokuwa hawakutaja majina, lakini tafsiri ya wengi ilikuwa, walisusia uamuzi wa Kamati Kuu kwa sababu jina la Lowassa, lilichomolewa kabla ya kufika kwenye kikao hicho.

Baada ya uchaguzi, Nchimbi alipewa onyo kali na kutakiwa kuomba radhi, Sophia alifukuzwa uanachama, wakati Kimbisa alisamehewa.

Baadaye Nchimbi alipelekwa kuwa Balozi wa Tanzania Brazil, kisha Misri, halafu akarejeshwa nyumbani bila kuwa na kazi yoyote.

Kuna wakati, Rais Samia alisema kuna balozi alimrudisha nyumbani kwa sababu alikuwa hafanyi kazi yoyote. Kipindi hicho, kwa kuwa Nchimbi alikuwa amerejeshwa Tanzania, watu wengi walidhani mlengwa alikuwa yeye.

Baada ya vuta nikuvute nyingi za kisiasa, kupanda na kushuka, leo Nchimbi ni Katibu Mkuu CCM, haitoshi, anaomba afya na ushindi kwa CCM Uchaguzi Mkuu 2025, awake historia ya kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania. Habari hii itamfanya Lowassa atabasamu.

Ni tafakuri ya mwaka mmoja tangu kifo cha Lowassa. Yapo mengi yamejiri, ambayo yangemstaajabisha, na mengine yangemuudhi.

Lakini hili la Nchimbi lingengemfurahisha, hasa hatua ambazo Nchimbi anapiga kuelekea mafanikio makubwa ya wasifu wake wa kisiasa.

Kifo cha Rais wa Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 98, kingemsononesha, kwamba kumbe baada yake na Mzee Mwinyi naye alifuata. Watanzania wengi walitamani na walisubiri kwa hamu kuona Mzee Mwinyi akitimiza umri wa miaka 100. Haikuwa hivyo. Mungu hakupanga. Maradhi ya kansa ya ngozi yalikatisha matarajio.

Mwaka mmoja tangu kifo cha Lowassa ni kumbukumbu ya Mtanzania mashuhuri, aliyeamini Watanzania ni rasilimali namba moja katika kuijenga Tanzania. Alitaka Watanzania wawe na elimu ya kutosha ili wawe na thamani kubwa kwenye ushindani wa soko la ajira, vilevile maarifa ya kuijenga nchi yao.

Wakati anawania urais mwaka 2015, aliweka vipaumbele vyake vitatu vya mwanzo kuwa elimu, elimu, elim. Aliamini kuwa bila Mtanzania kuwezeshwa kupata elimu bora, taifa litaendelea kubaki nyuma, huku mataifa mengine, zikiwemo nchi jirani, zikipiga hatua kwa kasi.

Kingine katika kuwajengea uwezo Watanzania, Lowassa alihubiri kuhusu vijana kuwa na fursa ya kutoka Tanzania kwenda kutembea nchi zilizoendelea. Aliamini kuwa vijana wangetoka kwa wingi wangejionea na kujiongeza, hivyo kupata usongo wa kujenga uchumi wao, vilevile taifa lao.

Hakuna kinachoweza kuchochea maendeleo binafsi na nchi kwa haraka kama mapinduzi ya fikra za watu. Lowassa aliamini kwenye uwekezaji mkubwa wa fikra za Watanzania. Alitaka waelimike, waijue dunia, wawe na mawazo chanya.

Lowassa aliteswa na wingi wa vijana wanaoingia mtaani kila mwaka bila uwiano mzuri wa ajira. Mamia elfu wanatoka vyuoni, wanaingia mtaani ambako ajira hakuna. Lowassa aliitafsiri hali hiyo kama “bomu”. Alisema, bila kuwa na mpango mzuri, bomu hilo litakuja kulipuka siku moja.

Mengi zaidi kuhusu Lowassa, nimeandika kwenye kitabu changu; “Kikwete Lowassa; Urafiki, Ndoa Yao ya Kisiasa, Uadui”, ambacho kipo madukani. Endelea kupumzika Edward Ngoyai Lowassa.

Related Posts