Arusha. Baba mzazi wa marehemu Dk Derick Magoma, Jumanne Magoma amesema atamkumbuka mwanaye kwa maono yake makubwa ya kiuchumi katika ngazi ya familia hadi Taifa kwa ujumla.
Ameenda mbali zaidi akisema anatamani kungekuwa na uwezekano wa kuchota akili na maono ya marehemu Derick ampandikize mmoja wa ndugu zake ili kuhakikisha yanatimia na kuleta manufaa aliyokuwa anayatarajia.
Mzee Magoma amebainisha hayo leo Jumatatu Februari 10, 2025 kwenye ibada fupi ya kumuaga aliyekuwa mwanaye ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Manyara, Dk Magoma, mbele ya mamia ya waombolezaji.

Waombolezaji wakiaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Manyara, Dr Derick Magoma nyumbani kwake Kimandolu jijini Arusha leo Februari 10, 2025. Picha na Bertha Ismail
Dk Magoma aliyefariki jana Jumapili Februari 9, 2025 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, ameagwa leo Februari 10, 2025 nyumbani kwake Kimandolu jijini Arusha kabla ya kasafirishwa jioni ya leo.
Marehemu anatarajiwa kuzikwa kesho katika mji wa Magugu, Kijiji cha Matufa, Wilaya ya Babati mkoani Manyara yakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu.
“Huyu hakuwa mtoto tu kwangu, bali alikuwa rafiki mkubwa, mbali na itikadi zetu za kisiasa kuwa tofauti lakini tulikuwa tunabishana kwa hoja na mwisho kila mtu anabaki na anachokiamini,” amesema na kuongeza:
“Mbali na mabishano lakini ukaribu wetu zaidi ulijengwa na malengo ya kuinua familia nzima kiuchumi ambapo alikuwa na maono makubwa ya miradi ambayo alitengeneza maandiko kwenye mataifa mbalimbali ili kutengeneza miradi mikubwa ambayo ingesaidia pia nchi,” amesema baba huyo.
Akitoa salamu za rambirambi, Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Elisa Mungure amesema watamkumbuka Magoma kwa mengi aliyoyafanya katika kukijenga chama lakini kutetea demokrasia ambayo hadi leo haijafanikiwa.
“Dk Magoma ameacha alama kubwa sana katika ujenzi wa chama hadi hapa ilipofikia hasa katika katika chaguzi mbalimbali za ubunge na madiwani na wenyeviti katika mikoa ya kanda ya kaskazini,” amesema Mungure.

Waombolezaji wakiaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Manyara, Dr Derick Magoma nyumbani kwake Kimandolu jijini Arusha leo Februari 10, 2025. Picha na Bertha Ismail
Mungure amesema kuwa, wataendelea kumuenzi katika malengo yake hasa ya kuhakikisha siku moja nchi hii inafanya uchaguzi wa kidemokrasia kama unavyofanyika wa Chadema Taifa hivi karibuni.
“Mbali na hilo, alitamani siku moja kukalia kiti cha ubunge katika nchi hii lakini amekufa bila kutimiza malengo hayo, hivyo sisi kazi yetu katika kumuenzi tutahakikisha mapambano yanaendelea hadi kushika nchi baadaye.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini, Aden Mayala akitoa salamu zake amesema Chadema itazidi kumkumbuka Magoma kutokana na uthubutu wake wa kupambania chama hata kujiingiza kwenye maeneo ya hatari ili mradi apate anachokiamini.
“Mwasisi wa chama chetu, Mheshimiwa Freeman Mbowe alikuwa anajivunia sana uwepo wa Magoma katika eneo lolote na hata alipokuja kwetu kusini katika kampeni mbalimbali, tuliona uthubutu wake wa kuhakikisha tunavuna kura za wenyeviti wa mitaa,” amesema.
Dk Magoma, enzi za uhai wake, mbali na kuwahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha na Miata, pia, aligombea ubunge wa Hanang’ kwa tiketi ya Chadema katika vipindi viwili, mwaka 2015 na 2020. Hata hivyo, alishindwa na wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).