Wakulima Pwani kuchimbiwa visima, DC atoa angalizo

Kibaha. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), imesaini mkataba wa mradi wa uchimbaji visima vitano vya umwagiliaji katika Mkoa wa Pwani utakaowanufanisha wananchi wa ndani na nje ya mkoa huo.

Mradi huo ukikamilika utawanufaisha wananchi wa kijiji cha Gwata (Kibaha), Mwetemo (Chalinze), Mkupuka (Kibiti) na Mbwara (Rufiji) ambapo zaidi ya Sh311 milioni zinatarajiwa kutumika.

Makubaliano hayo baina ya NIRC na Kampuni Paragon Engineering Ltd watakaochimba visima hivyo yameingiwa leo Jumanne, Februari 11, 2025 katika Kijiji cha Gwata wilayani Kibaha.

Meneja wa NIRC Mkoa wa Pwani, Ramadhanj Lusonge amesema visima hivyo ni sehemu ya Mpango wa Serikali wa Programu ya Mfumo Himilivu ya Chakula kwa Kuzingatia Matokeo ili kuhakikisha nchi inakuwa na chakula cha kutosha.

Amesema visima hivyo vinatarajiwa kutumika katika kilimo cha mbogamboga vitachimbwa katika wilaya tano za mkoa huo.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Saimon akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge amesema awamu ya kwanza itahusisha visima vinne vitakavyochimbwa katika Wilaya ya Kibaha, Kibiti, Chalinze na Rufiji. 

Amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha sekta ya kilimo cha umwagiliaji inakua katika mkoa huo na kuchangia ukuaji wa uchumi na Pato la Taifa.

“Visima vitafungwa umeme wa solar (jua) ili kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika wakati wowote hivyo kuwawezesha wakulima kulima mpaka misimu mitatu kwa mwaka badala ya mmoja kama ilivyozoeleka,” amesema. 

“Lengo letu mkoa wa Pwani ni kufikisha visima 240 ifikapo mwaka 2030 kwani mpaka sasa tuna jumla ya visima 140 na kwa kasi hii ya Tume ya Umwagiliaji chini ya Rais Samia Suluhu Hassan tunaamini hilo tutatekeleza,” alisisitiza Saimon.

Mkuu huyo wa wilaya amesema katika awamu hii ya mradi huo itahusisha visima 35 katika wilaya saba za mkoa huo ambako kila wilaya itachimbiwa visima vitano.

Aidha, mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi wanaonufaika na mradi huo kuhakikisha wanashirikiana kulinda miundombinu yake ili idumu na kuwanufaisha zaidi.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa alisema kwa mwaka huu wa fedha Tume inatarajia kuchimba visima 1,300 na kati ya hivyo visima 70 vitakahudumia mikoa 16 ikiwemo Pwani, Tanga, Mara, Songwe, Singida, Manyara, Dodoma, Lindi, Mtwara, Kigoma, Geita, Morogoro, Simiyu, Ruvuma na Njombe vitachimbwa na wakandarasi na visima vinavyobaki vitachimbwa kupitia mitambo inayonunuliwa.

Related Posts