Wasira: Uchaguzi Mkuu upo pale pale, awapa ujumbe Chadema

Mwanza. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 utafanyika kama ulivyopangwa na wala hakuna chombo chochote cha Serikali kinachoweza kuukwamisha.

Wasema amesema wanaosema pasipo mabadiliko haufanyika wanaota ndoto ya mchana huku akiwaomba Watanzania kuendelea kujiandaa na uchaguzi huo ambao amedai CCM itaibuka na ushindi wa kishindo.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bara, Stephen Wasira akizungumza na wafuasi wa chama hicho katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira.

Wasira amesema hayo leo Jumanne, Februari 11, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza akiwa kwenye mwendelezo wa ziara yake ya ‘kutesti mitambo’ akianzia Geita, Dar es Salaam, Mara na sasa yupo Mwanza.

Kauli ya Wasira inakuja kipindi ambacho chama kikuu cha upinzani Tanzania- Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiwa na kauli mbiu ‘No Reform, No Election’ ikielea pasipo mabadiliko ya kimfumo hakutakuwa na uchaguzi.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu mara baada ya kuchaguliwa Januari 22, 2025 kuibuka mshindi wa nafasi hiyo akimbwaga Freeman Mbowe alisisitiza umuhimu wa mabadiliko ya kimfumo. Inatarajiwa kesho Jumatano, Februari 12, 2025, Lissu atatoa msimamo wa suala hilo katika mkutano wake na waandishi wa habari utakaofanyika makao makuu ya Chadema, Mikocheni, Dar es Salaam.

Mara kadhaa viongozi wa Chadema, akiwemo Lissu wamesikika wakishinikiza mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi kabla ya kuushiriki kupitia kauli mbiu yao ya ‘No Reforms, No Election’ (Hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi).

Wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  wakimsikiliza Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, Stephen Wasira. Picha na Mgongo Kaitira.

Hata hivyo, Wasira amesema licha ya msimamo wao huo, uchaguzi utafanyika mara tu baada ya Tume Huru ya Uchaguzi kutangaza tarehe kama ilivyopewa mamlaka na katiba ya nchi.

Leo Jumanne, Februari 11, 2025, Wasira amesema hakuna taasisi yoyote ya kiserikali au chama cha siasa chenye uwezo wa kuhairisha uchaguzi mkuu labda itokee vita ambayo Tanzania hakuna.

“Sis ni wadau wa uchaguzi, kazi yetu ni kuitumia dola kuleta mabadiliko ya watu…kwahiyo hatuwezi kuambiwa hakuna uchaguzi. Wao kama wanataka kuingia kwenye uchaguzi bahati mbaya sisi tunawakaribisha maana uwezo wa kuwashinda tunao wanatusingizia CCM wanaiba tunaiba nini?

“Tumefanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuna mitaa hawakupata hata mtu mmoja wa kusiamamisha sasa mtu ambaye hana mtu wa kusimamisha kwenye mtaa na kijiji atakushinda kwa namna gani ni muujiza au ni kitu gani,” amehoji Wasira.

“Sasa mimi nataka kuwaambia hakuna mtu mwenye mamalaka ya kuhairisha uchaguzi hakuna! Hakuna chombo chochote kiwe cha kiserikali au cha nani kinachoruhusiwa kuhairisha uchaguzi ibara ya 41 sehemu ya nne ya katiba inaipa tume mamlaka ya kutangaza tarehe ya uchaguzi na wakati utakapofika tume itatangaza tarehe ya uchaguzi,” amesema.

Amesema hakuna reform itakayofanyika kwa sababu ni mambo ya sheria na Bunge Februari 14, 2025 linamalizika na kubaki kikao kimoja cha bajeti na baada ya kikao hicho wabunge watarejea ma kwao.

Aeleza chimbuko la No Reforms no election, Wasira amesema chimbuko la kauli mbiu hiyo ni baada ya Serikali kukataa ombi la Chadema la kuwaondoa wabunge 19 Bungeni ambao chama hicho kilitaka waondolewe pamoja na madai ya Katiba mpya akieleza vyama vingine vilitaka mchakato wake uanze baada ya uchaguzi mkuu.

“Maendeleo yanawezekana katika mazingira ya amani, Rais Samia katika miaka yake minne alianzisha maridhiano na vyama vya siasa ili tuwe na chi tulivu ambayo inasimamia maendeleo kwa sababu kama hakuna amani hakuna maendeleo kwahiyo akazungumza na vyama…Tunavyo vyama 19 vilivyosajiliwa na vyama hivi vyote vikakubaliana naye isipokuwa kimoja tu,”amesema Wasira.

“Kiimoja kikakataa kuhudhuria lakini akasema na hicho nacho tutazungumza nacho pembeni, vyama vikamshauri suala la katiba lisubiri tumalize uchaguzi sababu ni suala kubwa linahusu watanzania wote,” amesema.

Kada huyo ameeleza vyama hivyo vilivyokubali vilitoa sharti la sheria zinazohusu uchaguzi zifanyiwe marekebisho, zikafanyiwa marekebisho ikiwemo ya kuunda tume ya uchaguzi mpya, sheria ya uchaguzi wa Rais, Madiwani na Wabunge na sheria ya vyama vya siasa ambazo zilizpitishwa na Bunge baada ya marekebisho hayo.

“Chadema ambao hawakutaka kushiriki wao walisema wana matatizo yao wanataka yashughulikiwe pembeni wakaleta masuala 11 na kwa huruma za Rais Samia wakasikilizwa. Moja walitaka watu waliokuwa wamekimbia nchi warudi kwa amani…

Serikali ya (Rais) Samia ikasema wote warudi na Tundu Lissu alikuwa na kesi sita akasema zifutwe. Kulikuwa na wanachadema 400 wana kesi na wengine wamefungwa wote kwa kutumia mfumo wa sheria na mamlaka aliyokuwa nayo Rais akawasamehe hata waliokuwa jela,” amesema.

Wasira ameendelea kuwasimuliwa wana CCM na wananchi kuwa, Chadema pia walitaka mikutano na maandamano ambayo yaliruhusiwa lakini wakashindwa kutimiziwa madai ya katiba mpya na kuwaondoa Bungeni wabunge 19 wa viti maalum.

 “Sasa wakasema wanawake wale 19 waliopo Bunge waondolewe. CCM ikasema hatuwezi maana wako mahakamani kwa mujibu wa sheria hatuingilii Mahakama hilo likashindikana…wakasema wanataka katiba mpya wenzao walikuwa wameshasema katiba mpya isubiri tumalize uchaguzi ili watu wengi Watanzania wajue tunaandika katiba ya namna gani,” amesema.

Awali, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mkoa wa Mwanza, Jamal Babu amesema ziara ya Wasira inayoenda sambamba na ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya chama hicho, kuzungumza na wanachama na wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ni kupima mitambo kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Related Posts