Dodoma. Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imewaita waliokuwa wateja 3,119 wa Benki ya FBME ambao amana zao ni chini ya Sh1.5 milioni kwenda kuchukua fedha zao, huku ikitaja sababu mbili zilizochelewesha kulipa fidia ya bima kwao.
Wito huu unatolewa ikiwa ni siku tano kupita tangu waliokuwa wateja wa benki hiyo kuitaka DIB kutoa mrejesho wa malipo yao kufuatia ukimya uliokuwa umetawala tangu benki hiyo kuwekwa chini ya ufilisi.
Alipozungumza na wanahabari, Februari 6, 2025 kwa niaba ya wadai wengine, Dk Majura Mfungo alisema tangu benki hiyo ifungwe mwaka 2017, malipo ya amana za wateja na wadai wengine zaidi ya Sh31 bilioni bado hazijalipwa huku wengine wamefariki dunia.
“Pia, kumekuwa na kesi kadhaa ambazo zilipelekea malipo ya amana za wateja kuchelewa kulipwa, lakini hata baada ya kesi hizo zote kumalizika pamekuwa na usiri na sintofahamu ya ulipaji wa fedha za wateja,” amesema Dk Mfungo.
Benki ya FBME iliwekwa ufilisi Mei 2017, baada ya Marekani kuituhumu FBME tawi la Tanzania kuhusika na utakatishaji fedha jambo ambalo lilifanya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuiweka chini ya ufilisi.
Alipozungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Februari 11, 2025 jijini Dodoma, Mkurugenzi wa DIB, Isack Kihwili amesema benki hiyo ilikuwa ikifanya biashara kubwa ya asilimia 90 katika tawi lake lilopo nchini Cyprus huku Tanzania ikiwa na asilimia 10.
Hivyo, amesema ufilisi wa benki ya FBME umekuwa wa namna ya kipekee kutokana na sababu kubwa ya kuhusika kwa sheria na mamlaka za nchi mbili tofauti yaani Tanzania na Cyprus kwa kuwa benki hii ilikuwa na tawi nchini Cyprus.
“Hali hii ilisababisha mvutano wa muda mrefu na kufunguliwa mashauri (kesi) kadhaa nchini Cyprus kuhusu Mamlaka inayostahili kuwa Mfilisi wa tawi la Cyprus,” amesema.
Kihwili amesema mashauri hayo yalichukua muda mrefu hadi kuamuliwa.
Amesema sababu ya pili ni uwapo wa vikwazo vya Mamlaka za Marekani (FinCEN) dhidi ya fedha za tawi la Cyprus zilizoko katika benki mbalimbali nje ya Cyprus.
Amesema vikwazo hivyo vimechelewesha upatikanaji wa fedha hizo ili ziweze kugawanywa kwa wadai wa Tanzania na Cyprus.
Kihwili amesema ufilisi usingeweza kufanyika upande mmoja wa Tanzania pekee yake kwani fedha zote zinapaswa kukusanywa na kulipwa kwa wateja wa benki hii kwa uwiano sawa kwa mujibu wa sheria.
Amesema kwa wateja wanaodai bima ya amana chini ya Sh1.5 milioni wameanza kulipwa tangu Julai 2017 ambapo hadi kufikia Desemba 31 mwaka 2024, DIB ilikuwa imeshalipa fidia ya bima ya amana ya Sh3.51 kati ya Sh4.29 bilioni.
Amesema jumla ya wateja 3,509, wamelipwa fidia ya bima ya amana zao huku wateja 3,119 waliobakia ambao wanadai Sh1.80 bilioni wakisubiriwa kufika katika ofisi za DIB kuchukua fedha zao.
Kuhusu wateja wanaodai fidia ya bima ya amana yenye zaidi ya Sh1.5 milioni, Kihwili amesema baada ya Kamati kuhakiki madai na kuridhia ulipaji wa awamu ya kwanza ya malipo ya fidia ya ufilisi kwa kiwango cha asilimia 30 ilifanyika.
Amesema hadi kufikia Desemba 31, 2024, jumla ya wateja 928 sawa na asilimia 65.6 kati ya 1,414 walikuwa wamelipwa fidia ya ufilisi ya kiwango cha asilimia 30 sawa na Sh9.09 bilioni.
“Ifahamike pia kwamba malipo haya yamefanyika kwa wateja wa Tanzania pekee. Wateja wa Tanzania walioko nje ya nchi na wale wa tawi la Cyprus bado hawajalipwa,” amesema.
Amesema madai yote kwa wateja wenye amana wa Tanzania yalikuwa ni Sh343.45 bilioni ambapo wateja walioko nje ya nchi wanadai Sh308.22 bilioni, na walioko Tanzania wanadai Sh35.23 bilioni.
Kuhusu kusitisha ajira na kulipa stahiki kwa wafanyakazi kwa mujibu wa sheria, Kihwili amesema kutokana na kutoridhishwa na tafsiri ya kisheria juu ya stahiki za wafanyakazi baada ya benki kufungwa.
Amesema malalamiko ya wafanyakazi yalifikishwa katika vyombo vya kisheria hadi ngazi ya Mahakama ya Rufaa ambapo iliamuliwa DIB kuwalipa wafanyakazi hao mshahara wa mwezi mmoja kama mbadala ya Notisi ya kuachishwa kazi.
Ametaja malipo mengine ni likizo kwa wale ambao hawakulipwa, malipo ya kiinua mgongo na malipo ya kuwawezesha wafanyakazi hao warudi sehemu ambako waliajiriwa.
Kihwili amesema kwa kufuatia uamuzi huo wa Mahakama, DIB iliwasajili wafanyakazi 99 kama wadai ambapo malipo yao pamoja na malipo ya wadai wengine yatalipwa kwa kuzingatia mtiririko ulioainishwa na sheria ya ufilisi.
Kuhusu fidia ya ufilisi ambayo walikuwa na amana ya zaidi ya Sh1.5 milioni, Kihwili amesema wateja 1414, walikuwa wakidai Sh35.24 bilioni kwa upande wa Tanzania huku Cyprus wakidai Sh308.22 bilioni.
Amesema wateja 938 kati ya 1414, wa Tanzania ambao sawa na asilimia 65.6, walilipwa Sh9.09 bilioni kama fidia ya ufilisi ambayo ni asilimia 30.
Mkurugenzi wa Huduma ya shirika, Raphael Nombo amesema DIB ina nia ya kuwalipa wateja wote wanaodai fidia na kuwataka kuwa wavumilivu wakati madai yao yanashughulikiwa.