YANGA YATIMIZA MIAKA 90 LEO – Global Publishers

 

Klabu ya Young Africans SC (Yanga SC) leo, tarehe 11 Februari 2025, inasherehekea miaka 90 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1935.
Yanga imepitia safari ndefu ya mafanikio, ushindani, na historia kubwa katika soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla.


Tangu ilipoanzishwa, Yanga SC imekuwa klabu yenye mashabiki wengi zaidi Afrika Mashariki. Ilipoanzishwa mwaka 1935 Klabu ya Yanga, makao makuu ya Klabu yalikua kwenye nyumba ya kupanga. Mwaka 1963 uongozi wa Mzee Mohamed Sultani (Mobosti) – Mwenyekiti, Mzee Kitwana Kondo Makamu na Mzee Jabir Katundu akiwa Katibu Mkuu walikuja na wazo la Yanga kuwa na jengo lake.

Mwaka 1964 Viongozi hao waliandaa mchezo wa kirafiki na Klabu ya Abaluhya ( sasa FC Leopards) ya Kenya ambayo ilikua imeanzishwa mwaka huo, na kwenye mchezo huo wa kirafiki Yanga ilifanikiwa kupata Tsh. 13,000/=, hela mabayo ilitosha kabisa kununua Jengo la Mafia lililopo Mtaa wa Mafia na Nyamwezi hivyo kuwa Klabu ya Kwanza kuwa na jengo lake ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.

Mwaka 1969 viongozi waliona kuwa Yanga inahitaji makao makuu yenye hadhi zaidi ya waliokuwa nayo, hivyo kuamua kufunga safari kwenda kwa Rais wa Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karume kumuomba ufadhili, lakini mzee Karume alitoa sharti moja, kwamba lazima Viongozi wa Yanga waambatane na Viongozi wa Queens FC (Simba kwa sasa) watakapoenda kumuona, na walifanya hivyo.

Baada ya kupewa wazo hilo, Sheikh Karume alikubali kujenga jengo moja ambalo litamilikiwa na vilabu vyote viwili, lakini wazo hilo liligonga mwamba, ndipo aliamua kuipa Yanga Tsh. 2,000,000/= ili wakajenge jengo lao, Kupitia kwa mzee Rashid Kawawa, Mzee Karume aliwakabidhi hundi hiyo mzee Mangara na Mzee Ramadhani Mwinyikambi.


Viongozi wa Yanga kwa kushirikiana na Wajerumani waliweza kupata mchoro na mkandarasi wa kujenga jengo la Jangwani kwa Tsh. 800,000/=. Walipopeleka michoro hiyo City Council kwa ajili ya kuidhinishwa, Injinia mmoja aliyefahamika kwa jina la Lunyasi aliyekuwa mwanachama wa Simba alikataa kupitisha mchoro huo kwa madai kwamba eneo lile ni jalala likijengwa jengo litaanguka.Viongozi walimfikishia taarifa hiyo mzee Karume ambaye alifunga safari kuja mpaka Jangwani kuweka jiwe la msingi na kuruhusu ujenzi kuanza mara moja.

Yanga imetoa viongozi mbalimbali wa soka na serikali mmoja wapo ni aliyekuwa Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ambaye mwaka 1976 alipokuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili wa klabu hiyo na kuwezesha usajili wa Shaaban Katwila.

Pia Yanga iliwahi kutoa Rais wa CECAFA Leodegar Tenga, Rais wa TFF Jamal Malinzi, nahodha wa Taifa Stars na Zanzibar Heroes Hadir Haroub ‘Cannavaro’na aliyekuwa kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars Charles Boniface Mkwasa. Hivi sasa imetoa Rais wa Vilabu Afrika, Injinia Hersi Saidi.
Katika ngazi ya kimataifa, Yanga imeendelea kung’ara:
✅ 2024/25 – Ilicheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
✅ 2023/24 – Ilifika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
✅ 2022/23 – Iliandika historia kwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa klabu ya kwanza kutoka Tanzania kufika hatua hiyo.

 

Related Posts