Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimepanga kuitumia siku ya wanawake duniani mwaka huu, kutoa tamko na mwelekeo wa wanawake katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake Taifa wa chama hicho, Janeth Rithe ameyasema hay oleo Alhamisi, Februari 13, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari makao makuu ya ofisi za ACT Wazalendo zilizopo Magomeni, jijini Dar es Salaam.
Rithe amesema wataitumia siku ya wanawake dunia mwaka huu kufanya harakati sambamba na elimu inayolenga kuleta ukombozi wa wanawake kisiasa na kiuchumi nchini.
“Mara nyingi wanawake tumekuwa tunarudishwa nyuma na kutumika kuwasogeza wanaume kupata nafasi za kisiasa,” amesema kiongozi.
Amesema nguvu ya wanawake ni kubwa katika uchaguzi, lakini wameendelea kutumika kuwapandisha wanaume katika nafasi mbalimbali za uongozi.
“Kupitia sensa ya watu na makazi iliyopita, inaonyesha wanawake ni wengi kuliko wanaume na ndiyo tunaopiga kura kwa wingi,” amesema.
Hivyo, Rithe amesema kwenye uchaguzi ujao wa Oktoba, nguvu ya wanawake inapaswa kuonekana na Machi 8, 2025 watakuja na tamko na kutoa mwelekeo wa kundi hilo kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.
“Wanawake walioko kwenye vyama vya upinzani vya siasa na wale wasiokuwa kwenye vyama wanapaswa kuwa na kauli moja na kuonyesha mshikamano ili kutatua kwa pamoja changamoto zinawakabili,” amesema Rithe.
Amesema katika tamko litakalotolewa, litaeleza madai yao ya kisiasa ambayo yatato mwelekeo mpya wa nafasi ya mwanamke katika siasa za Tanzania.
Kiongozi huyo amesema ACT Wazalendo itaendelea kusimama pamoja na wanawake kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwa ajenda ya kweli katika maendeleo ya nchi.
Rithe amegusia pia nguvu ya wanawake inavyohitajika akiamini inaweza kuiondoa CCM madaraka.
“Tukiwa na kauli moja, wanawake wote wa vyama vya upinzani na wale wasiokuwa kwenye vyama, tutatimiza adhima hii,” amesema.
Akizungumzia maadhimisho ya siku ya wanawake inayoadhimishwa kila mwaka Machi 8, Rithe amesema mwaka huu, ACT watayatumia maadhimisho hayo kushiriki katika kuchangia damu na upimaji wa afya sanjari na kutoa msaada wa kisheria kwa wanawake.
“Wanawake wa Tanzania wamekuwa wakikabiliwa ukandamizaji katika nyanja tofauti ikiwamo ukatili wa kijinsia na wa kiuchumi na wengi wao kutengwa katika nafasi za uongozi kwenye siasa.
“Kupitia changamoto hizi tumeteua wanawake waliopo ACT ambao ni wanasheria kusikiliza kero na changamoto mbalimbali na kuwasaidia wanawake wote ambao ni wapenzi na wanachama wa ACT na wale waliopo nje ya Chama,” amesema.
Amesema lengo ni kuihamasisha jamii kuhusu nafasi mwanamke katika maendeleo ya taifa na kupaza sauti dhidi ya ukandamizaji wa kijinsia na kudai hatua madhubuti kwa usawa wa kijinsia katika siasa na uchumi
“Tunayo mapendekezo ambayo tunataka yachukuliwe wakati huu, Chama kina ilani inayoeleza namna bora ambayo wanawake wanataka kuongoza na kuongozwa na kufikia malengo tarajia,” amesema.
Mbali na mkakati huo, Rithe amesema katika wiki ya kuelekea kilele cha siku ya wanawake watakuwa na tuzo za mapambano na sanaa ya uombozi kwa wa wanawake, uchangiaji damu na maonyesho ya bidhaa za wanawake wajasiriamali.
“Vilevile tutakuwa na upimaji afya kwa hiari hasa saratani ya matiti na shingo ya mlango wa kizazi litakaloongozwa na wataalamu wa afya,” amesema.
Wakati Rithe akitoa kauli hiyo, Mwananchi imezungumza na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Husna Mohammed, ambaye amesema kuwa mkakati wa ACT kuhusu wanawake ni sawa na mkakati wa chama chao katika kuwahamasisha wanawake kushiriki siasa.
“Japokuwa ni washindani wetu, lakini katika jitihada za kuonesha nafasi ya mwanamke kwenye siasa, tuko pamoja nao. Tumeona kiongozi wao, ambaye ni mwanamke, ametangaza nia ya kugombea urais,” amesema Mohammed.
Amebainisha kuwa mkakati huo unaweza kuleta matokeo chanya kwa kuwa wanawake wameanza kujitambua, kutambua uwezo wao katika siasa na kuwa na dhamira ya kujikomboa.
“CUF tumekuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha wanawake, na tunafurahi kuona vyama vingine vikifuata nyayo zetu,” ameongeza.
Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Conrad Masabo ana mtazamo tofauti akisema kuwa ingawa mkakati huo ni mzuri, mafanikio yake yanategemea changamoto kadhaa.
“Bado vyama vingi vinaongozwa na wanaume, na kuna msemo usemao ‘adui wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe.’ Kwenye siasa pia kuna masuala ya ubinafsi. Ikiwa wanawake watashirikiana kwa umoja, basi ni jambo jema, lakini swali kubwa ni je watafanikiwa?” amesema Masabo.