Tarime. Askofu wa Kanisa la EAGT Kanda ya Ziwa, Joseph Maswi amewataka viongozi wa Serikali na wote wenye dhamana kuhakikisha haki inatendeka katika uchaguzi mkuu ujao ili kulinda amani na utulivu wa nchi.
Akizungumza leo Alhamisi Februari 13, 2025, wakati wa mahubiri yake kwenye hafla ya mapokezi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche, katika kijiji cha Kitagasembe, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Askofu Maswi amesema haki ni msingi wa maendeleo ya Taifa.
Baadhi ya wafuasi na wapenzi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakicheza nyumbani kwao Makamu Mwenyekiti wa Chadema bara, John Heche katika kijiji cha Kitagasembe wilayani Tarime, wakati wa sherehe za kumpongeza kwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo. Picha na Beldina Nyakeke
“Mwaka huu Taifa letu linafanya uchaguzi mkuu. Nawahimiza viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, na wote wenye dhamana kuhakikisha haki inatendeka, kwa kuwa haki huinua Taifa,” amesema.
Ameongeza kuwa wagombea wote, bila kujali vyama vyao wanapaswa kutendewa haki sawa ili kila mmoja aridhike na kudumisha amani na utulivu wa nchi.
“Sisi tunakaribia umri wa ahadi ya Biblia wa miaka 70, na tunatamani kuwaachia watoto na wajukuu zetu nchi yenye amani na utulivu. Nawahimiza viongozi kuhakikisha chaguzi zetu zinakuwa huru na haki,” amesema Askofu Maswi.

Aidha, aneipongeza Chadema kwa kukamilisha salama uchaguzi wa ndani wa viongozi wake na kuzitaka pia vyama vingine vya siasa kutenda haki katika mchakato wa uteuzi wa wagombea wao.
Uchaguzi wa Kitaifa wa Chadema uliofanyika Januari 21, 2025, ulimchagua Heche kuwa Makamu Mwenyekiti (Bara) kwa kura 577, akimshinda Ezekia Wenje aliyepata kura 372.
Awali, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, Lucas Ngoto aliwataka viongozi wa dini kutumia nafasi zao kukemea vitendo vinavyokiuka sheria na haki za wananchi.
“Baadhi ya watu wanaoshiriki uovu ndani ya jamii ni waumini na viongozi wa dini. Ni muhimu viongozi wa dini kuwawajibisha waumini wao,” amesema Ngoto.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Hellen Ghati, mkazi wa Kitagasembe, aliyesema baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali wanaokiuka haki za watu ni waumini wa makanisa na misikiti, hivyo wanaweza kubadilika wakikemewa na viongozi wao wa dini.