Iringa. Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kata za Izazi na Migori Wilaya ya Iringa Vijijini, kimewaonya viongozi wake dhidi ya tabia ya kupokezana nafasi za uongozi kwa misingi ya undugu, jambo linaloleta taswira mbaya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Onyo hilo limetolewa leo Alhamisi, Februari 13, 2025 na Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Sure Mwasanguti, alipokutana na mabalozi wa kata hizo katika Jimbo la Ismani.
Katika mkutano huo, pia alikabidhi mitungi ya gesi iliyotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo, William Lukuvi, kama sehemu ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
“Kata za Migori na Izazi katika Jimbo la Ismani zimekuwa na tabia ya kupachikana uongozi kwa misingi ya undugu, jambo ambalo si sera ya chama na linadhoofisha ustawi wa kisiasa,” amesema Mwasanguti.
Amesema mwenendo huo unatoa taswira mbaya kwamba wanachama wengine hawana haki ya kuchaguliwa.
“Tunapokaribia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ni muhimu kuachana na desturi ya kuchagua viongozi kwa misingi ya undugu, jamaa au urafiki. Tabia hii ni hatari kwa mustakabali wa chama,” amesisitiza.
Mwasanguti amesema uongozi wa kweli unapaswa kujengwa juu ya misingi ya umoja, mshikamano na uwazi.
Hivyo, ametoa wito kwa wanachama wa CCM kuhakikisha vigezo vya uongozi vinazingatiwa badala ya kuzingatia uhusiano wa kifamilia.
“Tunahitaji viongozi wenye uwezo na dhamira ya kweli ya kuleta maendeleo. CCM kama chama tawala lazima kiwe mfano bora wa uongozi wa kitaifa,” amesema.
Pamoja na hilo, amewahimiza viongozi wa CCM kuwa mabalozi wa matumizi bora ya nishati safi kwa kushawishi jamii kuachana na matumizi ya mkaa na kuni.
Kwa upande wake, Fifi Moshi akizungumza kwa niaba ya mabalozi, amesema watazingatia kanuni na taratibu za chama katika uteuzi wa viongozi, wakionesha matumaini kuwa uongozi bora utasaidia kusukuma maendeleo ya jamii.
Letisia Muhulage, mmoja wa viongozi wa CCM, amesisitiza umuhimu wa kuachana na tabia ya kuhalalisha uteuzi wa viongozi kwa kuzingatia uhusiano wa kifamilia, akisema mwenendo huo unadhoofisha maendeleo ya chama na jamii kwa ujumla.
Naye Diwani wa Izazi, Costantino Makala amekiri kuwa bado kuna baadhi ya mabalozi ambao wanahitaji kuelekezwa kuhusu kufuata sera za chama ili kuepuka kasoro katika uteuzi wa viongozi.
Aizungumzia hilo, Diwani wa Migori, Benitho Kayugwa ameweka msisitizo kuwa jamii inapaswa kutafuta viongozi wenye sifa, uzalendo na uwezo wa kusimamia maendeleo badala ya kuteua kwa misingi ya uhusiano wa kifamilia.
Katika hatua nyingine, uongozi wa CCM Wilaya umekabidhi mitungi ya gesi 144 kwa mabalozi wa kata hizo mbili, ikiwa ni sehemu ya mpango wa Mbunge wa Ismani, William Lukuvi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi.