DRC, Rwanda walivyotoana jasho Mahakama ya Afrika Jijini Arusha

Arusha. Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imemaliza kusikiliza hoja za pande mbili katika kesi iliyofunguliwa na Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo (DRC) dhidi ya Rwanda kuhusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kesi hiyo namba 007/2023 iliyofunguliwa Oktoba 2023, DRC inaishutumu Rwanda kufanya vitendo vya kikatili dhidi ya raia wake, ikidai hali hiyo ilikiuka haki za binadamu.

Ukiukwaji huo unadaiwa kuhusiana na mzozo wa silaha unaoendelea katika sehemu ya mashariki ya DRC tangu mwaka 2021.

Majeshi ya DRC yanapigana na kundi la waasi la M23, ambalo linaripotiwa kuungwa mkono na Rwanda.

Kesi hiyo, iliyoanza kusikilizwa jana Februari 12, 2025, jijini Arusha, imeendelea leo huku serikali ya DRC ikisisitiza mahakama kuiwajibisha Rwanda kwa ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya raia wake. DRC inaitaka Rwanda ilipe fidia kwa uharibifu wa mali na mauaji ya maelfu ya wananchi wake, pamoja na kuondoa majeshi na vikundi vyake vya uhalifu kutoka nchini humo.

Mbele ya majaji tisa, akiwamo Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Imani Daud Aboud kutoka Tanzania na Makamu wake Jaji Modibo Sacko kutoka Mali, mahakama ilisikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili.

Baada ya kufungwa kwa usikilizwaji wa hoja, Jaji Sacko amesema kuwa mahakama imezingatia hoja zote na itajadili kabla ya kutangaza tarehe ya uamuzi.

“Tunashukuru kwa ushirikiano wa pande zote mbili. Mahakama itachambua hoja zilizowasilishwa na kutangaza tarehe ya hukumu,” amesema Jaji Sacko.

Nje ya mahakama, Waziri wa Sheria na Wakili Mkuu wa Serikali ya Rwanda, Emmanuel Ugirashebuye, amesema DRC inapoteza muda kwa sababu kesi hiyo haihusiani na mamlaka ya mahakama hiyo. Amedai kuwa mizozo kama hiyo inapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo kulingana na mikataba ya kimataifa, ikiwemo ile ya Nchi za Maziwa Makuu.

“Endapo kuna waliodhulumiwa, wao ndio walipaswa kufungua kesi na kuwasilisha ushahidi wa madai yao. Hata hivyo, tusubiri maamuzi ya mahakama,” amesema Ugirashebuye, aliyekuwa ameambatana na jopo la mawakili saba.

Kwa upande wake, mmoja wa mawakili 17 wa DRC, Tresor Makunya amesema madhara yaliyosababishwa na uhalifu unaotekelezwa na waasi wanaodhaminiwa na Rwanda hayawezi kuelezwa kwa ukamilifu.

“Mauaji, ubakaji wa wanawake na watoto, mateso haya yote yamefanywa na wanadamu wenzao kwa msaada wa Rwanda. Tunaiomba mahakama itende haki,” amesema Makunya.

Oktoba 2023, DRC iliwasilisha kesi hiyo katika mahakama yenye makao yake makuu jijini Arusha, ikilalamikia Rwanda kwa ukiukwaji wa haki za binadamu.

DRC inadai kuwa ukiukwaji huo ni pamoja na mauaji ya halaiki, udhalilishaji, ubakaji wa wanawake na watoto, na kauli za matusi dhidi ya raia wake.

Pia, DRC inaituhumu Rwanda kwa kuharibu miundombinu muhimu kama shule, hospitali, na huduma za maji na umeme kupitia vikundi vya waasi vinavyodhaminiwa na serikali ya Rwanda. Inadai kuwa Rwanda inafanya haya kwa lengo la kupora rasilimali, ikiwemo madini.

Hata hivyo, Rwanda imekanusha madai yote na kuiomba mahakama kutupilia mbali kesi hiyo, ikidai kuwa ni mgogoro wa kisiasa badala ya kesi ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Related Posts