Kamati ya Bunge yabaini ongezeko la gharama stendi ya Ngangamfumuni

Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imebaini ongezeko la gharama ya Sh565 milioni baada ya kusimama kwa ujenzi wa stendi ya kimataifa ya mabasi ya Ngangamfumuni mjini, mkoani Kilimanjaro.

Stendi hiyo ya kimataifa, ambayo ujenzi wake umesimama kwa takriban miezi 22, ikikamilika itahudumia mabasi 300 kwa siku, na kati ya hayo, mabasi 72 yanaweza kuegeshwa kwa wakati mmoja.

Pia, stendi hiyo itakuwa na ofisi, maduka, migahawa, hoteli, maegesho ya magari binafsi 218, teksi 34, bajaji na bodaboda 20.

Kukamilika kwa mradi huo kutaifanya Manispaa ya Moshi kuwa mojawapo ya manispaa zitakazokuwa na stendi za mabasi zenye ubora zaidi nchini na ukanda wa Afrika Mashariki.

Akiwasilisha taarifa ya mwaka ya LAAC bungeni leo, Februari 13, 2025, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Halima Mdee, amesema ukaguzi uliofanywa kwenye mradi wa ujenzi wa Stendi ya Ngangamfumuni, ulioanza kutekelezwa Januari 28, 2019, ulikuwa na gharama ya Sh28.86 bilioni. Hata hivyo, ujenzi huo umesimama kwa miezi 22, hali iliyosababisha ongezeko la Sh565.09 milioni katika gharama za mradi huo.

Amesema muda wa awali wa ukamilishaji kwa mujibu wa mkataba ulikuwa Januari 28, 2021, lakini baada ya ongezeko la muda, ulikuwa ukamilike Novemba 12, 2021.

Mdee amesema mradi huo ulisimama Mei 14, 2022, kutokana na kukosekana kwa fedha za kutekeleza mradi kwa wakati. Hadi Kamati inafanya ukaguzi wa mradi huo, Sh7.85 bilioni kutoka Serikali Kuu na Sh820 milioni kutoka mapato ya ndani zilikuwa zimeshalipwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi, na kufanya jumla ya fedha iliyotumika kuwa Sh8.30 bilioni, ambayo ni sawa na asilimia 29 ya fedha zote za mradi.

Kutokana na ucheleweshaji huo, Bunge limeazimia kwamba Serikali ihakikishe inakamilisha miradi yote viporo kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi mipya ili lengo la uanzishwaji wa miradi hiyo lifikiwe.

Pia, Bunge limeazimia kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa kina katika miradi yote yenye changamoto.

Bunge pia limeazimia kuwa CAG afanye ukaguzi wa kina katika miradi yote yenye changamoto kwenye halmashauri, ambayo imejengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), na kubaini iwapo kuna thamani ya fedha.

Akizungumzia changamoto kwenye miradi ya TBA, Mdee ametoa mfano wa jengo la Halmashauri ya Kilosa, ambapo halmashauri hiyo iliingia mkataba na mkandarasi TBA kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala kwa gharama ya Sh3.7 bilioni. Mradi huo ulianza kutekelezwa Agosti 2023 na ulitarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 10, 2026.

Hata hivyo, amesema hadi halmashauri hiyo inatoa maelezo mbele ya Kamati, utekelezaji wa mradi huo ulikuwa umesimama, huku Sh1 bilioni, sawa na asilimia 26 ya fedha zilizotengwa, ikiwa imeshalipwa, wakati utekelezaji wa mradi ulikuwa umefikia asilimia 22.6.

Mfano mwingine ni ujenzi wa hospitali ya wilaya katika Halmashauri ya Mji Ifakara, ambapo mkandarasi (TBA) hadi wakati Kamati inakutana, malipo yalikuwa yamefanyika kwa asilimia 100, lakini ukamilikaji wa mradi kwa wastani wa majengo yote ulikuwa asilimia 65.

“Dosari iliyobainika katika mradi huu ni fedha zote kutumika huku majengo yakikosa kukamilika kwa wakati uliopangwa. Halmashauri bado inahitaji Sh342.9 milioni ili kukamilisha mradi huu,” amesema.

Wabunge na Serikali wazungumza

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema ni kweli kuna maeneo ambapo miradi haijatekelezwa kwa asilimia 100, lakini imetokana na mazingira yaliyojitokeza, ikiwa ni pamoja na mporomoko wa udongo uliotokea Hanang, mkoani Manyara.

“Hakuna mradi utakaobaki gofu kwa sababu fedha hazikuvuka mwaka kutokana na bajeti ya mwaka ule kutotosheleza. Hata miradi ambayo ilikumbwa na changamoto katika kipindi kilichopita, tutaendelea kuzungumza ndani ya Serikali ili kuhakikisha inakamilika,” amesema.

Akichangia taarifa hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya, amesema maazimio ya Bunge hayatekelezwi kwa kiwango kinachotakiwa, akibainisha kuwa ni asilimia 90 ya maazimio ya Bunge yaliyotolewa mwaka jana hayajatekelezwa na Serikali.

“Maazimio ya Bunge yaliyotekelezwa ni asilimia 10. Hii ni dharau kwa Bunge. Huku ni kufanya kazi kwa mazoea, kwamba LAAC watakuja, watawasilisha, watu watasikiliza, watachangia, sisi tutajibu na maisha yanaendelea. Hatuwatendei haki Watanzania, hatulitendei haki Bunge,” amesema.

Mbunge wa Nungwi (CCM), Simai Hassan Sadick, amesema changamoto zilizopo katika miradi hiyo ni ndogo kuliko faida inayopatikana, huku akieleza kuwa changamoto hizo zinatokana na kukosekana kwa tathmini ya kina wakati wa utekelezaji.

“Miradi mikubwa kama elimu na afya tunapaswa kuwekeza katika maeneo makubwa yanayotosheleza mahitaji ya sasa na baadaye. Kwa sababu sasa hivi tunaweza kujenga, lakini baada ya miaka miwili hatuwezi kupanua kwa kuwa hatuna eneo jingine,” amesema.

Naye Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba, amesema wanapokea mapendekezo ya kamati hiyo na watayafanyia kazi. Pia, amesema wamefanya mapitio ya gharama za miradi kulingana na jiografia ya eneo husika.

“Katika mwaka 2025 tunatarajia kutumia viwango vipya vya gharama ambavyo vitahakikisha miradi inakamilika na bajeti zinazotengwa zinatosheleza,” amesema.

Ametoa mfano kwamba, katika mapitio hayo, ujenzi wa madarasa utatofautiana kikanda, ambapo gharama zitakuwa kati ya Sh22 milioni hadi Sh25 milioni, huku ujenzi wa zahanati ukigharimu kati ya Sh288 milioni hadi Sh358 milioni, kulingana na maeneo husika.

Related Posts