Kidato cha nne, shahada waitwa ajira Zimamoto

Dar es Salaam. Vijana waliohitimu kidato cha nne na shahada wanatarajiwa kunufaika na ajira ngazi ya Konstebo wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo leo, Alhamisi, Februari 13, 2025, imetangaza mchakato wa ajira hizo, likiainisha sifa na vigezo vinavyohitajika kujiunga na Zimamoto na Uokoaji. Hata hivyo, haijaeleza idadi ya nafasi hizo za ajira.

Miongoni mwa vigezo vilivyoainishwa ni mwombaji kuwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa, mwenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 25, na urefu usiopungua futi 5.7 kwa wanaume na futi 5.4 kwa wanawake.

Pia, awe na afya njema kimwili na kiakili, hajawahi kutumia aina yoyote ya dawa za kulevya, hajaoa wala kuolewa, hajawahi kuajiriwa serikalini, asiwe na kumbukumbu za uhalifu wala alama za kuchorwa mwilini (tattoos).

“Anatakiwa kuwa na cheti cha kuzaliwa, kitambulisho au namba ya utambulisho iliyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA), na kuwa tayari kuhudhuria mafunzo ya taaluma ya Zimamoto na Uokoaji,” inaeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga.

“Vijana wenye elimu ya kidato cha nne au sita ambao wana ujuzi wa udereva wa magari makubwa, ufundi bomba, uuguzi, taaluma ya Zimamoto na Uokoaji, utabibu na urubani wa helikopta wanatakiwa kuhakikisha wanakidhi vigezo vilivyoainishwa hapo awali,” imeelezwa.

Taarifa imeeleza kuwa kwa wenye taaluma ya urubani wa helikopta wanatakiwa kuwa na umri wa kuanzia miaka 18 hadi 35, huku madereva wanatakiwa kuwa na leseni ya daraja E na umri wa kuanzia miaka 18 hadi 28.

Kwa wenye elimu ngazi ya shahada katika fani za uhandisi bahari, ndege, lugha (Kiingereza), ukadiriaji majenzi, teknolojia ya habari, uchumi, sheria (waliohitimu Shule ya Sheria kwa vitendo), ualimu, usafirishaji barabara na reli, na uhandisi wa kemikali wanatakiwa kukidhi vigezo vya jumla vilivyoainishwa. Umri ukiwa kuanzia miaka 18 hadi 28.

Waombaji wanatakiwa kutuma maombi kupitia mfumo wa ajira wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji unaopatikana kupitia kiunganishi cha ajira.zimamoto.go.tz. Mwisho wa kutuma maombi ni Februari 28, 2025.

Taarifa imewataka waombaji kuhakikisha wanaambatanisha barua ya maombi iliyoandikwa kwa mkono, nakala ya cheti cha kuzaliwa, fomu ya uthibitisho wa siha njema kutoka kwa mganga wa Serikali, nakala ya Kitambulisho cha Taifa au namba ya NIDA, picha ya pasipoti ya hivi karibuni, na namba ya mtihani wa kidato cha nne.

Related Posts