Unguja. Wakati Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Said Kiondo Athumani akikabidhiwa mikoba rasmi kuendesha taasisi hiyo, mambo kadhaa yanamsubiri ikiwamo kuzungumza na wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari.
Pia, anapaswa kuweka mikakati kuhakikisha wafanyabiashara wanatoa risiti za kielektroniki kwa kuwa, wengi wanatajwa kukwepa jukumu hilo kwa kisingizo cha mashine kukosa mtandao.
Kiondo anachukua nafasi ya Yusuph Mwenda aliyeteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Julai mwaka 2024 kuwa Kamishana Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) nafasi iliyoachwa na Alphayo Kidata aliyeteuliwa kuwa mshauri wa Rais katika masuala ya kodi.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa ofisi, Kiondo aliyewahi kuwa Kamishna wa Forodha TRA, amesema ana uzoefu wa kutosha katika makusanyo, hivyo anataka kuongeza mapato ya mamlaka hiyo zaidi ya inachokikusanya sasa.
Kiondo aliyeteuliwa Februari 8, 2025 akitokea Chuo cha Kodi cha Mamlaka ya Mapato Tanzania, aliapishwa Februari 12, 2025 na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi Ikulu Zanzibar.
Mdau wa masuala ya kodi na uchumi, Said Haji amesema bado changamoto kubwa ipo kwenye utoaji wa risiti za kielektroniki kwa kuwa, wafanyabiashara wengi hawatoi risiti kisa mtandao, kwa hiyo bado kuna elimu kubwa inatakiwa kushughulikia jambo hilo.
“Kuwa karibu na wafanyabiashara, kutoa elimu ya mara kwa mara akilifanikisha hili huenda akaongeza kweli mapato mara dufu, lakini bado kuna kodi nyingi inapote katika misingi hiyo,” amesema.
Akizungumza na kamati ya uongozi, Kiondo amesema ni mgeni katika ofisi hiyo lakini mwenyeji kwenye ukusanyaji kodi kwa kuwa, ameifanya kazi hiyo kwa miaka 25, akisema kikubwa anachoomba kwa watendaji hao ni kumtendea wema na kumpa ushirikiano katika ukusanyi wa kodi.
“Ninachoomba kwenu mnipokee na mnitendee wema, na kutenda wema ni rahisi sana, ni kunipa ushirikiano, kunisaidia na kutimiza wajibu tuliopewa, nipo kwenye kukusanya kodi miaka 25 sio kidogo nimekutana na mishale na marungu.
“Kama tunakusanya Sh70 bilioni kwa mwezi basi tukusanye na tupite hapo zaidi,” amesema Kiondo.
Amesema kila mmoja ajinasibu na kujisikia fahari kuwa mfanyakazi wa ZRA ikiwa na jina linalosifika na sio kuifanya taasisi ifanye vibaya na kuanza kuona aibu hata kutajwa kuwa mfanyakazi wa mamlaka hiyo.
“Hatutegemei tuanze kujificha, hupendi kusikia mtaani kwamba wewe ni mfanyakazi wa ZRA, tunapaswa tujinasibu na taasisi yenye jina zuri na wasifu kila mmoja ajisikie fahari na kujinasibu nayo,” amesema Kiondo.
Amesema kazi hiyo inahitaji mipango na mikakati ya kutosha kwa kuwa, watu wengi wanapenda pesa na sio rahisi kutoa na kumpa mtu.
Amesema ZRA itahakikisha inakaa na walipa kodi na kuwahimiza, kuwafundisha, kuwashawishi pamoja na kutumia utaalamu walionao ili waweze kulipa kodi kwa hiari.
“Zama hizi sio zile za kufukuzana huku na kule, kufanya vurugu bali ni zama za kushawishiana kila mtu aone umuhimu wa kulipa kodi, kwani kodi inarudi kwetu kwa ajili ya kuimarisha huduma za jamii,” amesema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya Salum amesema ZRA imekuwa ikifanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na mafanikio hayo yanatokana na mageuzi makubwa yaliyofanyika.
Amesema awali yalikuwepo mambo yanayoifanya ZRA kutofanya vizuri zaidi na masuala ya ndani ikiwamo ufujaji wa fedha na baadhi ya watumishi kutokuwa waaminifu na mifumo.
Waziri Saada amesema kwa sasa wastani wa makusayo ya ZRA yanapindukia zaidi ya asilimia 100 ambayo ni mafanikio makubwa.
“Hivi sasa tunakusanya Sh70 bilioni kutoka Sh30 bilioni kwa mwezi na tunajua bado Zanzibar ina nafasi ya kufanya vizuri zaidi ikiwa tutasimamia mifumo, uadilifu na ikiwa sera zetu zitakwenda vizuri tunaamini tutaondoka hapa tulipo na kwenda juu zaidi,” amesema Waziri Saada.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZRA, Profesa Hamed Rashid Hikmany amesema watampa ushirikiano watumishi hao na wasiridhike na kile wanachokusanya huku akikumbushia kutumia lugha ya kuelekeza zaidi kuliko kufoka.
Aliyekuwa Kaimu Kamishna Mkuu, Said Ali Mohamed amesema watahakikisha wanampa ushirikiano kwa kuwa kazi hiyo hawezi kuifanya peke yake.
“Hatutakuacha kwamba hili ni jukumu lako, tutakuwa pamoja hii ni kazi yetu sote tukishirikiana tutafikia malengo,” amesema Said.