Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar Shaib Ibrahim Muhammed amewataka Watendaji na Wafanyakazi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar na Baraza la Vijana Zanzibar kuwa na mashirikiano katika utendaji wao wa kazi ili kuleta ufanisi wa Taasisi hizo zinazoshughulikia masuala ya Vijana Zanzibar.
Kauli hiyo ameitoa huko Ukumbi wa Ofisi ya Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Kikwajuni Weles alipokuwa akizungumza na watendaji na wafanyakazi wa Taasisi hizo mbili katika kikao mkakati cha kuimarisha mashirikiano ya utendaji wa kazi kwa lengo la kuleta maslahi ya Vijana wa Zanzibar.
Amesema Taasisi hizo zinatakiwa kufanya kazi kwa pamoja ili kuwaunganisha Vijana bila ya kujali tofauti zao za kisiasa , kidini na kijamii kwa misingi ya kuwa Baraza la Vijana Zanzibar linaunganisha makundi yote ya Vijana.
Aidha amesema Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Zanzibar kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana imekusudia kujenga Vituo vya Mafunzo ya Vijana katika Mikoa yote ya Zanzibar.
Kwa upande wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan amesema Baraza la Vijana limeandaa mikakati ya kuimarisha mabaraza ya Vijana ya Shehia moja ya mikakati hiyo ni kutumia falsafa ya K5.
Aidha amewataka watendaji hao kuwahamasisha Vijana kujiunga na Baraza la Vijana Zanzibar kutoka makundi tofauti ndani ya jamii.
Pia amesema kuna umuhimu mkubwa kwa Maafisa Vijana wa Wilaya kushirikiana kwa pamoja katika utendaji wao kazi kuhakikisha wanasimamia kampeni ya kuimarisha mabaraza ya Vijana na kasi ya kuingiza Wanachama wapya kujiunga na Baraza hilo.
Akitoa Ushauri Afisa Maendeleo ya Vijana Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka Pemba Zadida Abdalla Rashid amesema ni vyema kwa Watendaji hao kutumia Vyombo vya Habari na Mitandao ya kijamii kuielimisha jamii kulifamu Baraza la Vijana Zanzibar na malengo ya kuanzishwa kwake hapa Zanzibar pamoja na kuvitangaza Vituo vya Mafunzo ya Vijana vilivyokuwepo Zanzibar.
Aidha Mkuu wa Divisheni ya Uwezeshaji na Uhamasishaji Vijana Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar Juma Rashid Ali amesema ni vyema kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi hizo kuendelea kushirikiana ili Vijana wapate kufaidika kupitia Taasisi hizo mbili za Vijana hapa Zanzibar.
Katika kikao hicho mambo mbalimbali yalijadiliwa kwa pamoja ikiwa ni pamoja na kujadili Vipaumbele vya Idara ya Maendeleo ya Vijana Zanzibar na Baraza la Vijana Zanzibar kwa Mwaka 2025/ 2026.