Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali na kumpangia kituo cha kazi Balozi Habib Galuss Kambanga kuwa balozi wa Tanzania nchini Rwanda.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habri iliyotolewa leo Alhamisi Februari 13, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka imesema Rais Samia amemteua Dk Amina Suleiman Msengwa kuwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali.
Taarifa inasema kabla ya uteuzi huu, Dk Msengwa alikuwa mhadhiri mwandamizi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anachukua nafasi ya Dk Albina Chuwa ambaye amemaliza muda wake.
Rais Samia amemteua Jaji Ntemi Nimilwa Kilekamajenga kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Masoko na Mitaji.
Jaji Kilekamajenga anachukua nafasi ya Jaji Deo Nangela ambaye aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Profesa Aurelia Kamuzora ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Kahawa ambapo ameteuliwa kwa kipindi cha pili.
Pia, amemteua Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania na anachukua nafasi ya Mustafa Hamis Umande ambaye amemaliza muda wake.
Mbali na hao, Rais Samia amemteua Profesa Hozen Kahesi Mayaya kuwa Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kwa kipindi cha pili.