Rais Samia kufanya ziara Ethiopia, kushiriki mkutano AU

Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi nchini Ethiopia kuanzia Februari 15 hadi 16 sambamba na ziara hiyo atashiriki mkutano wa Umoja wa Afrika (AU).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Februari 13, 2025 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga, imeeleza kuwa mkutano huo utamchagua mwenyekiti mpya wa AU.

“Rais Samia atashiriki mkutano wa kawaida wa 38 wa wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).

“Mkutano huo unatarajia kuchagua mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2025 atakayechukua nafasi ya mwenyekiti wa sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Pia, mkutano huo pia utachagua viongozi wapya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ikiwemo mwenyekiti, makamu mwenyekiti na makamishna sita.

“Vilevile, mkutano utajadili taarifa ya ushiriki wa Umoja wa Afrika kwenye Mkutano wa Nchi Tajiri Duniani (G20), utekelezaji wa ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na taarifa kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

“Mbali na masuala hayo, Mkutano utajadili ajenda kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia iliyopendekezwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” imeeleza taarifa hiyo.

Kabla ya kushiriki mkutano wa 38, Rais Samia atashiriki mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika utakaofanyika Februari 14, 2025.

Related Posts