Moshi. Mkuu Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewaagiza wakuu wa wilaya zote mkoani huo kukamata na kuondoka na gololi na fimbo zinazotumika kuchezea ‘pool table’ muda wa kazi.
Amesema kumeibuka wimbi la vijana kutojihusisha na shughuli zozote za kiuchumi na badala yake wakati wa saa za kazi wamekuwa wakicheza michezo hiyo ambayo ni hatari kwa maendeleo ya mkoa huo.
Mbali na kupambana na wacheza ‘pool table’, pia amewajia juu wakuu wa wilaya kwa kutosimamaia ipasavyo sheria ya vileo na kuruhusu pombe kuuzwa na kunyweka asubuhi na mchana wakati wa saa za kazi.
Akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) cha kujadili mapendekezo ya bajeti ya mwaka ya 2025/26 mkuu huyo, amesema baadhi ya vijana mkoani humo wamekuwa wakijihusisha na ulevi na uchezaji wa ‘pool table’ saa za kazi.
“Ni kweli pombe zimezidi, waheshimiwa wakuu wa wilaya mmeruhusu ‘pool table’ zinachezwa ovyo mtaani, watu hawafanyi kazi, unakuta wameibia watu huko wanakwenda kucheza ‘pool table’ muda wa kazi,”amesema na kuongeza;
“Nataka niwape ruhusa nyie mkifika mkiona meza ya ‘pool table’ simamisha gari chukua zile gololi zao na ile fimbo weka kwenye gari yako, nimefanya sana mimi hiyo kazi,” amesema.

Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Kilimanjaro,wakiwa katika kikao cha kamati ya ushauri (RCC)
Aidha, amewataka wakuu hao, kuhakikisha sheria za kufungua sehemu za vileo zinazingatiwa na hazikiukwi.
“Tumesema zipo sheria za kufunguliwa kwa ‘bar’ kwa nini ‘bar’zinafunguliwa asubuhi,”amehoji Babu.
“Sasa hivi tukitoka hapa twendeni kwenye hizo ‘bar’ kama hamjakuta watu wanalewa, wanafanya kazi sangapi? vijana wanalewa ovyo, wewe ukienda kwenye ziara ukikuta watu wanakunywa mbege pakia mapipa yale ondoka nayo, si ni sheria? nani atakulalamikia.
“Ni kweli watu wanalewa, ukienda maeneo ya Hai, Rombo, Siha, Same, Mwanga na Moshi utakuta, hatuwezi kupoteza nguvu kazi, Mheshimiwa Rais analeta fedha nyingi kwa ajili ya kujenga shule, barabara, umeme, maji, huduma za afya, tunakwenda kulewa?, pombe nyingine hazina majina watu wanakunywa tuu,” amesema.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Simon Maigwa amesema suala la kudhibiti unywaji wa pombe linahitaji nguvu za pamoja kwa kuhakikisha sheria zote zilizowekwa zinafuatwa.
“Viongozi wetu waliopo katika maeneo haya watupe ushirikiano, kwa sababu gongo zinapikwa katika maeneo mbalimbali, wapo viongozi kwenye maeneo hayo, lakini wanasubiri mpaka polisi aende, wewe umechaguliwa kwa ajili ya kulinda raia na mali zao pamoja na afya za hawa wananchi,” amesema Maigwa.
“Lakini, hata hivi vilevi kidogo vinachanganya kwa sababu duka la kuuza bidhaa kule ndani utakuta kuna pombe kali, hapo sijui sheria ya vilevi inasemaje kuchanganya vilevi na bidhaa za kawaida,” amehoji RPC.
Amesema ipo haja ya sheria zilizowekwa kuzingatiwa na sio kutegemea taasisi moja kusimamia.
“Mimi ninachokiona sheria ndogo zisimamiwe muda wa kunywa, sasa hii inaonekana taasisi moja ndio imeachiwa,” amesema RPC
Kamanda Maigwa amesema, suala la ‘molasesi’ kutoka viwandani liangaliwe kama matumizi yake ni sahihi kwa kuwa baadhi yao huchukua na kwenda kutengenezea pombe haramu aina ya gongo badala ya kulishia wanyama.
“Kibaya zaidi mahali wanapopikia wanapikia kwenye vyanzo vya maji ambavyo vinaathiri afya za watu kwa sababu yale maji tunatumia, ombi langu ili tuweze kukomesha tuwe na muunganiko wa pamoja,” amesema.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala ameshauri mambo matatu ili kukabiliana na tatizo la ulevi ikiwemo, kuwekwa nguvu ya pamoja, sheria kufanyiwa mapitio na baadhi ya vilevi vilivyothibitishwa na TBS kuangaliwa upya kutokana na gharama zake kuwa ndogo.
“Vita hii ya ulevi tunapaswa kuipiga kwa pamoja Mkoa wa Kilimanjaro, kwani tatizo hili liko maeneo yote ya mkoa huu na changamoto kubwa tunayoiona ni kwamba kuna maeneo mengine vilevi vimepimwa na TBS, lakini ni hatari, kwa sababu ukipima unakuta kiwango chake cha kilevi ni kikubwa na kinauzwa Sh300 au Sh 500. Mtu akipiga viwili amezimika lakini vinaviwango vya TBS na mwisho wa siku unakuta mtu unapambana na gongo, lakini kumbe kuna kinywaji kingine ukikipima ni hatari zaidi.”
Ameongeza kuwa “Mimi nilikuwa napambana na gongo lakini ukija kuangalia kuna pombe zimepitishwa ambazo zinauzwa bei nafuu sana. Lakini, suala lingine ni namna adhabu inayotolewa watu wakikamatwa, sheria zetu lazima zifanyiwe mapitio kwani unaweza kukuta mtu anakamatwa kwenye tatizo hili, lakini akienda mahakamani faini yake ni Sh20,000 au 30,000”.