Sowah avunja rekodi ya JKT Tanzania

BAO la dakika ya 51 la mshambuliaji wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah limetosha kuvunja rekodi ya JKT Tanzania ya kutokufungwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo msimu huu, baada ya mwenendo mzuri wa kikosi hicho cha Maafande.

Sowah amefunga bao hilo likiwa ni la pili kwake katika Ligi Kuu Bara tangu ajiunge na timu hiyo dirisha dogo akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya, ambapo amevunja rekodi hiyo baada ya JKT Tanzania kucheza michezo minane bila ya kupoteza.

JKT ilikuwa inashikilia rekodi bora ya timu ambazo hazijapoteza zikiwa nyumbani kwani kabla ya mchezo wa leo, timu hiyo ilikuwa imecheza michezo tisa ya mashindano yote, ambapo kati yake minane ni ya Ligi Kuu Bara na mmoja wa Kombe la FA.

Katika michezo minane iliyocheza JKT ya Ligi Kuu Bara imeshinda mitatu na kutoka sare mitano, huku mmoja pekee ambao ni wa Kombe la FA wa hatua ya 64 bora, ulishuhudia kikosi hicho kikishinda mabao 5-1, dhidi ya Igunga United kutoka Tabora.

JKT iliingia katika mchezo huu ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuilazimisha suluhu Yanga mechi ya mwisho, huku kwa upande wa Singida ikiwa na machungu makali baada ya kushuhudia ikichapwa mabao 2-0, dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa KMC Complex.

Kichapo hiki kwa JKT kinaifanya kufikisha jumla ya michezo minane ya Ligi Kuu Bara bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Fountain Gate bao 1-0, Novemba 29, mwaka jana, ambapo kati yake imepoteza minne na kutoka pia sare minne.

Kiujumla matokeo haya yanaifanya JKT kufikisha michezo 19 ya Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hiyo imeshinda minne tu, sare minane na kupoteza saba, ikifunga mabao 11 na kuruhusu 15, huku ikishika nafasi ya 10 kwenye msimamo na pointi zake 20.

Kwa upande wa Singida huu unakuwa ni ushindi wake wa kwanza kwa kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Mkenya David Ouma tangu ateuliwe Februari 5, mwaka huu akichukua nafasi ya Miloud Hamdi aliyejiunga na Yanga Februari 4, kurithi mikoba ya Sead Ramovic.

Ouma aliyekuwa msaidizi wa Miloud aliyetambulishwa Desemba 30, mwaka jana akichukua nafasi ya Patrick Aussems, alianza kukiongoza kikosi hicho katika sare ya mabao 2-2, dhidi ya Kagera Sugar, kisha kuchapwa 2-0, na KMC, mechi iliyopita.

Kabla ya mchezo wa leo, Singida mara ya mwisho kushinda ilikuwa Desemba 24, mwaka jana ilipoichapa KenGold mabao 2-1 na kuanzia hapo ilikuwa imecheza michezo yake minne ambapo kati ya hiyo imeshinda mmoja, sare mmoja pia na kuchapwa miwili.

Matokeo haya yanaifanya Singida kuendelea kusalia nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi na pointi 37, baada ya kucheza michezo 19, ikishinda 11, sare minne na kupoteza pia minne, ikifunga jumla ya mabao 25 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa 15.

Akizungumza baada ya mchezo huo Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally alisema ilikuwa ni siku mbaya kazini kutokana na jinsi walivyocheza, huku akieleza kichapo hicho kimetokana na mabadiliko ya lazima ya wachezaji wawili dakika 45 za kwanza.

“Kipindi cha kwanza tulifanya mabadiliko ya lazima ya beki, Wilson Nangu na kiungo Hassan Kapalata ambao walishindwa kuendelea na mchezo kutokana na uchomvu walioupata, nimesikitishwa na matokeo hivyo niseme tumekuwa na siku mbaya.”

Kwa upande wa kaimu kocha wa Singida, David Ouma alisema ushindi huo ni muhimu kwao baada ya kutokuwa na mwenendo mzuri huku akiomba mashabiki wa timu hiyo kuendelea kumpa muda, ili aweze kutengeneza kikosi bora na cha ushindani msimu huu.

Related Posts