Addis
Ababa, 13 Februari 2025.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeshinda
nafasi mbili zilizokuwa zikigombewa katika uchaguzi wa Taasisi za Umoja wa
Afrika ambazo ni nafasi ya Mjumbe wa Tume ya Umoja wa Afrika inayohusiana na
Sheria za Kimataifa iliyokuwa ikigombewa na Prof. Kennedy Gastorn na nafasi ya
Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Umoja wa Afrika dhidi ya Rushwa iliyokuwa
ikigombewa na Bw. Benjamin Kapera.
Prof. Kennedy Gaston ameshinda kura 45 kati ya
48 na Bw. Benjamini Kapera ameshinda kwa kura 33 kati ya 48 zilizopigwa na
kikao cha 46 cha Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika na kuibuka washindi
katika nafasi husika.
Uchaguzi huo umefanyika tarehe 13 Februari,
2025 wakati wajumbe wa Baraza hilo wakiwa katika hatua za mwisho za maandalizi
ya nyaraka za Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika tarehe
15 na 16 Februari, 2025.
Zoezi la uchaguzi huo lilienda sambamba na
kunadi wasifu na uwezo wa wagombea kiutendaji ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) na
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ethiopia ambaye pia ni
Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya
Uchumi Afrika (UNECA), Mhe. Innocent Shiyo waliongoza mchakato huo.
Wajumbe hao walioshinda watawakilisha kanda ya
Mashariki wakiungana na wajumbe wengine kutoka katika kanda za Magharibi,
Kaskazini, Kusini na Kati katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo.
Nafasi ya Ujumbe wa Tume ya Sheria za Kimataifa ni miaka mitano (5) na ujumbe
wa Bodi ya Masuala ya Rushwa ni miaka (6).
Pamoja na nafasi hizo Waziri Kombo ametumia pia
fursa ya kikao hicho cha Mawaziri kumnadi mgombea wa nafasi ya Mkurugenzi wa
Shirika la Afya Duniani – Kanda ya Afrika, Prof. Mohamed Janab.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano
ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.