Ulega ashauri wataalamu kufikiria magari binafsi kulipia barabara mwendokasi

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema endapo foleni za magari zitapungua maeneo ya mijini zitaiongezea mapato Serikali, huku akiwataka wataalamu wa wizara hiyo, kuutumia Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi kubuni njia za kuondokana na tatizo hilo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mkutano wa baraza hilo, unaofanyika mkoani Singida, Waziri Ulega amesema pamoja na mkutano huo kuwa na ajenda zake za kawaida kisheria, lakini ni muhimu kama ya foleni ambayo yanagusa wananchi wengi yakajadiliwa kwa kina kwa kikao hicho kimesheeni wataalamu wa kutosha.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Februari 13, 2025 kwa vyombo vya habari imeeleza hayo huku ikifafanua waziri huyo amesema anaona fursa ya kupunguza kero ya foleni na Serikali kujiongezea mapato endapo ubunifu utafanywa kwenye maeneo ambako kuna barabara za Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).

“Hivi hakuna namna ambayo kwa kulipia, magari ya kawaida yanaweza kutumia barabara endapo njia za kawaida zitakuwa na foleni? Kwa nini barabara moja ikae nusu saa bila gari kupita wakati kwingine hakuendeki kwa sababu ya foleni,” amehoji.

“Kwenye daraja la Mwalimu Nyerere tunafanya hivyo tayari kwa mfumo wa PPP na watu wanalipa kuvuka daraja. Nchi nyingine watu wanalipia kutumia baadhi ya barabara kama hawataki foleni, tunaweza kufanya kitu lakini tunahitaji wataalamu mtushauri,” amesema Ulega.

Katika hatua nyingine, Ulega amewaagiza watumishi wa Wizara ya Ujenzi kuhakikisha wanazingatia thamani ya fedha wakati wa utekelezaji na usimamizi wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo barabara, madaraja, vivuko, majengo ya Serikali na viwanja vya ndege.

“Endeleeni kuunga mkono dhamira hii njema ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana kwenye miradi mnayoisimamia,” amesema Ulega.

Ulega ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanrodas) kuongeza juhudi za usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya dharura ya miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua El-Nino na Kimbunga Hidaya yenye thamani ya Sh868.56 bilioni.

Waziri Ulega ameelekeza wizara hiyo, kushirikiana na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), kuhakikisha dhana ya uwezeshaji wa makandarasi wa ndani inatekelezwa kama ilivyokusudiwa ili kunufaisha na kuwajengea uwezo watalaamu hao.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuufungua mkoa huo kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara za lami zilizosaidia kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Aisha Amour amesema wizara hiyo, inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikwemo ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato, daraja la Kigongo- Busisi na miundombinu ya BRT jijini Dar es Salaam.

Mkutano wa baraza la wafanyakazi la sekta ya ujenzi umefanyika mkoani Singida ukiwa na ajenda mkutano ni kupokea, kujadili na kuidhinisha bajeti ya wizara hiyo,kwa mwaka wa fedha 2025/26 kabla ya kusilishwa bungeni.

Related Posts