Vuguvugu la mabadiliko: Chadema kuanza ziara kusini

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Heche amesema kuanzia mwezi ujao chama hicho kitaanza ziara ya mikoa ya kusini ili kuunganisha nguvu za Watanzania katika kudai haki kwenye mfumo wa uchaguzi.

Heche ambaye ni mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini mkoani Mara amesema katika ziara hiyo, viongozi wakuu wa Chadema watawaambia Watanzania kuwa kama ‘Hakuna mabadiliko, Hakuna uchaguzi’ (No Reforms, No Elections).

Kiongozi huyo ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 13, 2025 wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Sirari wilayani Tarime mkoani Mara. Katika hotuba yake Heche amesisitiza chama hicho, hakitaruhusu uchaguzi ufanyike pasipokuwepo na mabadiliko ya mfumo wa mchakato huo.

Uwepo wa ziara hiyo, uligusiwa jana Jumatano Februari 12, 2025 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu aliyekuwa akihutubia Watanzania ambapo aligusia kwamba wataanza ziara ya kutembelea kanda zote 10 za Chadema ili kuzungumza na wananchi kuwaambia maana ya ‘No Reforms No Elections.

Kwa mujibu wa Heche, pamoja na kufanya ziara hiyo, lakini Chadema watazungumza na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini asasi za kirai na mashirika ya kimataifa yatakayaoelezwa maana ya No Reforms, No Elections ili kuungwa mkono katika vuguvugu hilo.

“Tutazungumza na kila taasisi kwenye nchi hii, si mlimuona mwenyekiti wetu (Tundu Lissu), alikuwa anazungumza na Mzee Warioba (Jaji Joseph), tutazungumza na watu maarufu tukiwaomba watuunge mkono,” amesema Heche.

Februari 10, 2025 zilisambaa picha katika mitandao ya kijamii zikumuonyesha Lissu, Aman Golugwa (Naibu katibu mkuu wa Chadema bara), wakiwa pamoja na Jaji Warioba walipomtembelea nyumbani kwake waziri mkuu huyo mstaafu.

Picha hizo ziliambatana na ujumbe ulioeleza:“Katika ziara hiyo, Lissu amekuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu mstaafu kuhusiana na masuala mbalimbali ikiwemo uchaguzi wa ndani ya chama uliomalizika hivi karibuni, uchaguzi serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2024 pamoja na ulazima wa kuwa na mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi Tanzania ili kuwa na chaguzi zilizo za huru na haki.”

Related Posts