Dar es Salaam. Licha ya mapokezi chanya ya wadau wa demokrasia kuhusu vuguvugu la mabadiliko lililotangazwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa upande mwingine wameonyesha wasiwasi wa kufanikiwa kwa hoja hiyo katika muda mfupi uliobaki kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Wapo wanaoona, miezi iliyosalia kuelekea inatosha kufanya mabadiliko yoyote ya kisheria, kisera na kikatiba kuhusu mifumo ya uchaguzi na wengine wakilitazama jambo hilo tofauti.
Wanaosema muda unatosha wanajenga hoja zao kuwa, Serikali ina nafasi ya kupeleka muswada wa dharura bungeni wakati wowote, ili mabadiliko madogo ya Katiba yafanyike kuruhusu sheria Tume ya Huru Taifa ya uchaguzi mwaka 2024 ianze kufanya kazi.
Wenye mtazamo tofauti na huo, wanasema ni muhimu kuutumia muda uliobaki kuhamasisha wananchi wajitokeze kupiga kura kwenye uchaguzi huo, wakidai “upo uwezekano wa kupata wabunge wengi kwa sheria zilizopo”, wakirejea uchaguzi wa mwaka 2015.
Mitazamo hiyo tofauti ionatokana na msimamo wa Chadema uliotangazwa Februari 12, 2025 na Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, ambapo pamoja na mambo mengine, alitangaza nia ya kualika makundi yenye ushawishi katika jamii kujiunga na vuguvugu la mabadiliko, la kushinikiza mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.
Vuguvugu hilo, ni utekelezaji wa msimamo wa chama hicho wa kutoruhusu uchaguzi mkuu ufanyike, bila mabadiliko ya kisera, kisheria na kikatiba wa “No reforms, No election.”
Katika hotuba hiyo ya kwanza ya Lissu tangu achaguliwe mwenyekiti, alisema atazifuata asasi za kiraia, kidini, jumuiya ya kimataifa, viongozi wa kisiasa, wanahabari kuomba ziunge mkono vuguvugu hilo kwa kuzingatia maeneo yao.
Kutokana na hilo, baadhi ya taasisi za kidini zimeonyesha kuunga mkono na asasi nyingine za kiraia zikionyesha wasiwasi kuhusu muda.
Hoja ya kukosekana muda, imeibuliwa na Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Matrona Kabyemela, anayesema ni vigumu kufanikisha vuguvugu hilo ndani ya muda uliobaki.
Hata hivyo, amesema vuguvugu hilo, lilianza kitambo ingawa kwa sasa limebadilishwa jina, lakini maana ni ile ile.
“Tamko hilo limekuwepo miaka mingi na ni kitu kilichoainishwa kwenye ripoti nyingi zinazotazama uchaguzi na kuna zilizosema ili tuwe na demokrasia ya vyama vingi, lazima pawepo na mfumo huru wa uchaguzi na tume imepigiwa kelele muda mrefu,” amesema.
Kama lilikuwepo tangu muda mrefu na halikufanikiwa, Dk Matrona amesema kwa muda uliobaki haoni kama litafanikiwa kama inavyotarajiwa.
“Kufanikiwa itategemea na njia watakazotumia na mara nyingi huwa tunafanya vitu kwa kushtukiza, nadhani tusiwakatishe tamaa waendelee kusukuma hiyo ajenda lakini muda uliobaki ni mfupi sidhani kama kuna uwezekano wa kubadili chochote,” amesema Dk Matrona.
Hata hivyo, aliisihi Serikali isikilize madai hayo kwa kuwa kuna gharama kubwa imetumika kujenga mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, na kinachohitajika ni kipengele kizuri katika kudumisha uwekezaji uliofanyika.
“Kama wanaweza kusikiliza na kufanya marekebisho yatakayokuwa kikatiba zaidi lazima sheria zibadilike, ikiwezekana sawa, lakini kama haitawezekana waendelee kudai mabadiliko yanakuja taratibu,” alisema.
Mtazamo kama wa Dk Matrona ulitolewa pia na Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe aliyesema haoni jambo lolote likifanikiwa kwa muda uliobaki.
“Mwanzoni mwa mwaka 2024 tulipata sheria ya uchaguzi na ile ya Tume huru ya Uchaguzi ambayo bado hawajaridhika nayo, ilikuwa ni mabadiliko yaliyoungwa mkono na wadau wengi,” amesema.
Anaona itakuwa vigumu hasa kwa sababu, hata Bunge lililopo sasa kwa sehemu kubwa linaundwa na chama kimoja, jambo litakalofanya hoja hiyo isipitishwe kwa masilahi ya kisiasa ya wabunge walio wengi.
“Chadema wanachoongea ni sahihi, lakini sidhani kama kwa muda uliobaki unatosha kufanikiwa wanachotaka,” amesema.
Ingawa muda uliobaki hautoshi, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi anapendekeza yawepo makubaliano ya kusogeza mbele uchaguzi kutoa nafasi ya mabadiliko.
“Mchakato wa kikatiba ni mrefu na mabadiliko yake yanachukua muda mrefu, huwezi kusema ndani ya muda wa miezi minne unaweza kumaliza, lakini kama tunazungumzia mabadiliko madogo ya kutuongoza katika masuala haya muhimu, kukutana na kuweka makubaliano kama taifa muda bado upo,” amesema.
Wahariri nao, wanaona kama kuna nia ya mabadiliko ya kweli, bado kuna Bunge la Bajeti linaloweza kutumika kupeleka muswada wa kufanikisha kinachohitajika.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema: “Kuendelea kusema ‘hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi’ bila kutaja mabadiliko hayo kwa njia nzuri, sidhani kama watafanikiwa, itakuwa ni kujifurahisha kwenye mikutano ya hadhara na hawezi kupata jambo la maana.”
Hata hivyo, Balile amesema kama utafuatwa utaratibu wa kawaida, Bunge la Bajeti halipaswi kuingizwa muswada wowote na mchakato wa mabadiliko ya Katiba ni mkubwa unahitaji kukusanya maoni.
“Mchakato ni mrefu uhalisia ni kwamba kwa muda ulibakia mabadiliko hayo hayawezi kutokea, labda iwe zimamoto,” amesema.
Pamoja na kuona muda hautoshi, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini Tanzania, Juma Ali Khatibu amesema ni vema kuangalia mambo muhimu na kuishauri Serikali kuliko kuishinikiza.
“Wanachotaka kufanya Chadema si njia sahihi kulingana na muda tulionao, tuko mwaka wa uchaguzi, tutumie busara na tushauri kwa kutumia lugha za staha,” amesema.
Hoja ya muda hautoshi, ilitolewa pia na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)-Bara, Stephen Wasira aliyesema baada ya kusigana katika vikao vya maridhiano, walikubaliana kuandika Katiba baada ya uchaguzi kwa kuwa si jambo la kukurupuka.
“Katiba si uchaguzi pekee, Katiba unaweka haki za wote na wanapaswa kushiriki wakiwemo wenye ulemavu, wafugaji, wavuvi, wakulima, mamantilie kuna machinga, wote ni Watanzania, Katiba lazima ijibu matatizo ya wote,” amesema.
Wasira amesema anashangaa wanaozungumza Katiba ni kama wanazungumza uchaguzi na haki za wengi hazitazamwi, lakini msingi yote hayo yalikuwa maridhiano yaliyozaa zile sheria tatu zilizosainiwa na Rais mwaka 2024.
“Kuhusu Katiba tulikubaliana baada ya uchaguzi na ushauri huo ulitolewa na wadau na Chadema hawakushiriki, wao walitaka wasikilizwe kiupekee,” alisema.
Wakati wengine wakiona muda hautoshi, wapo wanaosema muda uliopo unatosha kufanya mabadiliko yoyote, iwapo viongozi watakuwa na utashi wa kisiasa, kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo.
“Kuna mabadiliko madogo ya sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi yalifanyika, katika hali ya kawaida ilitakiwa kuanza kazi kwa kuwa Rais alishasaini, lakini hadi leo haijaanza kufanya kazi ile sheria, ilitoa utaratibu wa upatikanaji wa watumishi wa tume,” amesema.
Dk Masabo amesema wanachotaka Chadema hata kile kidogo kilichopatikana kupitia mabadiliko madogo ya sheria, kwanza kifanyike na kinaweza kubadilisha sura nzima ya ufanyaji wa uchaguzi.
“Naona Chadema wana hoja kwa kuwa tayari sheria imepitishwa na haijatekelezwa, ndiyo maana kuna watu walienda hadi mahakamani kudai hata uchaguzi wa serikali za mitaa usimamiwe na sheria mpya na walihakikishiwa sheria zilizopo zitatenda haki, lakini kila mmoja anaona kilichotokea,” amesema.
Dk Masabo amesema wanachotaka kuna vitu vikitekelezwa kupitia mabadiliko ya sheria na ianze kufanya kazi ni lazima Katiba ifanyiwe mabadiliko kwanza, ili kuingiza masharti yaliyowekwa na hiyo sheria.
“Tukiweka kwenye Katiba, tayari tutakuwa tumejenga mfumo mpya wa uchaguzi. Unaweza ukawa si mzuri, lakini hautakuwa kama ulivyo sasa, kwa sababu sheria ile imeweka masharti ya upatikanaji wa watumishi wa tume,” amesema.
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda alisema kwenye jambo hilo kinachopaswa kutazamwa ni haki kutendeka na si muda.
“Suala la muda haliangaliwi zaidi, kinachozingatiwa ni haki inayopatikana na kinachozungumza ni hoja ya msingi zaidi, lazima tuweke misingi iliyo bora ambayo itafanya haki iweze kupatikana, ndipo tuingie kwenye jambo lenyewe,” amesema.
Sheikh Ponda amesema muda uliobaki unatosha. “Lazima hilo lifanyike ili haki iweze kutendeka na kama haki haitatendeka manaake maksudio hayafikiwi.”
Ili kufanikisha vuguvugu hilo, Matrona amesema ni muhimu vyama viungane na si Chadema peke yake kuibeba ajenda hiyo, hapo ndiko ambako aghalabu wanakosea.
“Serikali inajua namna ya kuwachezea kwa sababu kama huna nguvu ya watu nyuma una nguvu ya viongozi tu na watu wachache, huwezi kufanikiwa, kama hawajafanikiwa mara hii basi wabadilike waanzie chini kwenye matawi,” amesema.
Pia, ametaka hilo lianzie ngazi za chini za vyama isiishie kwenye maeneo ambayo vyama husika vina ngome.
Massawe kwa upande wake, ameshauri kwa muda uliobaki waingie kwenye kampeni ili kupata wabunge wengi, baadaye washiriki kufanikisha vuguvugu hilo.
Dk Masabo amesema ni muhimu sheria iliyosainiwa na Rais ikaanze kutekelezwa kwa kufanywa mabadiliko madogo ya sheria ili kuruhusu sheria hiyo ianze kutumika.