Wachekelea wingi vituo uboreshaji Daftari la Kudumu la Mpiga Kura

Tanga. Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Tanga waliojitokeza kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura wamepongeza zoezi hilo, hasa kutokana na uwepo wa vituo vingi vya kujiandikisha, hali ambayo imewasaidia kutumia muda mchache kukamilisha mchakato huo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi katika vituo mbalimbali vilivyoanza uandikishaji leo Alhamisi, Februari 13, 2025, wananchi hao wameeleza kuridhishwa kazi hiyo.

Abubakari Ali, mkazi wa Kata ya Mabawa Jijini Tanga, amesema alikumbana na makosa ya jina kwenye uandikishaji uliopita, lakini kupitia uboreshaji huu, ameweza kurekebisha taarifa zake na sasa kitambulisho chake kina majina sahihi.

Aidha, Mwanaharusi Moyo, mkazi wa Kaeza A amesema uandikishaji unaenda vizuri kutokana na idadi kubwa ya vituo, hivyo wananchi wanahudumiwa kwa haraka.

“Ninachoomba labda sasa Serikali iongeze elimu na hamasa ili wananchi wajitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao, na wananchi wajue kitambulisho hicho si kwa ajili ya kupiga kura pekee, bali pia kinaweza kutumika katika shughuli mbalimbali kama kuchukua mikopo na dhamana polisi,” amesema Moyo.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mwalimu Taji Mussa, mmoja wa waandikishaji, amepongeza mwamko wa wananchi na kuwataka kutumia siku za mapumziko ya mwisho wa wiki kufika vituoni kuboresha taarifa zao ili kuepuka msongamano unaoweza kutokea mwishoni mwa kazi hiyo.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji  Jacobs Mwambegele akiongea na wananchi  waliojitokeza kuboresha taarifa zao wakati alipotembelea kituo cha cha shule ya Msingi Kwakaeza A kilichopo Kata ya Mabawa katika Halmashauri ya Jiji la Tanga katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Picha na Rajabu Athumani

“Kusubiri dakika za mwisho kunaweza kusababisha foleni ndefu na wengine kushindwa kufanikisha uboreshaji wa taarifa zao,” amesema.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele, katika ziara yake ya kutembelea baadhi ya vituo vya uandikishaji katika Halmashauri ya Jiji la Tanga, amesema baadhi ya wananchi wanadai kubadilishiwa vitambulisho vyao bila sababu za msingi.

Hivyo, amesisitiza kuwa ni wale tu waliopoteza vitambulisho au wenye makosa kwenye taarifa zao ndio wanaopaswa kubadilishiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amewahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kuboresha taarifa zao, huku akiwakumbusha vijana wanaotarajia kutimiza umri wa miaka 18 ifikapo Oktoba mwaka huu, nao wajitokeze kujiandikisha ili waweze kushiriki katika uchaguzi.

Uboreshaji wa taarifa katika Mkoa wa Tanga umeanza katika halmashauri za Wilaya ya Lushoto, Kilindi, Muheza, Korogwe, Mji wa Korogwe, Mji wa Handeni na Jiji la Tanga.

Related Posts