Dar es Salaam. Jumuiya ya Ulaya (EU) imetoa ufadhili wa zaidi ya Sh17. 8 bilioni kwa asasi za kiraia 11 nchini Tanzania, kwa lengo la kukuza demokrasia kwa kujenga jamii yenye uwazi, haki, na ujumuishi zaidi, kwa kuimarisha sauti za wananchi na taasisi.
Ufadhili huo wa miaka mitatu uliotolewa kupitia Mpango wa Asasi za Kiraia na Mpango wa Fedha kwa Ukuaji, umezingatia maeneo muhimu kama utawala bora, uhuru wa vyombo vya habari, uwezeshaji wa vijana, na uwajibikaji wa kifedha wa umma.
Akizungumza wakati wa kutoa ruzuku hizo leo Februari 14, Mkuu wa EU Tanzania, Marc Stalmans amesema asasi za kiraia ni kiungo muhimu kwa jumuiya hiyo na katika jamii.
“Tunazungumzia vita, uhalifu wa kiuchumi, tunazungumzia kuibuka kwa watu wenye misimamo mikali, tunazungumza zaidi na zaidi kuhusu ugumu wa kuchapisha kile ulichonacho.
“Kwa hiyo ni muhimu kuweka mshikamano na watu wa Afrika na ni muhimu kwa azaki kuwa pamoja nasi, kwani zinakuza demokrasia na ni sauti ya wanajamii,” amesema.
Amesema wanatarajia kuona asasi za kiraia zikipigania utawala bora, usimamizi wa fedha, demokrasia na utawala wa sheria.
“Sisi Umoja wa Ulaya tunashiriki tunu za kimataifa ambazo ni utawala wa sheria, demokrasia, ustawi wa wanawake na vijana katika jamii.
“Tulipoamua kujipanga upya mwaka 2021 tuliweka mambo mawili, kwanza haki za binadamu na demokrasia na pili kuwa pamoja na Azaki na mashirika yasiyo ya kiserikali,” amesema.
Amezitaka Azaki zilizopewa ufadhili kutumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Balozi wa EU nchini Tanzania, Christine Grau amesema ruzuku hiyo inalenga kujenga ushirikiano unaotegemea uaminifu, matarajio ya pamoja na dhamira ya kutoa sauti kwa wale ambao mara nyingi husahaulika.
“Asasi za kiraia zenye nguvu ni nguzo muhimu zinahakikisha uwajibikaji, zinaboresha utawala wa kidemokrasia, na zinaimarisha jamii zetu,” amesema.
Akizungumzia ufadhili huo, Fausta Musokwa, Meneja wa Programu ya Kimataifa ya ufadhili wa vyombo vya habari (IMS Tanzania), amesema
“Sasa zaidi ya wakati wowote, uandishi wa habari bora ni muhimu sio tu kwa kupambana na hotuba za chuki na habari potofu, bali pia kwa kusaidia kujenga jamii yenye uwazi, uwajibikaji, na demokrasia nchini Tanzania,” amesema
Arafat Lesheve, kiongozi kijana kutoka mradi wa Vijana Plus ukiongozwa na Save the Children na Tanzania Bora Initiative, amesema watafaidika kwa kukuza sauti za vijana.
“Kupitia mpango huu, sisi vijana sio tu washauri; bali ni wabunifu wa suluhisho na waelimishaji wenzao. Kuwezesha mashirika yanayoongozwa na vijana ni sawa na kuwezesha mustakabali wetu,” amesema.
Mradi mwingine uliofadhiliwa ni wa utetezi wa haki za binadamu kupitia Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki na Chama cha Wanasheria wa Afrika (PALU), na Chama cha Wanasheria Wanawake wa Zanzibar (Zafela).
“Kutetea haki, kuimarisha haki na kupanua nafasi ya kiraia mpango huu unawawezesha wananchi, wataalamu wa sheria, na asasi za kiraia kusimamia utawala wa sheria na kuimarisha uwajibikaji nchini Tanzania,” amesema Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC.