Miili mitatu yatolewa ajali ya lori Kimara

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amethibitisha kutokea kwa ajali iliyohusisha lori lililohama njia na kuparamia kituo cha bodaboda kilichopo Kimara Stop Over usiku wa kuamkia leo Februari 14, 2025.

Lori hilo lilikuwa likitokea Morogoro kuelekea kuja Dar es Salaam ambapo katika ajali hiyo Chalamila amesema hadi saa 9:00 alfajiri miili mitatu iliyokuwa imekandamizwa na kontena la lori hilo imeshatolewa.

“Miili ya watu hawa inasemekana walikuwa madereva pikipiki,  pia tumefanikiwa kutoa pikipiki ambazo kwa idadi ni nyingi kuliko watu tuliowakuta kwa mantiki hiyo taarifa ya Polisi itaweka bayana,” amesema Chalamila.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, RPC Mtatiro Kitinkwi amesema kutokana na idadi ya pikipiki kuwa kubwa kuliko miili iliyokutwa, inawezekana wakati wa tukio watu walikimbia kujiokoa.

“Taarifa kwa kirefu tutaitoa tukishajua chanzo cha ajali hii kwa kuwa imetokea usiku na tumekuwa hapa kwa zaidi ya saa mbili,” amesema Kamanda Kitinkwi.

Aidha katika hatua nyingine Chalamila ametoa rai kwa watumiaji wa barabara kuwa makini na waangalifu kila mahali wanapokuwa barabarani.

Endelea kufuatilia mitandao ya Mwananchi kwa taarifa zaidi.

Related Posts