Serikali yasaini kandarasi ya Sh 350 bilioni ujenzi wa uwanja Dodoma

Serikali imesaini mkataba wa ujenzi wa uwanja wa mchezo wa mpira wa miguu jijini Dodoma na mkandarasi kampuni ya LimontaI Spa ya nchini Italia wenye thamani ya zaidi ya Sh350 bilioni.

Mradi huo utatekelezwa kwa miaka miwili kuanzia sasa, huku ukitarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji zaidi ya 32,000 ambao ni mradi wa pili wa ujenzi wa viwanja vipya vilivyotangazwa na Serikali.

Hayo yamejiri leo Februari 13,2025 jijini Dodoma wakati  Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi  akishuhudia utiaji saini wa mkataba huo

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema wakazi wa Dodoma walikuwa wakijiuliza juu ya uwanja huo huku michezo ya Afcon 2027 ikikaribia.

Profesa Kabudi amesema mradi huo ni kielelezo cha kuendelea kuimarisha sekta ya michezo nchini.

Kusainiwa kwa mkataba huo kunaondoa sintofahamu ya muda mrefu ya ujenzi wa uwanja Dodoma kutokana na kukwama kwa ufadhili wa Serikali ya Morocco ambapo kwa sasa mradi huo utafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.

Related Posts