Wadakwa wakitoa shahada za uzamili, PhD ndani ya siku tatu hotelini

Moshi/Nairobi. Polisi nchini Kenya wamewatia mbaroni watu wanne wakiwamo raia wawili wa kigeni, wakiwatuhumu kutoa shahada za uzamili (master’s degree) na Shahada ya Uzamivu (PhD) ya heshima wakiwa hotelini mjini Mombasa.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Februari 13, 2025 na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ya Kenya, saa 1:04 usiku kupitia ukurasa wake wa X zamani Twitter, imesema wanufaika wa shahada hizo walipewa mafunzo kwa siku tatu.

DCI amewataja waliokamatwa katika operesheni hiyo kuwa ni Dayis Bennett ambaye ni raia wa Marekani, Faraha Akab ambaye ni raia wa Pakistan na Wakenya wawili ambao wametajwa kuwa ni Ekra Ndung’u na Josephine Ndune.

Kulingana na taarifa hiyo, operesheni ya makachero kutoka ofisi ya DCI ililenga washukiwa ambao waliweka makao katika hoteli ya White Sands iliyopo kaunti ya Mombasa na wanufaika walipatiwa mafunzo kwa muda wa siku tatu.

Baadhi ya shahada zilizokamatwa katika operesheni hiyo ya makachero wa DCI ni shahada tatu za uzamili katika Utawala wa Biashara (Uongozi na Usimamizi) na PhD mbili za heshima katika uongozi (Phd in Leadership-Hon causa).

Tayari washukiwa wawili ambao hata hivyo hawakutajwa kwa majina, kati ya wanne waliokamatwa, wamefikishwa mbele ya mahakama ya Shanzu huko Mombasa wakituhumiwa kutoa shahada za vyuo vya nje bila kibali.

Kosa hilo ni kinyume cha kifungu cha 28(2) kikisomwa pamoja na kifungu cha 5 cha Sheria ya Vyuo Vikuu na walikana kutenda kosa hilo na walipewa dhamana kwa kuweka bondi ya Ksh400,000 ambazo ni sawa na Sh8.8 milioni kwa kila mmoja.

Hati za kusafiria za raia hao wa kigeni zilikabidhiwa mahakamani kama moja ya sharti la dhamana na kesi hiyo imepangwa kutajwa Februari 18, 2025 kwani endapo hawana mdhamini, basi waweke mahakamani fedha taslimu Ksh300,000 sawa na Sh6.6 milioni.

Kukamatwa kwa washukiwa hao kumekuja miezi miwili tu tangu Tume ya Vyuo Vikuu (CUE), itoe tamko Desemba 24, 2024 ikionya umma wa Wakenya kuhusu kuibuka kwa wimbi la utoaji wa shahada za heshima zisizotambuliwa na CUE.

Miongoni mwa waliopata shahada hizo ni baadhi ya wabunge huku CUE ikianzisha uchunguzi wa shahada hizo na kusisitiza kuwa hakuna chuo cha kigeni kinaruhusiwa kutoa shahada ya aina yoyote nchini Kenya bila kuwa na kibali.

“Wakenya wanafahamishwa kwamba utoaji wa hadhi za kitaaluma na taasisi ambazo hazijaidhinishwa ni ukiukaji wa moja kwa moja wa Sheria ya Vyuo Vikuu, sura 210 ambayo inakataza utoaji wa elimu ya chuo kikuu bila kibali,” ilieleza.

Kutokana na taarifa hiyo, mjadala mkali uliibuka nchini Kenya huku baadhi ya wananchi wakitaka wabunge waliopewa shahada hizo wawajibike na Chuo cha Northwestern Christian kilichotoa PhD bila kuwa na Ithibati kichukuliwe hatua.

Mijadala kama hiyo ya nchini Kenya, iliwahi kuibua hapa Tanzania, baada ya Watanzania wa kada mbalimbali, kutunukiwa shahada za udaktari wa heshima na vyuo ambavyo ilidaiwa havitambuliwi na Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU).

Kuliibuka madai kuwa baadhi ya waliopewa PhD hizo za heshima walikuwa wamezinunua kati ya Dola 2,000 hadi Dola 5,000 kutoka katika baadhi ya vyuo visivyo na ithibati hapa nchini na nchi vinapojitambulisha vinatoka.

Related Posts