Wadau washauri Afrika kutumia sera za Trump kama fursa

Arusha. Nchi za Afrika zimeshauriwa kutumia mabadiliko ya sera za kibiashara za Marekani kama fursa ya kipekee ya kukuza uchumi wake.

Rai hiyo imetolewa leo Februari 14, 2025 na wataalamu wa masuala ya kibiashara Afrika katika mjadala wa mtandao ulioandaliwa na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) uliohusisha wadau zaidi ya 300 kutoka Afrika na Marekani, wakiwemo wataalamu, watunga sera na wakuu wa biashara.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutishia kuongeza ushuru kwa Mexico na Canada huku akiweka ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa zote zinazoingizwa kutoka China.

Katika mjadala huo uliolenga kujadili njia za kubadili mabadiliko ya sera kuwa fursa halisi za kukuza uchumi wa Afrika, watalaamu hao wamesema nchi za Afrika zinahitaji kuweka mkakati madhubuti wa kuongeza thamani kwa bidhaa, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuwekeza katika sekta zenye thamani kubwa ili kuhakikisha biashara na Marekani inakuwa chachu ya maendeleo endelevu kwa bara hili.

Mjadala huo uliopewa jina la “Trump, Biashara na Afrika: Mabadiliko ya Sera kuwa Fursa”,  Mwenyekiti wa EABC, John Lual Akol amesema upo umuhimu wa Afrika kuwa na msimamo wa pamoja na kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi ili kuhakikisha kuwa mabadiliko katika sera za Marekani yanawezesha ukuaji wa kiuchumi wa bara zima.

“Afrika inahitaji kuwa na mikakati madhubuti ya kutumia mabadiliko haya kama fursa ya kuleta maendeleo endelevu na ya pamoja,” amesema Akol.

“Hata hivyo, hatuwezi kufanikiwa bila kuwa na msimamo wa pamoja lakini pia kushirikiana kwa sekta binafsi na za serikali ili kufanikisha hili,” amesema Akol.

Naye John Thomas kutoka Nestpoint Associates ameelezea kuwa utawala mpya wa Marekani unatumia mbinu ya kibiashara inayolenga kujenga mikataba ya biashara na nchi mbalimbali.

 Ameongeza kuwa Afrika ina nafasi kubwa ya kunufaika na ongezeko la ushuru wa Marekani kwa bidhaa za China, hasa kwa kujitambulisha kama kitovu mbadala cha mnyororo wa ugavi.

“Hata hivyo ili kupata nafasi hiyo ni muhimu kujikita zaidi katika sekta ya teknolojia na hasa maendeleo ya vituo vya data, kama maeneo ya fursa kwa Afrika,” amesema.

Akizungumzia mabadiliko makubwa katika biashara ya kimataifa, Mwenyekiti wa Chama cha Sekta Binafsi Kenya (KEPSA), Jas Bedi amesema dunia inaelekea katika mwelekeo wa uendelezaji wa bidhaa na huduma kwa kanda na maeneo, badala ya kutegemea utandawazi wa kimataifa.

Amesema kwa sasa Sheria ya Ukuaji na Fursa ya Afrika (AGOA) inakaribia kumalizika, hivyo Afrika inapaswa kufikiria mbinu mpya za kuhakikisha inafaidika na biashara na Marekani.

Ameongeza kuwa sasa Afrika inachangia asilimia 3.5 tu ya uchumi wa dunia wenye thamani ya dola za Marekani 100 trilioni na inachangia asilimia mbili ya uagizaji wa bidhaa za Marekani. Hii ina maana kwamba Afrika haina ushindani mkubwa kwa Marekani, lakini bado haijatumiwa ipasavyo kama mshirika wa kibiashara,” amesema Bedi.

“Bara hili lina idadi kubwa ya watu vijana, ni muhimu kutumia rasilimali hii ili kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa kuongeza thamani ya bidhaa na kuimarisha ushirikiano wa kanda na bara, nadhani hii ndio itakuwa manufaa makubwa kwetu Afrika,” amesema.

Akizungumzia umuhimu wa kuboresha usafirishaji wa bidhaa kati ya Afrika na Marekani, mtaalamu wa Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi Afrika, Dk Valencia de la Vega amesema upo umuhimu wa kutumia teknolojia ya ‘AI’ ili kuongeza ufanisi wa mnyororo wa ugavi.

Sekta za nishati mbadala, uzalishaji wa betri na utafiti wa kuongeza thamani katika viwanda, Dk Vega amesema ndiyo maeneo yenye fursa kubwa za biashara nchini humo.

Naibu Mwenyekiti wa EABC, Simon Kaheru amesema Afrika inapaswa kuweka mikakati ya kibiashara badala ya kutegemea msaada wa kimataifa. “Afrika inahitaji kuwa na mipango madhubuti ya kibiashara na sio kutegemea misaada ya nje,” amesema Kaheru.

Related Posts