Buidhaa hizi zapaisha mfumuko wa bei Zanzibar

Unguja. Mfumko wa bei kwa Januari 2025  Zanzibar umeongezeka na kufikia asilimia 5.27 kutoka asilimia 4.9 iliyorekodiwa Desemba 2024, huku bidhaa za mchele na ndizi zikichangia kwa kiwango kikubwa.

Bidhaa zilizosababisha kuongezeka kwa mfumuko wa bei ni pamoja na mchele wa mapembe kwa asilimia 1.5, mchele wa Mbeya asilimia 4.4, mchele wa Jasmin asilimia 0.8, unga wa ngano asilimia 2.9, ndizi za mtwike asilimia 4.5, na mafuta ya kupikia OKI asilimia 3.9.

Wakati mfumuko ukifikia hatua hiyo, lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba hauzidi asilimia tano ili kuleta uhimilivu kwa wananchi na kuwasaidia kumudu gharama za maisha bila changamoto yoyote.

Mtakwimu kutoka Divisheni ya Takwimu za Bei, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Salma Saleh Ali, amesema kwa ujumla faharisi za bei zimeongezeka na kufikia asilimia 114.86 kwa Januari 2025 ikilinganishwa na asilimia 109.11 iliyorekodiwa Januari 2024.

Ametoa kauli hiyo wakati wa kutoa taarifa za mfumuko wa bei Februari 15, 2025, ambapo amesema kuwa kundi la vyakula na vinywaji visivyo na kileo kwa Januari 2025, limefikia asilimia 7.21 ikilinganishwa na asilimia 7.9 iliyorekodiwa Desemba 2024.

“Kinachochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei ni kutokana na bidhaa zilivyoingizwa katika kipindi hiki,” amesema.

Amesema kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za chakula wa mwaka unaoishia Januari 2025, umepungua na kufikia asilimia 6.64 ikilinganishwa na asilimia 8.11 iliyorekodiwa Desemba 2024.

Amesema faharisi za bei za bidhaa za chakula kwa Januari 2025 zimeongezeka na kufikia asilimia 122.73 kutoka asilimia 116.02 iliyorekodiwa Desemba 2024.

Kwa upande wa bei ya bidhaa zisizo za chakula kwa mwaka, umepungua na kufikia asilimia 4.22 kwa Januari 2025 ikilinganishwa na asilimia 2.51 iliyorekodiwa Desemba 2024.

Amesema kuwa faharisi za bei za bidhaa zisizo za chakula zimeongezeka na kufikia asilimia 108.81 Januari 2025 ikilinganishwa na asilimia 104.40 iliyorekodiwa Desemba 2024.

Hata hivyo, Meneja Msaidizi Uchumi na Takwimu Benki Kuu (BoT) Tawi la Zanzibar, Shamy Chamicha, amesema hali ya mfumuko wa bei bado ipo vizuri kwa upande wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kwani haujawa na athari katika kiwango kikubwa.

“Hivyo, kuna kila sababu kwa wananchi kuendelea kufanya shughuli zao za uzalishaji mali ili kupata faida na kujikwamua kiuchumi,” amesema.

Related Posts