Na Humphrey Shao, Michuzi Tv
MKUU wa Wilaya ya Ilala,Edward Mpogolo amesema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inaingia katika majiji bora kwa usafi barani Afrika.
Amesema nia, sababu na uwezo wanao kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa usafi hapa nchini na Bara la Afrika.
Mpogolo ameyasema hayo Dar es Salaam, leo alipoongozs wananchi na wadau katika kampeni ya usafi wa kila jumanosi kuanzia eneo la Kamata Kata ya Gerezani, kupitia Barabara ya Sokoine, Magogoni, Ocean Road, Barack Obama na Seview Kata ya Kuvukoni.
Amesema, usafi utafanyika usiku na mchana na dhamira ni kulifanta Jiji la Dar es Salaam kuwa safi na kuenzi jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika matumizi ya nishati safi na usimamizi wa mazingira.
“Nia ya usafi tunayo, uwezo tunao, nguvu tunazo na ari tunayo ya kulifanya Jiji la Dar es Salaam kuwa safi. Tunataka kulifanya kuwa moja ya majiji safi Afrika,”amesema Mpogolo.
Amesema tayari wadau wamenza kupongeza hali ya usafi iliyopo katika jiji hilo tangu alipotangaza kampeni ya usafi wa kika siku, kila Jumamosi na kila Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi.
Ameeleza ili kufanikisha azima hiyo wakandarasi wa usafi kuhakikisha wananunua na kutumia vifaa bora vya usafi.
“Tuna kasi kubwa ya kufanya Dar es Salaam iwe safi, na tunapaswa kuwa mfano kwa miji mingine. Uwezo tunao, nia tunayo, na lazima tuthibitishe hilo kwa vitendo,”amesema Mpogolo.
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya,amesema kuwa usafi ni utamaduni na tabia inayojengeka hivyo watahakikisha Jiji la Dar es Salaam lina kuwa safi na nadhifu wakati wote.