Jinsi Raila alivyoukosa uenyekiti Umoja wa Afrika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahmoud Youssouf amemshinda Raila Odinga wa Kenya kwenye kinyang’anyiro cha mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC).

Mchuano huo uliokwenda hadi mzunguko wa saba Youssouf ameshinda kwa kupata kura 33, baada ya Raila kuondoa jina lake.

Raila alilazimika kuondoa jina lake kwenye mzunguko wa sita, wakati huo Youssouf alikuwa akiongoza kwa kupata kura 26 na Raila kura 22.

Utaratibu wa mshindi kwenye uchaguzi anatakiwa apate theluthi mbili ya kura ili ashinde uchaguzi huo.

AU ina nchi wanachama  55 wenye haki ya kupiga kura, hata hivyo kuna mataifa sita ya Burkina Faso, Gabon, Guinea, Mali, Niger  na  Sudan ambayo uanachama wao ulisitishwa kutokana na mizozo kwenye nchi zao.

Hata hivyo, Raila baada ya kupata kura 22 kwenye mzunguko wa sita na Youssouf akiwa anaongoza kwa kura 26, aliamua kujitoa na kumwacha Youssouf kujaribu duru ya saba na ya mwisho kwa ajili ya kupata wingi wa theluthi mbili ili kushinda kiti hicho.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mahmoud Youssouf aliyeshinda nafasi ya uenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC).

Mgombea mwingine wa tatu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Richard James Randriamandrato aliondolewa kwenye kinyang’anyiro baada ya duru ya tatu.

Mzunguko wa kwanza na kura zikiwa kwenye mabano Raila (20), Youssouf (19), Richard (10). Mzunguko wa pili Raila (22), Youssouf (18), Richard (7), mzunguko wa tatu Raila (20), Youssouf (23), Richard (5), mzunguko wa nne Raila (21) Youssouf (25), Richard (0).

Mzunguko wa tano Raila (21) Youssouf (26), Richard (0) na mzunguko wa sita Raila (22) Youssouf (26), Richard (0).

Viongozi wa zamani wa nafasi hiyo  wamekuwa wakitoka maeneo ya magharibi, kati, na kusini mwa Umoja wa Afrika.

Hata hivyo, Baraza la Utendaji la AU liliweka wazi haki ya eneo la Afrika Mashariki kutoa kiongozi wa kiti hicho na ndipo akateuliwa Raila Odinga wa Kenya, huku eneo la Afrika Kaskazini wakipewa nafasi ya naibu mwenyekiti.

Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) ina nchi wanachama 16 ambazo ni  Angola, Botswana, Comoros, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Seychelles, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ina nchi wanachama nane ambazo ni Burundi, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.

Raila alikuwa akiungwa mkono na EAC, lakini sekretarieti ya Sadc iliandika barua kwa wanachama wake wakitaka mgombea wa Madagascar, Richard James Randriamandrato aungwe mkono.

Wasifu wa mwenyekiti mpya

Mohamoud Ali Youssouf alizaliwa Septemba 2, 1965 huko Djibouti na amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti tangu mwaka 2005.

Ali Youssouf alisoma isimu, biashara, na usimamizi huko Lyon, Ufaransa, Liverpool, Uingereza, na Laval, Ufaransa kabla ya kuandika thesis yake katika Chuo Kikuu cha Bure cha Brussels katika miaka ya 1990. Kati ya mwaka 1992 na 1997, akiwa bado mwanafunzi, Ali Youssouf alikuwa mkuu wa masuala ya Kiarabu ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Djibouti.

Mwaka 1997 aliteuliwa kuwa Balozi wa Misri hadi mwaka 2001 aliporudi Djibouti na kuteuliwa kuwa naibu waziri wa ushirikiano wa kimataifa.

Aliendelea kushikilia wadhifa huu hadi Mei22,  2005 alipopewa jukumu la kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Tangu wakati huo ameendelea kushikilia wadhifa huu licha ya mabadiliko matatu ya rais. Yeye ni mwanasiasa huru na anachukuliwa kuwa na mtazamo chanya kuhusu mustakabali wa Djibouti.

Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao

Related Posts