Lissu: Nimejiandaa kushinikiza mabadiliko | Mwananchi

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema haofii kifo katika mapambano ya kudai haki kwenye mfumo wa uchaguzi ili kuondokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo wagombea wa upinzani kuenguliwa pasipo sababu za msingi.

Kwa kauli yake Lissu amesema: “Kama ni kufa kwani kuna atakayeishi milele hapa, kuna ambaye hatakufa hapa? Mimi nipo tayari kufa, nilishachungulia huko, nikarudi tunaendelea.”

Lissu aliyewahi kuwa Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani alinusurika kifo Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi 30 na watu wasiojulikana katika makazi yake Area D, jijini Dodoma akitoka kuhudhuria kikao cha Bunge.

Baada ya kushambuliwa kwa risasi zilizomjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake, Lissu alipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, kisha Nairobi nchini Kenya kwa matibabu zaidi kabla ya kuhamishiwa Ubelgiji alikomalizia matibabu yake.

Lissu ambaye ni mbunge wa zamani wa Singida Mashariki ametoa msimamo huo leo Februari 15, 2025 alipozungumza na wananchi wa Manyoni, mkoani Singida katika mkutano wa hadhara aliposimama kuwasilimia akielekea wilayani Ikungi, ambako ni kijijini kwao.

Mwanasiasa huyo machachari amesema katika mapambano hayo ya kudai haki katika mfumo wa uchaguzi amejiandaa kwa lolote ikiwemo kufungwa.

“Kama hawataki kufanya mabadiliko kwa hiari, basi tunakwenda kwenye kushurutishana, kama ni kufungwa mimi nimejiandaa. Tutapata mageuzi kwa shuruti na maumivu, hiari hawaitaki tutashurutishana,” amesema Lissu kisha akanyamaza kwa sekunde kadhaa na kuwasikiliza wananchi aliokuwa akiwahutubia ambao walisikika wakisema tupo pamoja.

“Kaulimbiu yetu bila mabadiliko, hakuna uchaguzi, tujiandae kuzuia uchaguzi kama hawataki kuleta mageuzi. Nitaongoza mfumo wa kudai mapambano haya ya kushurutisha ili tupate mfumo mzuri wa uchaguzi,” amesema.

Februari 12, 2025 akiwahutubia Watanzania katika ofisi za makao ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam Lissu alitangaza chama hicho kuanzisha vuguvugu la mabadiliko ya kimfumo ya uchaguzi kuekelea Uchaguzi Mkuu 2025 likiwa na kaulimbiu ya No reforms, No elections (hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi).

Lengo la vuguvugu hilo, ambalo kampeni yake itaanza mwezi ujao (Machi) katika mikoa ya kusini ni kuunganisha nguvu za Watanzania katika kudai mabadiliko kwenye mfumo wa uchaguzi.

Kwa mujibu wa Lissu, endapo chama hicho, kitakwenda kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, basi hakitaambulia chochote kwa madai ya kuwa mifumo ya chaguzi siyo rafiki.

Amesema Chadema kitakwenda kupata maumivu pasipo kuambulia kitu, huku akirejea matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa Novemba 27, 2024 ambayo Chadema kiliambulia viti vichache katika ngazi ya vijiji, jambo ambalo Lissu amedai halikuwa na uhalisia.

Lissu amesema hana imani iwapo uchaguzi mkuu utakuwa huru na haki, endapo mifumo ya mchakato huo haitarekebishwa.

Amesema anakwenda Ikungi na Mahambe mkoani Singida kupata baraka za wazee katika jukumu lake jipya la uenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

“Nakwenda nyumbani kwetu kuwaomba wazee waweke mikono yao ya baraka kwenye hii kazi nitakayoenda kuianza. Nataka wazee waweke mikono na kusema sasa mtoto wetu nenda kafanye kazi, tukishamaliza tutaingia kazini, tutaitembea nchi yote kuzungumzia habari za chaguzi za Tanzania.

“Jiandaeni kila mmoja wetu aweke mkono wa baraka na afanye kwa sehemu yake, tujitolee hii kazi ni yetu sote,” amesema.

Akiwa wilayani Ikungi akiambatana na viongozi mbalimbali wa Chadema Kanda ya Kati, Lissu na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila walitawazwa kama mashujaa wa kabila la Kinyaturu.

Shughuli hiyo ilikwenda sambamba na kupewa au kutumwa majukumu ya kupambana ili kupata mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi, kupinga vitendo vya uporaji wa rasilimali za nchi kinyume cha sheria za nchi.

Lissu na Mahinyila walivishwa vazi asili, kisha kupewa ngao na mkuki ikiwa ishara ya mashujaa wa kabila hilo.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Devota Minja amesema kanda hiyo itamuunga mkono Lissu kwa kila hatua kuhakikisha ajenda za chama hicho zinatekelezeka kwa vitendo

“Tumekusikia ukisema kama hakuna tume huru, hakuna uchaguzi, tumeilewa vizuri, tukiwa wajumbe wa kamati kuu tulikubaliana kwamba hatupo tayari kwenda katika chaguzi za maumivu, hatupo tayari kwenda katika chaguzi zisizo na haki au kuwa wasindikizaji wa chaguzi,” amesema.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), Suzan Lyimo amesema anamfahamu Lissu kama kiongozi mpambanaji na anayepigania haki muda wote.

“Tumepata kiongozi atakayeenda kuleta mabadiliko makubwa katika nchi yetu. Tunaposema no reforms, no elections tunamaanisha kwamba lazima mifumo ibadilike,” amesema.

Related Posts