Marufuku shughuli za kibinadamu mapango ya Amboni

Tanga. Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Japhari Kubecha amepiga marufuku shughuli zote za kibinadamu zinazofanyika katika Hifadhi ya Mapango ya Amboni, kama vile kukata miti, kuchimba mchanga, kwani kufanya hivyo kunaweza kuharibu uhalisia wa eneo hilo.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye hafla ya kutangaza vivutio vya utalii kwa Mkoa wa Tanga iliyofanyika katika mapango hayo na kupewa jina la Diko la Amboni, mkuu huyo wa wilaya amesema anazo taarifa kuwa wapo wananchi wanaoingia kwenye eneo hilo na kukata miti, kuni na kuchimba mchanga.

Amesema Serikali haiwezi kukubali kitendo hicho na amepiga marufuku wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kuacha kabisa vitendo hivyo, na kuwa ambao watabainika hatua kali za kisheria dhidi yao zitachukuliwa.

Kubecha anasema Mapango ya Amboni yamekuwa na faida kwa Wilaya ya Tanga, kwani watu kutoka maeneo tofauti wanafika hapo kwa ajili ya kutalii na Serikali inaingiza mapato, huku wananchi na wao wakipata faida kwa kuuza bidhaa na vyakula kwa wageni.

“Eneo la Amboni linatunufaisha kwa mambo mengi sana… Tuendelee kusisitiza umuhimu wa uhifadhi na kulinda misitu. Limekuwa na manufaa makubwa sababu linakutanisha watu, lakini wananchi wanakwenda hapo na wenzi wao kuburudika,” amesema Kubecha.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mariam Kobelo kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA), amesema wameamua kuanza kutangaza vivutio vya asili kama Mapango ya Amboni, ambavyo inaonekana kwamba wananchi wanavisahau ingawa vipo kwenye maeneo yao.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Japhari Kubecha akiongea na wananchi kwenye hafla ya uzinduzi wa kutangaza vivutio vya utalii kwenye Mapango ya Amboni yaliyopewa jina la Diko la Amboni. Picha na Raisa Said

Amesema Mapango ya Amboni hutembelewa na Watanzania 13,000 kwa mwaka, idadi ambayo anasema ni ndogo, na lengo ni kufikia zaidi ya 20,000, ukiacha watalii wa kigeni, ambao wao malipo yao ni tofauti na Watanzania.

Kamishna Mariam anasema wamefanya maboresho makubwa ndani ya mapango hayo, ikiwemo kuweka taa na njia ambazo mgeni anaweza kupita muda wote, kwani awali zilikuwa zikitumika tochi, ambazo uwezo wake ulikuwa mdogo kwa kushindwa kuhimili muda mrefu.

Msanii Zena Mohammed, maarufu kama Shilole, amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii kwa kushirikiana na mamlaka kama Ngorongoro, kwani zimekuwa na faida kwa nchi na kuongeza kipato kwa nyanja mbalimbali.

Anasema ameshuhudia mabadiliko makubwa ndani ya hifadhi ya Mapango ya Amboni na yanavutia zaidi kuliko awali, kwani alishawahi kufika hapo zamani na hakuona maboresho kama yaliyofanyika sasa hivi.

Mkazi wa Rombo, mkoani Kilimanjaro, Katherine Njau, amesema amefurahishwa na mazingira ya eneo la Amboni, akisema ni tulivu na kuna uhalisia wa asili yake.

Related Posts