KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua baada ya mchezo wao wa Ligi Kuu uliokuwa upigwe leo dhidi ya Dodoma Jiji kuahirishwa, lakini mapema bilionea na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Mohammed ‘MO’ Dewji amechochea moto wa kuzoa pointi kwa timu hiyo.
Kabla ya mechi za jana, Simba ilikuwa kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 47, moja zaidi na ilizokuwa nazo Yanga iliyokuwa uwanjani kucheza na KMC, huku ikielezwa Mo Dewji alikutana na mstaa wa timu hiyo saa chache kabla ya mchezo uliopita dhidi ya Prisons uliowarudisha kileleni.
Kwa mujibu wa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo ni kwamba bilionea huyo wa Simba waliwatia hasira akiwataka kutoendelea kudondosha pointi kama ilivyofanya kwa Fountain Gate na ndio maana waliingia kwa morali na kuifyatua Prisons kwa mabao 3-0 na kuing’oa Yanga iliyokuwa kileleni awali.
Mastaa hao walisema agizo la Mo Dewji halijaishia kwa mechi hiyo tu ya maafande, bali zote nyingine zilizosalia msimu huu ili kuhakikisha Simba inarejesha ubingwa iliyoupoteza misimu mitatu iliyopita kwa watani wao wa Yanga.
Taarifa za ndani ya kambi ya Simba, zinasema bilionea huyo alianza kwa kuwapongeza kwa juhudi za uwanjani, lakini akawakumbusha juu ya kutokudharau mechi kama ilivyotokea Manyara ilipotoka sare ya 1-1 na Fountain Gate na kuwasihi mastaa hao wazibebe mechi zote kwa uzito.
“Bosi mwenyewe ameahidi kwamba bonasi zitakuwa zinatoka kwa wakati, lakini wachezaji waendelee kushinda na amewakumbusha kuhusu wapinzani wao Yanga na Azam wana nafasi za kuwa bingwa.
“Hivyo kama watarudi tena juu ya msimamo wasibweteke wajue wana jukumu la kuongeza ushindi, ili kujiongezea nafasi ya kwenda kuwa bingwa. Amewaambia pia wachezaji wapendane wacheze kwa kuipigania timu na sio kila mmoja kujipambania kirekodi,” kilisema chanzo hicho kutoka Simba.
Kikao hicho ni kama kilikwenda kuwasha gari la mastaa hao, kwani walikwenda kuwachakaza Wajeda wa Mbeya mabao 3-0 na baada ya kuahirishwa kwa mechi dhidi ya Dodoma, kikosi hicho sasa kinajiandaa kuifuata Namungo itakayoumana nao Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi.
Simba chini ya kocha Fadlu Davids imecheza mechi 18 na kushinda 15, ikitoka sare mbili na kupoteza moja, huku ikifunga mabao 38 na yenye kuruhusu sita tu, ikiwa ndio iliyofungwa idadi ndogo hadi sasa.