Hatimaye Pamba Jiji imeingia kwenye nafasi 10 za juu katika Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union huku ikijihakikishia mamilioni ya bonasi.
Mchezo huo wa raundi ya 19, umechezwa leo Jumamosi Februari 15, 2025 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Alama tatu ilizopata Pamba Jiji katika mchezo wa leo na kufikisha 21, zimeipaisha kutoka nafasi ya 13 hadi ya 8 sawa na Namungo na Fountain Gate lakini zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, huku Mashujaa ikifuata nafasi ya 11 na alama zake 20.
Pamba Jiji ilimaliza duru la kwanza ikiwa inakamata nafasi ya 15 baada ya kucheza mechi 15 lakini duru la pili imefanikiwa kushinda mechi tatu mfululizo na hatimaye kutinga kumi bora kwa mara ya kwanza.
Katika mchezo wa leo ambao umeanza kwa kasi ya chini bila kushuhudia mashambulizi yoyote ya hatari huku timu hizo kila moja ikimsoma mwenzake, mambo yalibadilika ghafla kuanzia dakika ya 18 baada ya Pamba Jiji kugeuza kibao na kupata bao la kwanza.
Bao hilo la kwanza Pamba Jiji imelipata kupitia kwa John Nakibinge raia wa Uganda aliyefumua shuti kali kutoka nje ya 18 na kujaa wavuni. Nakibinge amefunga bao hilo katika mchezo huo ambao ni wa kwanza kwake tangu atoke kuuguza majeraha ya muda mrefu.
Kiungo kutoka Guinea, Abdoulaye Yonta Camara anayecheza hapo kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, akaifungia Pamba Jiji bao la pili dakika ya 21 baada ya kupokea krosi kutoka kwa Mathew Tegis na kuudonoa mpira uliomshinda kipa.
Ushindi huo ni watatu mfululizo kwa Pamba Jiji baada ya dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15 mwaka huu, ambapo imezifunga Dodoma Jiji (1-0), Azam FC (1-0) na Coastal Union (2-0).
Pia ni ushindi wa tatu kwa Pamba Jiji katika uwanja wa CCM Kirumba msimu huu baada ya kuzichapa KenGold (1-0) na Azam FC (1-0).
Wana TP Lindanda wamelipa kisasi kwa Wana Mangushi kwani mchezo wa kwanza uliopigwa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Coastal Union ilishinda kwa mabao 2-0.
Kutokana na ushindi huo, wachezaji wa Pamba Jiji wamejihakikishia bonasi ya Sh10 milioni kutoka kwa uongozi kwani utaratibu uliowekwa katika duru la pili ni kwamba endapo timu itashinda inapata Sh10 milioni, huku mfungaji wa bao akipata Sh250,000, mtoa pasi ya bao (Sh100,000) na kipa akipata cleensheet anapewa Sh100,000.
Baada ya kichapo cha leo, Coastal Union inabaki nafasi ya sita na alama zake 22 ambapo imecheza michezo 19 na kushinda tano, sare saba na kupoteza saba huku ikifunga mabao 18 kuruhusu 20.
Kichapo hicho ni cha tatu kwa kocha Juma Mwambusi wa Coastal Union tangu alipokabidhiwa mikoba Oktoba 23, 2024 ambapo alifungwa pia na Yanga (1-0) na Fountain Gate (3-2), huku ukiwa ni mchezo wake wa 12 wa Ligi Kuu.
Matokeo ya Coastal Union chini ya Mwambusi ni Mashujaa (0-0), JKT Tanzania (2-1), KMC (1-1), Tabora United (1-1), Fountain Gate (2-3), Tanzania Prisons (2-1), Ken Gold (1-1), Singida Black Stars (0-0), Kagera Sugar (1-0), Yanga (0-1), Dodoma Jiji (2-0) na Pamba Jiji (2-0).