Dar es Salaam. “Nilimfahamu Mkama Sharp mwaka 1984 nikimuona stendi ya daladala ya Sabasaba (sasa Msimbazi A) nikiwa nasoma Chuo cha Biashara Kisutu. Pamoja na wenzangu tulipotoka shule tulikuwa tukisema huyu askari ni mkorofi.”
Ndivyo anavyoanza simulizi, Arafa Hamis aliyekuwa mke wa Mkama Sharp, ambaye Desemba 11, 2024 Gazeti la Mwananchi liliandika kuhusu historia yake. Alikuwa askari polisi maarufu jijini Dar es Salaam miaka ya 1980 hadi 2000.
Umaarufu wake haukuwa kwenye utekelezaji wa majukumu yake pekee, bali hata kwa mwonekano, ubunifu na uchapakazi wake.

Mkama Sharp aliyeshika bunduki akiwa na askari wengine wakiwa wanajiandaa kwa ajili ya lindo.
Solole Mkama Rugeje ndilo jina lake kwa mujibu wa Arafa, ambaye katika simulizi anaeleza Februari 1985 akiwa na mama yake mzazi Magomeni, Mkama Sharp alimuona akampenda.
“Mkama baada ya kuniona alimwambia mtu ambaye nimemsahau, nimemuona binti amepita hapa namuhitaji. Mtu huyo alikuja kwetu akawaeleza wazazi wangu,” anasema Arafa katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika Februari 5, 2025 nyumbani kwake Chamazi, wilayani Temeke.
Anasema Mkama Sharp alikwenda kwa ndugu zake wa ukoo wa Mahendeka waliokuwa wakiishi Mtaa wa Congo, Kariakoo jirani na kwao Arafa.

Mkama Sharp (wa pili kulia) akiwa na askari wengine kwenye mafunzo.
“Kwa kina Mahendeka walisema binti anayemuhitaji ni Muislamu wakati yeye ni Mkristo na familia ya mzee Hamis wasingekubali mtoto wao abadili dini wala kufunga ndoa mseto.
“Kwa kuwa bwana yule alikuwa ameshanipenda alisema kuhusu dini si sababu ya kutonioa yupo tayari kubadili kwa kuwa alishapita kwenye mikono ya Waislamu akiwa Tabora kwa baba yake mdogo,” anasimulia.
Anaeleza Mkama Sharp alibadili dini akaitwa Ramadhani. Walipofunga ndoa mwaka 1985 anasema alikuwa na miaka 20 akiwa amemaliza mafunzo ya katibu mahsusi.
“Kipindi hicho nilishakataa wanaume wawili, huyu alikuwa wa tatu. Baba mkubwa alisema wamechoka kusikiliza misimamo yangu, hivyo nitake nisitake nitaolewa na Mkama Sharp,” anasema.
Anasema hakuwahi kuwa na urafiki na Mkama, bali kwa amri ya wazazi alitii na kukubali kuolewa.

Mkama Sharp na mkewe mkewe, Arafa Hamis pamoja na ndugu wengine siku ya ndoa yao iliyofungwa jijini Dar es Salaam mwaka 1985.
Anasema waliishi Mtaa wa Kibambwe, Kariakoo wilayani Ilala na hata Mkama alipohamishwa vituo vya kazi hawakuwahi kuhama hadi pake alipohamishiwa Oysterbay.
Anasema hakuwahi kusikia Mkama amegombana au kukwaruzana na mtu.
Maisha mengine ya Mkama Sharp
Anasema Mkama Sharp hakuwahi kwenda msikitini hata wakati wa mfungo hakufanya hivyo kwa sababu hakuzoea kukaa muda mrefu bila kula.
“Anaweza kufunga ikifika saa nane mchana anasema mke wangu nasikia vitu vinapiga kelele tumboni nisongee ugali kidogo lakini usiseme sijafunga,” anasema.
Japokuwa hakuweza kufunga, anasema alijitoa kulisha watu kipindi cha mfungo na wengine aliwaalika nyumbani kufuturu.

Mkama Sharp mwenye shati la maua akiwa kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo kwenye Muziki wa Msondo Ngoma.
Kwa mujibu wa Arafa, Mukama Sharp alichukiwa na wauza gongo, bangi na vibaka aliowakamata mara kwa mara, ambao nao anasema ilifika hatua walikuwa walicheka naye wakitambua kuwa anatekeleza majukumu ya kazi yake.
Katika ndoa yao anasema walipata watoto wanne na kwamba, Mkama alikuwa na wengine wawili wa awali, hivyo walikuwa na watoto sita, wa kike wanne na wa kiume wawili.
Licha ya kazi ngumu aliyokuwa akifanya, anasema Mkama Sharp alikuwa karibu na familia, akiwapatia kila walichohitaji.
“Mume wangu nilimsifu kwa kukumbuka familia, anaweza kwenda huko akarudi akasema mke wangu tutoke, tunakwenda muziki. Hakuna starehe niliyoitaka nikaikosa,” anasema.
Anasema alipenda apendeze, hivyo chochote alichoona kitamfaa alimpelekea zawadi na kuna wakati alikuwa akimpeleka saluni.
“Alikuwa akiona mtu amesuka akapenda, alimsimamisha na kuuliza alikosuka, kisha anatuma mtu anifuate nyumbani kisha ananipeleka alikoelekezwa,” anasema.

Mkama Sharp na mkewe mkewe, Arafa Hamis pamoja na ndugu wengine siku ya ndoa yao iliyofungwa jijini Dar es Salaam mwaka 1985.
Kuna wakati anaeleza alikuwa akiwafuata wasusi wa Kimasai Kinondoni ambao walikuwa wakienda kumsuka nyumbani kwao Oysterbay.
Anasema Mkama Sharp ni mzaliwa wa Musoma mkoani Mara na kabila lake ni Mjita.
Katika familia yao anasema wamezaliwa 15, watoto watano kwa mama mmoja na wengine 10 kwa mwingine.

Mkama Sharp akiwa amekaa nje ya kilichokuwa Kituo Kidogo cha Polisi (Police Post) cha Jangwani kilichokuwa kinaangaliana na Uwanja wa Kaunda (Yanga).
Anasema Mkama kwa mama yake walizaliwa 10, yeye akiwa pacha katika uzao wa sita. Yeye alikuwa mdogo kwa maana ya Doto.
Akiwa askari pekee katika familia yake, alijiunga na Jeshi la Polisi mkoani Tabora akiwa kwa baba yake mdogo aliyekuwa dakatri katika hospitali ya mkoa huo.
Utendaji kazi, jina la Sharp
Kwa mujibu wa Arafa, mumewe aliitwa Mkama Sharp kutokana na utendaji wake wa kazi wa haraka.
“Askari wenzake walikuwa wanamzungumzia kwa vitendo vyake, kila anapoona jambo fulani alikuwa anachukua hatua papo hapo wakasema huyu askari yupo ‘sharp’ sana,” anasema.
Anaeleza kwa ufahamu wake hapo ndipo Sharp likaongezwa kwenye jina lake la Mkama akaanza kuitwa Mkama Sharp.
Anasema Mkama Sharp alifanya kazi vituo vinne na alipokuwa akihamishwa alimtambulisha kwa askari wenzake. Anataja vituo hivyo kuwa Msimbazi, Brash, Keko na Oysterbay.
“Katika vituo vyote alivyohamishiwa alinialika nipajue anapofanyia kazi. Nakumbuka alipohamishiwa Keko alinikaribisha na zawadi ya kitenge, akanitambulisha kwa wenzake,” anasema.
Kutokana na utendaji wake anasema alihamishwa vituo na kwamba, alikuwa akisema atamkamata mhalifu alifanya hivyo, kisha alipita naye mtaani ili jamii imuone, yeye akitembea kwa madaha kwa kutekeleza wajibu huo.

Mkama Sharp akitoa heshima mbele ya viongozi siku ya mahafali baada ya kuhitimu mafunzo aliyohudhuria katika Chuo cha Polisi Kurasini, jijini Dar es Salaam mwaka 2006.
Anasema alikuwa akitembea kwa kujitanua akiwa na bastola kiunoni, akiwa na kirungu mkononi, redio call na filimbi, watu wakipiga kofi wakiita Mkama Sharp.
“Majigambo alikuwa akifanya akiwa peke yake, nikiwa naye ilikuwa ni heshima, wakati huo amevaa nguo za nyumbani hayupo kazini,” anasema.
Anasema Mkama pia alikuwa anakwenda kwenye mikutano na misafari ya viongozi.
“Ikitokea matukio ya aina hiyo alikuwa ananiambia leo nitakuwa na kazi ngumu maana kuna ugeni unaingia kwa hiyo nitakuwa sana barabarani,” anasimulia.
Anasema alikuwa akifika kwenye vituo vya daladala anapanga makundi ya wajawazito, wenye watoto na wazee kuwa mstari wa mbele halafu wengine watafuata.
“Alifikia uamuzi huo baada ya kuona mtu mmoja kabla gari halijasimama alidandia akaanguka, bahati mbaya lilimpitia miguuni na kumsababishia ulemavu,” anasema.
Anasema ili kuafuata utaratibu kabla ya kwenda kupanda gari alipuliza filimbi na kutangaza wajawazito, wenye watoto na wazee wakae upande mmoja kisha wanapanda, atakayekiuka alimpiga kirungu.
Utaratibu huo anasema uliwasaidia madereva na kuhakikisha usalama wa vyombo vyao, kwani walikuwa na uhakika ikifika jioni kuna mtu anakwenda kuwasaidia kupanga watu.
Kuhusu ukamataji wahalifu anasema alikuwa akiwakusanya, kuwafunga mashati na kuwapeleka polisi wale waliokamatwa wakijihusisha na uvutaji wa bangi.
“Kipindi hicho mambo ya uuzaji ‘unga’ hayakuwa kama ilivyo kwa biashara ya bangi na gongo katika mitaa ambayo alikuwa anasimamia,” anasema.
Anasema alikuwa akijua vibanda vyote vilivyokuwa vinauza gongo na vichochoro kulikokuwa kukifanyika biashara ya bangi.
Anasema alipohamishiwa Oysterbay alimwambia hana uhakika iwapo atapaweza kwa sababu alishazoea kufanya kazi Wilaya za Ilala na Temeke, eneo la Keko.
“Mabadiliko hayo yalimpa wakati mgumu kwa sababu ya ugeni wa maeneo. Alihisi utendaji kazi wake ungepungua kutokana na mazoea ya sehemu za awali,” anasema.
Arafa anasema Mkama Sharp alihamishiwa Oysterbay mwaka 2001 ambako walipewa vyumba kwenye kota za polisi, wakati huo ghorofa jipya la makazi likiwa limezinduliwa.
Anasema wakati huo Mkama Sharp alikuwa na cheo cha Sajenti. Mwaka 2006 alikwenda kozi akapata nyota moja (Mkaguzi Msaidizi wa Polisi) ambayo hakuitumikia akaanza kuugua hadi alipofariki dunia.
“Alipotoka kozi alirudi kituoni kuripoti kabla ya kupangiwa kazi nyingine kutokana na kupata nyota moja. Aliporudi nyumbani hakukaa muda mrefu akaanza kuumwa hadi akafariki dunia,” anasema.
Kwa mujibu wa Arafa, alianza kuugua akiwa Chuo cha Polisi Kurasini na ikamlazimu kurudi nyumbani kila mwisho wa wiki.
“Alifanya hivyo hadi alipomaliza mafunzo, bahati mbaya siku anayomaliza sikuwepo nilikuwa Musoma kwenye msiba, nilikwenda kumwakilisha yeye,” anasema.
Anaeleza baada ya kumaliza kozi na kurejea nyumbani hali yake ilibadilika wakampeleka Hospitali ya Hindu Mandal, alikaa hapo siku mbili akaruhusiwa lakini baada ya wiki hali yake ilibadilika akapelekwa Hospitali ya Jeshi Lugalo alikofariki dunia Novemba 12, 2006. Alizikwa nyumbani kwao Musoma.
Kifo chake anasema kiliwashtua wengi kutokana na kutokuwapo taarifa kuhusu kuugua kwake, hivyo marafiki na wafanyakazi wenzake walifikiri ni cha ghafla.
“Wengi walikuwa na taarifa kuwa yupo chuoni, hivyo kwa kutokuonekana kwake wakajua bado yupo huko. Walipopata taarifa ya msiba walishangaa,” anasema.
Kutokana na taarifa za ghafla za kifo cha Mukama Sharp, anasema ofisi yake haikumuhamisha haraka kwenye nyumba hadi alipoomba kuondoka mwaka 2010.
“Nafikiri walikuwa wanajiuliza mambo mengi kutokana na utendaji kazi wa mume wangu, waliamua kuniacha kwani kwa kawaida mtu akifiwa na mumewe hakai muda mrefu analipwa mafao na kuondoka lakini mimi hadi niliomba mwenyewe,” anasema.
Arafa anasema alipoondoka alikwenda kupanga vyumba Kinondoni.
Baada ya kupata mafao ya mume wake, anasema alikarabati nyumba ya Mkama Sharp iliyopo Manzese, ambayo aliwaweka wapangaji pamoja na mwanaye mmoja.
Uchezaji muziki, korokoro
Anasema Mukama Sharp alipenda kucheza muziki, aliposikia bendi inapiga sehemu yoyote alikuwa anakwenda na wakati mwingine walikuwa wanakwenda wote.

Mkama Sharp mwenye shati la maua akiwa kwenye ukumbi wa DDC Kariakoo kwenye Muziki wa Msondo Ngoma.
Kutokana na mapenzi yake kwenye muziki anasema alianzisha kikundi cha Mchiriku mwaka 1987 kilichoongozwa na Halfan Mizoga kwa kushirikiana na vijana wengine.
Katika kutengeneza mazingira mazuri ya kazi na kuchukua tahadhari anasema walipokuwa maeneo wanayopiga muziki waliingiza mistari inayomuhusu Mkama Sharp wakiimba: “Kimbia, kimbia mbio mbio Mkama Sharp anakuja kimbia.”
Anasema wimbo huo ukipigwa baadhi ya vijana ambao hawakuwa na nia njema kwenye eneo hilo, wakiwamo wanaojihusisha na uhalifu walikuwa wakikimbia, huku Mkama Sharp akiingia na kucheza.
Si kikundi hicho wala wahudhuriaji walijua iwapo Mkama Sharp alikuwapo na vivyo hivyo alindoka pasipo wao kujua, anasimulia.
Kikundi hicho anasema kilidumu kwa miaka mitatu kikafa kwa sababu wahusika walianza kuuza vifaa na Mkama Sharp hakutaka kuendelea, akiwaeleza vijana hao ana majuumu mengine.
“Alipenda kucheza korokoro (mchezo wa bahati nasibu inayochezwa kwa kuchezesha dadu na kubashiri tarakimu) ambalo lilikuwa jirani na Kituo cha Msimbazi kulikuwa na supamaketi ya Imalaseko.
“Ili kujua alicheza mchezo huo nilikuwa naangalia mikono, nikiona rangi nyeusi najua alikuwa wapi. Lakini pia alikuwa akipata pesa anagawa kwa watu mtaani na wengine aliwanunulia vinywaji wapendavyo,” anasema.
Anasimulia kuwa Mkama Sharp alipenda kwenda baa ya Congo iliyokuwa maarufu wakati huo ikiwa Mtaa wa Congo na Nyati.
“Tukifika Congo baa watu wote walikuwa wanajua Mkama Sharp ameingia, tutakula hapo na vingine tunabeba kwa ajili ya watoto. Hakuwahi kukubali kubeba watoto kwenda nao baa kula, hivyo tuliwaacha nyumbani,” anasema.
Anasema hakuwa na upendo kwa ajili ya kujionyesha kwa watu ili aonekane mwema, kwani ulikuwa ni utaratibu wake kujitoa hata kwa familia.
“Alikuwa anapenda familia kuanzia yangu hadi yake, wakati mwingine alikwenda nyumbani kwetu anawapatia mahitaji muhimu, vikiwamo vyakula. Hakuwa akiniambia hadi niambiwe na ndugu zangu,” anasema.
Arafa anasema kwa kutambua kazi ya mumewe hakufikiri tofauti kuhusu kuwa na wanawake, japokuwa walikuwepo waliomtambia.
“Sikuwahi kumfumania lakini nilikuwa nikipata tambo zao. Wakati mwingine tukiwa wote namwambia leo huendi kwa wenzangu, alikuwa akicheka akisema nimeanza kusikiliza maneno ya watu, tunaishia kucheka,” anasimulia.

Mke wa Mkama Sharp, Arafa Hamis akiwa nyumbani kwake Chamazi, wilayani Temeke, Dar es Salaam.
Anasema alifanya hivyo kwa kuwa ni mzaliwa wa Kariakoo, Mtaa wa Msimbazi na tabia za wanawake wa eneo hilo kwa wakati huo alikuwa akizifahamu.
Arafa anasema mtoto wake mmoja ni askari polisi anayefanya kazi mkoani Mbeya, ambaye anaeleza amefuata nyayo za baba yake.
“Kila nikimtazama naona akifuata nyayo za baba yake hadi tabia kwenye kazi. Anacheka na kila mtu, nilipokwenda baadhi ya watu walikuwa wanamuelezea vitu ambavyo vilikuwa kwa baba yake,” anasema.