Watatu waliofariki kwa ajali Kimara watambuliwa, yumo kondakta wa daladala

Dar es Salaam. Miili ya watu watatu kati ya wanne waliyofariki katika ajali iliyohusisha lori lililohama njia na kuparamia kituo cha bodaboda kilichopo Kimara Stop Over jijini Dar es Salaam imetambuliwa, huku mmoja ikielezwa alikuwa ni kondakta wa daladala.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana Februari 14, 2025 ambapo lori hilo lilikuwa likitokea Morogoro kuelekea Dar es Salaam ambapo pia pikipiki 11 ziliharibiwa.

Moja ya viongozi waliofika muda mfupi baada ya kutokea ajali hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ambaye alisema kazi ya kuondoa miili iliendelea hadi saa 9:00 usiku wa kuamkia jana.

Chalamila alisema katika uokozi huo, walitoa pikipiki nyingi kuliko watu waliowakuta na kwa mantiki hiyo taarifa ya Polisi itaweka bayana.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Februrai 15,2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi  amewataja marehemu hao kuwa ni Emmanuel Kimbweleza (27) na Abbas Salum (23) madereva wa pikipiki na wakazi wa Kimara.

Mwili mwingine uliotambuliwa ni wa Adam Athuman (41), Mkazi wa Msongola, ambaye alikuwa kondakta wa daladala.

“Marehemu Adam wakati ajali hiyo inatokea alikuwa akisubiri usafiri kituoni hapo baada ya kutoka kupeleka gari kwa bosi wake maeneo hayo ya Kimara lakini kwa bahati mbaya umauti ndio ukamkuta hapo,” amesema Kamanda huyo.

Hata hivyo amesema mwili mmoja hadi sasa bado haujatambulika na kuutaja kuwa ni wa mwanaume.

Kuhusu majeruhi, Kamanda Kitinkwi alisema walikuwa sita, kati ya hao watatu bado wanaendelea kupata matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na watatu wamesharuhusiwa baada ya hali zao kuendelea vizuri.

Amewataja majeruhi ambao bado wapo hospitali kuwa ni Elizabeth Hamis, Ibrahim Kefa na Yahaya Mbailwa huku walioruhusiwa baada yakupata matibabu ni Hellen James, Bakari Hamis na Mahsin Sabaya wote wakazi wa Kimara.

Kuhusu bodaboda 11 zilizoharibiwa amesema bado wenyewe hawajajitokeza na zimehifadhiwa katika kituo cha Polisi Gogoni Mbezi.

Kwa upande wake Meneja uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi, amekiri taasisi hiyo kuwapokea majeruhi watatu Februari 14, 2025 wote wakiwa wa rufaa kutoka Hospitali ya Kimara.

Mvungi amesema Elizabeth mwenye miaka 17 aliyepokewa saa 6:02 usiku na kufanyiwa upasuaji wa Kichwa.

Wakati Ibrahim aliyepokewa hospitalini hapo saa 7:40 usiku alifanyiwa upasuaji wa miguu yote miwili, huku Yahya aliyepokelewa saa 8:05 usiku amefanyiwa upasuaji wa mguu wa kulia.

“Majeruhi wote hao kwa sasa hali zao wanaendelea vizuri,”alisema Mvungi.

Dereva wa lori bado anaswakwa

Katika ajali hiyo, dereva wa lori aliyesababisha ajali alitoroka baada ya tukio hilo.

Alipouliziwa kuhusu dereva huyo, Kamanda Kitinkwi amesema bado wanamsaka na wana imani watampata kwa kuwa ni mtu anayejulikana.

Kwa mujibu wa Shuhuda wa ajali hiyo, Aboubakar Rashid walieleza kuwa wakati ajali hiyo inatokea lori hilo halikuwa kwenye mwendokasi.

Hata hivyo Rashid alisema dereva alionekana kama mtu aliyekuwa usingizini kwani alikuwa kama mtu mwenye mawenge na aliposhtuka badala ya kukanyaga breki akakanyaga mafuta maana taa zilikuwa zimewaka nyekundu.

Related Posts