Moshi. Wazee wasiojiweza zaidi ya 60 wanaoishi Kijiji cha Msae Kinyambuo, pembezoni mwa msitu wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro (Kinapa), wamepatiwa mitungi ya gesi ili kuweza kutumia nishati safi na kuondokana na matumizi ya kuni ambayo huchangia uharibifu wa mazingira katika msitu huo.
Wazee hao wenye umri zaidi ya miaka 65 wamepatiwa mitungi hiyo na Mke wa Chifu wa Marangu, Frank Marealle ikiwa ni kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali za kuhamasisha nishati safi na kuwawezesha majirani zake kuondokana na matumizi ya nishati ya kuni, ambayo huwaathiri kiafya.
Akizungumza leo Februari 15, 2025 wakati wa kukabidhi gesi hizo, Rose Marealle amesema ameguswa kutoa nishati hiyo kwa wanawake wenzake wazee ikiwa ni moja ya jitihada za kulinda mazingira ya msitu unaowazunguka na kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
“Mimi niko karibu sana na msitu na hivyo katika kulinda hii misitu na mazingira nimeamua kutoa mitungi ya gesi kwa akinamama wenye umri wa miaka 65 na kuendekea ambao ni majirani zangu, ili kuwawezesha kutumia nishati safi na kuondokana na matumizi ya kuni,” amesema Marealle.
Ameongeza kuwa “Nimefanya hivyo ili kulinda huu msitu wa asili na kumuunga mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, kwani ukiangalia kina mama hapa kijijini kitu kikubwa ni kupika, hivyo nimeamua kuwapa hii mitungi ya gesi kuendeleza maisha yao kwa nishati safi”.
Akizungumza Frank Marealle amesema pamoja na nia njema ya serikali ya kulinda na kuitunza misitu, kumekuwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa misitu unaotokana na ukataji kuni, hivyo ili kusaidia kuondoa changamoto hiyo, wameamua kuwapa wazee wasiojiweza mitungi ya gesi.
“Baada ya kuhamia hapa Kinyamvuo tuliona pamoja na kwamba nia ya serikali ni kuulinda na kuutunza msitu huu unaotuzunguka, bado ipo changamoto ya ukataji miti kwa ajili ya kuni na wapo kina mama wazee ambao hawana uwezo wa kutumia nishati safi, hivyo leo tumeona tuwasaidie ikiwa ni sehemu ya sisi kuonyesha upendo kwao na kupunguza matumizi ya nishati ya kuni,” amesema Marealle.
Wakizungumza baadhi ya wanawake waliopata mitungi hiyo, mbali na kushukuru wameeleza namna ambavyo itawasaidia kuondokana na matumizi ya nishati chafu na kuwapunguzia gharama.
Dora Mgase mkazi wa kijiji hicho, amesema katika suala la kupika, kina mama wamekuwa wakiteseka na matumizi ya kuni kutokana na moshi na wengine hupata maradhi ya kifua na macho hivyo matumizi ya nishati safi yatahakikisha maisha yao yanakuwa salama.
“Kina mama tumekuwa tukiteseka sana wakati wa kupika kwani huku tunatumia kuni lakini msitu tuliokuwa tukiutegemea kukata kuni tumezuiliwa na serikali kuingia, hivyo kupata nishati ya kuni imekuwa ni shida. Tumefarijika sana leo kupewa chanzo kingine cha nishati ambacho itaturahisishia shughuli zetu za kupika,” amesema Mgase.
Janeth Mariki amesema “Tunamshukuru mama Marealle kwa kutuona sisi majirani zake na kutufanya marafiki, kwani serikali imekuwa ikihamasisha nishati safi lakini tulishindwa kumudu kununua, hali iliyotufanya tuendelee kuteseka na matumizi ya nishati ya kuni, kwani kutokana na mazingira ya upatikanaji wake msitu kuwa mgumu, wakati mwingine tunalazimika kutumia kuni mbichi hivyo moshi unatuumiza macho na kufanya chakula kunuka moshi”.
Naye, Mary Makyao amesema matumizi ya nishati safi yatawawezesha kupunguza gharama za maisha kwa kuwa mzigo mmoja wa kuni hugharimu Sh5000 ambao hutumia siku tatu lakini kwa sasa gesi waliyopewa wanaweza kuitumia hata mwezi mmoja.
“Tunamshukuru mama huyu kwa kutuona na kutuwezesha kutumia nishati safi, kwani mbali ya kupunguza gharama ametuokoa na maradhi ya kifua na macho yanayosababishwa na moshi wa kuni lakini pia kutuondolea adha tuliyokuwa tukikutana nazo pindi tunaingia msituni kuokota kuni,” amesema Makyao.
Ameongeza kuwa “Nishati safi inaturahisishia kupikia, waume zetu wataenda kazini kwa wakati na hata watoto wataenda mashuleni kwa wakati”