Simiyu. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahimiza wakulima wa zao la pamba kuongeza uzalishaji kwa ekari kwa kufuata kanuni bora za kilimo.
Kanuni bora za kilimo cha zao hilo ni uchaguzi wa mbegu bora, maandalizi ya shamba, upandaji wenye kufuata vipimo, palizi kwa wakati, udhibiti wa wadudu na magonjwa pamoja na kuvuna kwa wakati muafaka.
Akizungumza leo Februari 15, 2025 katika Wilaya ya Itilima alipokuwa mgeni rasmi katika utekelezaji wa ilani ya CCM kwenye Jimbo la Itilima, amesema wakulima wataweza kunufaika zaidi kutokana na zao hilo na kuchangia katika maendeleo ya viwanda vya pamba nchini.
Amesema Serikali kwa kuona umuhimu wa zao hilo katika msimu wa kilimo, imeamua kutoa bure pembejeo za zao hilo kupitia bodi ya pamba nchini.
“Zao la pamba tumeliwekea mkakati katika msimu huu ili kuhakikisha ya kuwa linaongeza thamani ili mkulima aweze kunufaika na Serikali imetoa bure pembejeo kwa wakulima,” amesema.
Majaliwa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, amesema kuwa ili zao hilo liweze kuzalishwa kwa tija wameongeza maofisa ugani kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT) ili kuhakikisha kila kijiji kina ofisa ugani ili waweze kuwafikia wakulima kwa urahisi.
Mbunge wa jimbo hilo, Njalu Silanga amesema wilaya hiyo imekuwa ikikabiliwa na uzalishaji mdogo wa pamba, ambapo kwa wastani wanapata kilo 200 kwa ekari moja badala ya kilo 1,500 zinazotarajiwa.
Amesema kuwa changamoto hiyo inatokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ukosefu wa mbegu bora, matumizi duni ya pembejeo, ukosefu wa elimu ya kilimo bora, na usimamizi hafifu wa kanuni za kilimo cha pamba.
“Sisi ni wazalishaji wakubwa wa zao la pamba, lakini changamoto kubwa tuliyonayo ni uzalishaji wa pamba kwa ekari moja kwa sasa tunazalisha kilo 200 badala ya kilo 1,500, ila kutokana na serikali kuwajali wakulima wa zao hilo tayari bodi ya pamba imeanza kuchukua hatua,” amesema.
Amesema zaidi ya wakulima 1,500 katika wilaya hiyo wamepatiwa bure vinyunyizi na viuatilifu kwa ajili ya kudhibiti wadudu waharibifu wa pamba.
Nao baadhi ya wakulima wamesema kuwa uzalishaji mdogo huo unachangiwa na baadhi ya viongozi kutotimiza wajibu wao katika kusimamia wakulima kufuata sheria na kanuni za kilimo cha pamba.
“Kuna ile kanuni ya zao la pamba kutochanganywa na mazao mengine kama vile mahindi, lakini cha kushangaza viongozi wetu tulionao hasa wa kisiasa kushindwa kusimamia sheria hiyo,” amesema Samweli Bomani, mkulima wa Kijiji cha Mitobo wilayani humo.
Pia, amesisitiza umuhimu wa viongozi kuwa mfano bora na kuhakikisha wakulima wanazingatia mbinu bora za kilimo ili kuongeza tija.
Naye Sophia Jilala, mkazi wa Kijiji cha Minato wilayani humo amesema ili kufikia malengo haya, inahitajika ushirikiano wa karibu kati ya wakulima, viongozi wa serikali za mitaa, wataalamu wa kilimo, na wadau wengine katika sekta ya kilimo.
Wilaya hiyo imeweka malengo ya kuzalisha tani milioni moja za pamba kwa mwaka 2024/ 2025.