AU yampongeza Rais Samia kuibeba ajenda ya nishati safi

Adis Ababa. Umoja wa Afrika (AU) umepongeza Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa ajenda ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Pongezi hizo zimetolewa leo Februari 16, 2025 na baraza la AU baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSSCC), Rais wa Kenya, William Ruto kupokea wasilisho la azimio la Dar es Salaam baada ya mkutano wa misheni 300 lililotolewa na Rais Samia.

Tanzania iliandaa mkutano huo wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu Nishati Afrika Januari 28, 2025.

Sambamba na pongezi hizo, Rais Samia amewasilisha ajenda ya nishati safi ya kupikia iliyopendekezwa na Tanzania katika Baraza la Umoja wa Afrika ambapo ameeleza nishati hiyo safi ya kupikia ni hitaji muhimu kwa watu milioni 900 barani Afrika ambao kwa sasa hawatumii nishati hiyo.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga leo imeeleza: “Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CAHOSSC Rais wa Kenya William Ruto, Rais Samia amewasilisha Azimio la Dar es Salaam na kueleza kuwa Afrika inapaswa kuendelea kushiriki kikamilifu kwenye majadiliano ya mabadiliko ya tabianchi, kutetea maslahi ya Afrika na kuhahakisha inakuwa na mbinu mpya za kutetea na kutumia rasilimali zake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Akipokea Azimio hilo, Rais Ruto amempongeza Rais Samia kwa kufanikisha Mkutano wa Misheni 300 na kikao kiliridhia azimio hilo kuwasilishwa kwenye Baraza la Umoja wa Afrika kwa ajili ya kupitishwa na baraza hilo ambapo lilipitisha azimio hilo bila kupingwa,”imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa; “Baraza hilo limemtambua na kumpongeza Rais Samia kama kinara wa ajenda hii barani Afrika.”

Hii si mara ya kwanza kwa Rais Samia kupigia chapuo matumizi ya nishati safi katika mikutano ya kimataifa, Novemba 29, 2024 akishiriki mjadala wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha alisema Tanzania inayo mikakati ya kuhakikisha inatumia nishati safi kwa kiwango kikubwa ikiwamo kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na umeme.

Aidha, Rais Samia alisema licha ya gharama kubwa za upatikanaji wa nishati safi, Tanzania imeweka mikakati ya vyanzo vya nishati hiyo.

Tanzania mjumbe kamati ya uongozi AU

Sambamba na hilo, Umoja wa Afrika umeichagua Tanzania kuwa mjumbe wa Kamati ya Uongozi wa Umoja wa Afrika (Bureua of the African Union Assembly) kwa mwaka 2025.

Kamati hiyo inaundwa na Angola kutoka Kanda ya Kusini (Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika 2025); Burundi kutoka Kanda ya Kati (Makamu wa Kwanza wa Mwenyekiti); Ghana kutoka Kanda ya Magharibi (Makamu wa Pili wa Mwenyekiti) na Tanzania kutoka Kanda ya Mashariki (Makamu wa tatu wa Mwenyekiti).

Aidha, Mauritania iliyokuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2024 kutoka Kanda ya Kaskazini itakuwa katibu wa kamati hiyo.

Related Posts