Fadlu awabakiza mastaa Simba Kambini

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema licha ya wachezaji kuwa katika fomu nzuri ya ushindani, lakini amegoma kuwapa mapumziko wakati mchezo wao na Dodoma Jiji ukiwa umeahirishwa kwa kuhofia kupoteza utimamu wa mwili kabla ya kuvaana na Namungo wiki ijayo.

Fadlu ameyasema hayo kutokana na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuahirisha mchezo wa Ligi Kuu baina ya timu hiyo na Dodoma Jiji uliotakiwa kuchezwa jana Jumamosi, kufuatia ajali iliyowapata Dodoma ilipokuwa ikitokea Lindi kucheza dhidi ya Namungo mapema wiki hii.

Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema Simba ipo katika kilele cha ubora na alitamani kuona wanaenda na ratiba, lakini kutokana na kilichotokea ataendelea kuwashikilia wachezaji ili waendelee kutengeneza utimamu.

“Huu ni mzunguko wa lala salama, utimamu wa wachezaji ndio chachu ya matokeo tunayoyapata ukifuatilia kila mchezaji anayepata nafasi ya kucheza sasa anapambana kuhakikisha tunafikia malengo.

“Wachezaji ukiwapa nafasi ya kupumzika hata kwa siku mbili tu, unaanza upya labda utoe ratiba ya mazoezi maalum kitu ambacho sio sahihi hasa duru hili, naamini wakitoka hata majumbani kwao wakifanya mazoezi mara moja kwa siku watakuwa kwenye ubora,” alisema Fadlu.

Kocha huyo alisema kwa sasa anaendelea na maandalizi kwa ajili ya mechi zilizo mbele yao bila kujali mchezo dhidi ya Dodoma Jiji utapangwa kuchezwa lini, anaamini akiwaandaa wachezaji wake wataendelea na ushindani na kupambania malengo yao.

“Malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo, huwezi kuwa bingwa kwa kushinda mechi nne, tunatakiwa kuendelea kukusanya pointi na kuhakikisha tunaweza pia kuzuia vizuri.

“Ushindani ni mkubwa, kila timu zinataka matokeo mazuri, kuna ambazo zinatafuta nafasi ya kubaki msimu ujao na nyingine zinapigana zisishuke daraja, hivyo utimamu wa mwili kwa wachezaji ni muhimu sana ili kuendana na kasi iliyo mbele yetu.”

Simba kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 47 baada ya kucheza mechi 18, ikizidiwa pointi mbili na Yanga inayoongoza msimamo ikicheza mechi 19.

Related Posts