Familia kijana anayedaiwa kuuawa yamwangukia IGP

Dar es Salaam. Wakati Mkuu wa Shule ya Sekondari Ipogolo, Mkoa wa Iringa alikohitimu kidato cha nne Elvis Mvano Pemba ikielezea maisha ya kijana huyo shuleni, familia yake imesema haiwezi kufungua kesi polisi mkoani Songwe kwa kuwa haina imani na jeshi hilo mkoani humo.

Familia ya Elvis imekwenda mbali zaidi na kuomba Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camillius Wambura kuwasaidia katika uchunguzi wa kifo cha ndugu yao ili polisi wanayedai amehusika na mauaji hayo achukuliwe hatua.

Elvis (19), alifariki dunia Februari 10, 2025 Mjini Tunduma mkoani Songwe na kuzikwa jijini Dar es Salaam Februari 14, 2025 huku ndugu wakidai kigogo wa polisi mkoani humo ndiye amehusika kwa mauaji yake kwa kile walichodai ni wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi mkoani Songwe Agustino Senga alipotafutwa na Mwananchi leo Jumapili Februari 16, 2025 simu yake iliita mara kadhaa bila kupokewa.

Februari 14, 2025 kamanda huyo alipoulizwa kuhusu madai ya familia kijana wao ameuawa na polisi mkoani humo alisema mwenye usahidi aupeleke akisisitiza maneno ni mengi juu ya kifo hicho.

“Huyu kijana alipigwa na watu wasiojulikana baada ya kuiba simu, hatuna uchunguzi mwingine zaidi ya huo, kama kuna mtu ana ushahidi kwamba ameuawa na polisi aulete na sisi polisi huwa tunachunguzana wenyewe kwa wenyewe, mwenye ushahidi aulete,” alisema.


Polisi lawamani kifo cha Elvis, baba aangua kilio msibani

Senga alisema Elvis aliuawa na watu wasiojulikana akidaiwa kuiba simu na kusisitiza mwenye ushahidi kwamba chanzo cha kifo hicho ni wivu wa mapenzi aupeleke polisi wafungue kesi, madai hayo yachunguzwe.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti leo Jumapili, Februari 16, 2025 mama na baba mkubwa wa marehemu wamesema wataendelea kupambana ili haki itendeke kwa waliohusika na kifo cha kijana wao wachukuliwe hatua.

Wamesema katika hilo, hawana imani na polisi mkoani Songwe wanakodai mhusika wa mauaji ya kijana wao ndipo yupo.

Mama wa marehemu, Veronica Mwang’onde huku akilia amesema:”Siwezi kufungua kesi Songwe wakati watuhumiwa wa mauaji ya mwanangu wako pale pale, sina imani nao katika hili, nahitaji msaada wa IGP.”

Akizungumzia kupotea kwa kijana wake, kisha kuonekana yuko na polisi na baadaye hospitali na kisha kuambiwa amekufa, mama huyo amesema alitoweka nyumbani Ijumaa (Februari 7) kisha akaonekana yupo na polisi.

“Mimi sikuwepo nyumbani, nilikuwa safarini, mjomba wake akaniambia Elvis hajarudi, nikasema si kawaida yake, tukaanza kumtafuta Jumapili akaonekana yuko na polisi hospitali, kisha wakaondoka naye hospitali akiwa taabani wakidai wana kazi naye na Jumatatu (Februari 10) tukaambiwa amekufa yupo mochwari,” amesema mama huyo.

Amesema pale mochwari mwili wa Elvis uliandikishwa kama mtu asiye na ndugu, huku Veronica akisema kama iliwezekana polisi walihoji Elvis akiwa mzima na kutaja majina yake, walishindwa kumhoji kuhusu ndugu zake au alikotoka?

“Akiwa polisi wanatuambia Elvis aliandika majina yake yote, swali la kujiuliza kama alikuwa na uwezo wa kutamka majina yake, ilishindikana vipi kueleza ndugu zake kama kweli alipelekwa pale baada ya kupigwa na watu wasiojulikana,” amehoji kwa uchungu mama huyo.

Amesema polisi waliwaambia Elvis aliiba simu aina ya Tecno na kupigwa na watu wasiojulikana, huku uchunguzi wao ndiyo ukiwa umeishia hapo wakati si kweli.

“Familia tunafahamu kigogo wa polisi hapa Songwe ndiye amehusika na mauaji yake kwa sababu ya wivu wa mapenzi, halafu hapo hapo ambapo tunajua ndipo kuna mtu aliyekatisha maisha ya mwanangu niende kufungua kesi, siwezi upata msaada,” amesema na kuongeza.

“Kama mzazi nilikuwa siruhusu kijana wangu awe kwenye mahusiano kwa umri wake, lakini alishakuwa kijana na kulikuwa na binti anatokea Tukuyu anakuja Tunduma, ndiye chanzo cha yote hadi kumsababishiwa kifo,” amesema mama huyo akimtaja kigogo wa polisi kuhusika.

Baba mkubwa wa marehemu, Eliud Pemba amesema tumaini lao kwa sasa ni kwa IGP kuingilia kati suala hilo ili haki ipatikane.

“Hatuna imani na polisi Songwe, majibu yao kuhusu kifo cha ndugu yetu ni mepesi kana kwamba maisha ya mtu hayana thamani.

“Hatutegemei kupata msaada kwa mkuu wa kituo Tunduma wala RPC Songwe, ni bora twende mbele zaidi, IGP atusaidie, ikimpendeza aandae watu wa kulichunguza hili ili ukweli ujulikane,” amesema.

Amesema wana ushahidi wa namna polisi walivyomchukua kijana wao na kuondoka naye kisha kutoa taarifa kwamba aliiba simu na baadaye kumpeleka hospitali, kisha kumtoa akiwa taabani na kumrejesha tena na kueleza amekufa.

“Polisi wanasema Elvis alipigwa na wananchi, lakini katika postmoterm (uchunguzi wa maiti) alivunjwa shingo na mbavu na alikuwa na majeraha miguuni, swali jepesi tu je? watu waliompiga walikuwa wakichagua maeneo hayo matatu tu ya kupiga,” amehoji.

Amesema katika miaka 19 ya maisha ya kijana wao, hajawahi kuwa na historia wizi kuanzia nyumbani, mtaani hadi shuleni alikosoma.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Ipogolo aliposoma Elvis, Yohannes Sanga akimzungumzia amesema hakuwahi kusikia tukio la wizi au utovu wa nidhamu kwa kijana huyo.

“Alimaliza kidato cha nne mwaka 2023, huyu dogo (Elvis), mama yake ni mtumishi wa benki, alikuwa mtulivu, sijawahi kumshuhudia tofauti, nilimfahamu hivyo,” amesema Mwalimu Sanga.

Amesema hata darasani alikuwa ni kijana mwenye uwezo, alikuwa mkimya na hakuwa na matukio ya ajabu katika kipindi chote cha masomo shuleni hapo hadi anahitimu kidato cha nne.

Related Posts