Dar es Salaam. Katika mchakato wowote wa malezi, adhabu inatajwa kuwa sehemu mojawapo ya mzazi au mlezi kumfunda mtoto vile anavyotaka.
Hata hivyo, changamoto inabaki ni wakati gani mtoto anapaswa kuadhibiwa, aina gani ya adhabu apewe na itolewe kwa namna ipi.
Ni kutokana na changamoto hii, si taarifa ngeni kusikia watoto wadogo ambao nasaha za mdomo zingetosha kuwaadabisha, wakiadhibiwa kwa kuchomwa moto au kupigwa vipigo vikali kiasi cha kuwasababishia majeraha, yakiwamo ya kudumu.
Aina mbalimbali za utafiti kuhusu malezi zimefanywa na wataalamu wa sikolojia, afya na elimu, ukiwamo uliowahi kufanywa na Chama cha Wanasaikolojia wa Marekani (APA) mwaka 2012 na kueleza kuwa adhabu isiyofaa inaweza kuwa na madhara ya kudumu kwa mtoto badala ya kumjenga, hasa kwa watoto chini ya miaka mitano.
Utafiti huo, ulionyesha kuwa adhabu kwa mtoto inapaswa kuwa yenye utu na huruma na kuwa watoto wa chini ya miaka mitano ni bora waelekezwe na si kupewa adhabu kali.
Aidha, watoto wachanga na watoto walio na miaka miwili mpaka mitatu, utafiti huo ulieleza kuwa, wanaelewa zaidi wakieleweshwa kwa njia ya mazungumzo na mifano na si kupewa adhabu kali.
Utafiti huo ukapendekeza kuwa ni bora kuepuka adhabu za vipigo, badala yake watoto waeleweshwe na kufundishwa polepole na kwa kutumia mifano.
Aidha, zipo tafiti zilizoenda mbali na kuzungumzia umri sahihi wa mtoto kuadhibiwa na miongozo inayotolewa na wataalamu kuhusu mbinu bora za kuadhibu watoto.
Utafiti wa jarida la ‘Child Development’ wa mwaka 2016, ulisisitiza umuhimu wa kumuelewesha mtoto wa miaka 3-5 na matokeo yake huwa mazuri, tofauti na kipigo au adhabu kali.
Kadhalika, utafiti wa jarida la ‘Family Psychology’ wa mwaka 2009 ulionyesha watoto wa miaka 6-12 wanaelewa vizuri na huwa na ufanisi ikiwa adhabu itatolewa kwa upole na kwa kuzingatia muktadha wa matendo yao.
Hii ni kwa sababu, watoto wa umri huu tayari wana uwezo wa kutambua jema, baya na kutambua makosa, ingawa bado wanahitaji uongozi wa wazazi au walezi wao, huku watafiti wakisisitiza adhabu wanazopewa ziendane na makosa waliyoyafanya ili lengo liwe kuelimisha zaidi kuliko kuumiza.
Mwanasaikolojia, Jacob Kilimbi anaeleza, unapotoa adhabu unapaswa kujua lengo la kuitoa adhabu hiyo.
“Wengi wanaadhibu kisa tu yeye amekasirika, lakini kiuhalisia adhabu hiyo inapaswa iwe na malengo, watoto wa umri wa miaka 0 hadi 10 wanajifunza zaidi kwa kuona mifano na kuiga baadhi ya vitu,” anaeleza.
Anasema, kama unampa mtoto adhabu kwa malengo ya kumfundisha akiwa na umri huo inaweza isifanye kazi, ila tu, itamfanya kuwa muoga katika mazingira fulani.
“Adhabu nyingi za Kiafrika ni viboko na adhabu nyingine za maumivu, kisaikolojia adhabu ya fimbo, mtoto huitumia kumtafsiri mtoa adhabu na si kosa alilolifanya,” anaeleza
Baada ya adhabu hiyo, Kilimbi anasema, watoto huanza kupoteza mshikamano kati yao na wazazi.
“Adhabu ngumu, humpotezea mtoto uwezo wa kufanya vitu tofautitofauti katika ukuaji wake,” anaeleza.
Kilimbi anaongeza kuwa, mtoto anapofanya baadhi ya vitu wazazi wengi hawajui kwa nini mtoto anafanya hicho anachokifanya. Katika umri huo watoto hufanya ubunifu kama namna ya kuonyesha vipawa vyao.
“Katika kuonyesha uwezo wake, wazazi wanapaswa wawe makini, watoto wengi hufanya vitu kama majaribio ya kuona matokeo kutokana na kukosa taarifa sahihi ya kile anachokifanya katika ubongo wake,” anasema.
Katika kipindi hicho, mtaalamu huyo anasema mtoto huhitaji taarifa sahihi tu, na kuwa hata ukimwadhibu, unapaswa umwelekeze anatakiwa kufanya vipi ili kiwe sahihi.
“Mweleweshe mtoto njia sahihi ya kufanya kile anachokifanya, na umpe adhabu isiyoumiza ila imfundishe kwa wakati husika,” anaeleza na kuongeza kuwa mtoto hana uwezo wa kutafsiri adhabu imetokana na nini, hivyo mzazi au mlezi unapaswa umuonyeshe kwa mfano.
Kilimbi anasema adhabu za vipigo zina madhara mengi kuliko faida.
“Tumezalisha watu wengi wasio na uwezo kutokana na adhabu zilizokuwa zikitolewa kipindi cha nyuma. Nchi za wenzetu kiupeo wametuzidi sana, na ni kutokana na kuua vipaji vya watoto wengi kwa kuvitafsiri vipaji hivyo kama utundu,” anasema.
Anaongeza kuwa, kuanzia umri wa miezi 18 hadi miaka 3 mtoto anajijengea uwezo wa kujitegemea mwenyewe kwa kujaribu baadhi ya vitu anavyofanya mzazi wake.
“Utakuta unaosha vyombo yeye anatia mchanga kwenye beseni, yote hayo ni katika kujitengeneza, ukimwadhibu unampa uwezo wa kuacha kujitegemea na kukutegemea wewe siku zote,” anaeleza.
Kuna umri utafikia utaanza kumfundisha, ila hataweza, kutokana na kile ulichomfanyia kilimuathiri.
Anasema, miaka mitatu hadi 10 ni kipindi cha mtoto kupenda kujichanganya na wenzake na kucheza nao.
“Miaka 0 hadi 2 ni kipindi cha mtoto kuamini watu walio karibu naye, miaka 3-5 mtoto huanza kujitegemea kwa kugundua vipaji alivyonavyo kwa kutengeneza vitu mbalimbali huku ikiashiria ubunifu,” anaeleza.
Anasema tatizo kubwa la wazazi wengi, kila anachofanya mtoto, wao hukitafsiri kiutuuzima, bila kuwaza kiutoto.
“Hiki kipindi ni cha kutoa maelekezo zaidi na mifano ili mtoto ajifunze,” anaeleza.
“Kupitia marufuku unazompa mtoto, vipigo na adhabu ngumu, unaua uwezo wa mtoto katika vitu mbalimbali, ambapo huanza kujifunza kwa kusikiliza mtu wake wa karibu. Mzazi unapaswa kuwa rafiki kwa mtoto ili akusikilize, na ikiwa kuna ulazima wa adhabu, basi mnyime kufanya vile vitu anavyovipenda ili ajifunze,” anaeleza.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Maadili Centre na mtaalamu wa malezi, Florentine Senya anasema mtoto wa miaka 0-5 huwa na tabia ya kudadisi na kugusa vitu, na kuwa umri huo ni wa kuzungumza zaidi na mtoto.
“Unapozungumza halafu asikuelewe, unampa adhabu za kawaida ambazo hazitamwathiri kisaikolojia,” anasema.
Katika makuzi ya mtoto, mzazi unapaswa kuzungumza, kushauri, kuelekeza na kuonya kuliko kutoa adhabu za kuumiza katika umri wowote.
“Wazazi wasitoe adhabu mara kwa mara, bila kuzungumza na mtoto, na kuwa akizoea hali hiyo atafanya mengi ya ajabu kutokana na kuwa sugu,” anasema.
Senya anasema, kwa wale wa rika la balehe wanahitaji zaidi elimu ya maisha kupitia kupewa nasaha na ushauri zaidi.
“Unapomshirikisha mtoto mambo halisi, mara nyingi anajifunza na kujutia mabaya anayoyafanya, hiki ndicho kipindi ambacho ukimfanyia mabaya, unampoteza mtoto, wakati anahitaji ukaribu zaidi kutoka kwa wazazi na si adhabu,” anasema.
Anasema, kipindi hiki, ndicho muhimu kumshirikisha mtoto kuhusu mafundisho ya dini na kuchambua zaidi yaliyowahi kutokea ili ajifunze.
“Tumia mifano katika familia, ukoo na majirani waliochezea maisha. Hii ni mifano halisi ya makosa mengi, umri wa ukuaji unahitaji msaada wa kimawazo na si adhabu. Mzazi unapaswa uongee naye ili apate uchungu na maumivu ya baadhi ya mifano uliyompa,” anasema.