Maajabu mawili bao la Zidane Azam

NYOTA mpya wa Azam FC, Zidane Sereri amefungua ukurasa wa mabao ndani ya kikosi hicho baada ya kutupia bao moja katika ushindi wa 2-0, dhidi ya maafande wa Mashujaa, huku kukitokea maajabu mawili wakati mshambuliaji huyo akiweka kambani.

Zidane aliyesajiliwa na kikosi hicho akitokea Dodoma Jiji, aliifungia Azam bao la utangulizi dakika ya 72 katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, huku lingine kali likifungwa na Yoro Diaby dakika ya 82.

Moja ya ajabu la bao hilo ni la kwanza kwake tangu ajiunge na Azam, akitokea Dodoma Jiji katika dirisha dogo la Januari mwaka huu, huku likiwa ni la mwisho aliloifunga pia Mashujaa wakati akiwa na kikosi hicho cha ‘Walima Zabibu’.

Kabla ya nyota huyo kujiunga na Azam, bao lake la mwisho kufunga akiwa na Dodoma Jiji ambalo lilikuwa la tatu kwake msimu huu, alilifunga kwenye mchezo na Mashujaa ambao kikosi hicho kilishinda kwa mabao 3-1, Desemba 28, mwaka jana.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma mbali na Zidane aliyefunga, ila mengine yalifungwa na Heritier Lulihoshi na Mwana Kibuta, huku lile la kufutia machozi kwa upande wa Mashujaa likifungwa na Crispin Ngushi.

Sasa wakati nyota huyo amejiunga na Azam, bao lake la kwanza amelifunga pia dhidi ya Mashujaa ikiwa ni mwendelezo wa pale alipoishia akiwa na kikosi cha Dodoma Jiji na kumfanya kufikisha jumla ya mabao manne hadi sasa ya Ligi Kuu Bara.

Akizungumzia bao lake la kwanza ndani ya kikosi hicho, Zidane alisema ni furaha kwake kwani imemuongezea hali nzuri ya kujiamini, licha ya kukiri ushindani ni mkubwa, hivyo anapaswa kupambana ili kuendelea kuaminiwa na benchi la ufundi.

“Kama mshambuliaji unapofunga lazima ujisikie vizuri lakini nikiri wazi hapa nilipo ni tofauti na nilipotoka, ushindani ni mkubwa na kila mchezaji anaonyesha kiwango kizuri mazoezini, kocha ananiamini na sitaki kumuangusha akinipa nafasi.”

Related Posts