Majaliwa: Rais Samia ni tiba ya maendeleo

Maswa. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni tiba ya maendeleo, hivyo Watanzania wanapaswa kwenda naye kwa kuwa ataifikisha nchi kule kunakotarajiwa.

Majaliwa ambaye pia ni Waziri Mkuu amesema Rais Samia ni kiongozi anayeona, kusikiliza na kutatua changamoto za Watanzania kwa ustadi wa hali ya juu na amedhihirisha hilo katika kipindi chake cha uongozi.

Amesema CCM inaendelea kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025, huku akisisitiza wagombea wa chama hicho wataingia kwenye uchaguzi wakiwa na rekodi thabiti ya utekelezaji wa Ilani ya chama.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Februari 16, 2025 wakati Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho Maswa Mashariki, uliofanyika katika uwanja wa nguzo nane, Maswa mkoani Simiyu.

“Rais Samia kwa uwezo wake na maono yake ameonesha anadhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania, wote tumeshuhudia nia yake ya kusimamia utekelezaji wa miradi katika sekta mbalimbali za maendeleo na tumeona namna alivyosimamia kukamilisha miradi yote ya kimkakati.”

Akizungumzia sekta ya maji, Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha inatekeleza miradi mikubwa ya maji kutoka katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na upatikanaji wa majisafi na Salama.

“Mpango wetu ni kuendelea kufikisha huduma ya maji mpaka vitongojini,”amesema.

Majaliwa amesema katika sekta ya afya, Serikali imeendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuhakikisha huduma zinaimarishwa na kuwapunguzia adha wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata tiba.

Amesema ili kuhakikisha huduma ya upatikanaji wa umeme inaimarika nchini, Serikali imeendelea kutekeleza miradi umeme.

“Tumeshafikisha umeme karibu asilimia 99 kwenye vijiji vyetu, sasa tunakwenda vitongojini,”amesema

Wakati huohuo, Majaliwa  amesema chama hicho kipo imara na kinaendelea kuwahudumia Watanzania. 

Amesema kutokana na sera imara zinazotekelezeka za chama hicho, kimeendelea kufikisha huduma na mahitaji muhimu kwa Watanzania 

“Chama hiki wakati wote kimesimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, kinafikisha huduma ambazo wewe Mtanzania kila ukiamka ni lazima uzitumie, chama hiki pia kimeendelea kusimamia amani na utulivu nchini,” amesema Majaliwa.

Pia, amesema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, CCM itaendelea kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana, ili wagombea wa chama wasiwe na kazi kubwa ya kueleza waliyoyafanya, bali waombe kura tu.

“CCM ni chama kikubwa, chama pendwa na chama kinachoaminiwa. Kina sera zinazotekelezeka, kikiahidi, kinatekeleza. Wanamaswa, leo mpo hapa na Mheshimiwa Nyongo (Mbunge wa Maswa Mashariki), anawapasha yanayotekelezwa ili mgombea wetu atakapofika hapa, kazi yake iwe ni ndogo ya kuomba kura,” amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema wakati wa kampeni, mgombea urais wa CCM, Samia na mgombea mwenza wake, Dk Emmanuel Nchimbi, watafika Maswa kuzungumza na wananchi na kueleza mipango yao kwa miaka mitano ijayo.

“Wakati wa kampeni, mheshimiwa Rais Samia na mgombea mwenza wake Dk Nchimbi watakuja Maswa kuomba ridhaa yenu. Tunataka kazi yao iwe nyepesi kwa sababu tayari mmeona kazi nzuri iliyotekelezwa,” amesema. 

Amesema kupitia Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Nchini Vijijini (Ruwasa), Maswa imetekeleza miradi yenye thamani ya Sh 2.68 bilioni na ongezeko la upatikanaji wa maji limefikia asilimia 81 kutoka asilimia 74.3.

“Katika Kijiji cha Ipililo, umetekelezwa mradi wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 1.32,”amesema Majaliwa.

Amesema katika sekta ya nishati wamefanikiwa kupokea mradi wa Wakala wa Nishati vijijini wenye thamani ya shilingi bilioni 2.79 ambazo zilitumika kuunganisha umeme katika vijiji vyote 56 na vitongoji 117 jimboni humo.

Stanslaus ambaye ni Naibu Waziri wa Mipango na Uwekezaji amesema kuwa Serikali imetoa Sh1.57 bilioni kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya na kukamilisha miundombinu ya afya.

Mbunge wa Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo amesema Wilaya ya Maswa imepokea fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta ya elimu, maji, afya, barabara, umeme na kilimo.

Related Posts